1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

ECOWAS yaidhinisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Niger

11 Agosti 2023

Viongozi wa Afrika Magharibi wameidhinisha kutumwa kile wanachosema ni kikosi cha dharura kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger, uvamizi ambao utafanyika haraka iwezekanavyo kumrejesha madarakani Rais Bazoum.

https://p.dw.com/p/4V1PV
Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen zu Niger-Putsch
Picha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Akizungumza baada ya kurejea kutoka mkutano wa kilele wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Uchumi wa Afrika Magharibi (ECOWAS) uliofayika mjini Abuja nchini Nigeria siku ya Alkhamis (Agosti 10), Ouattara alisema wakuu wa majeshi ya nchi hizo wangelifanya mikutano mingine kujadiliana hatua zinazoendelea kwenye kampeni hiyo ya kijeshi dhidi ya watawala wa kijeshi wa Niger.

Bila ya kuzitaja hatua hizo kwa undani, rais huyo wa Ivory Coast aliongeza kuwa wao kama viongozi wakuu wa wa nchi walishatoa idhini ya kuanzisha operesheni na kwamba nchi yake itachangia wanajeshi zaidi ya 1,000, ambao watashirikiana na wenzao wa Nigeria, Benin na mataifa mengine wanachama wa ECOWAS.

Soma zaidi: ECOWAS waamua kujizuia kuingilia kati kijeshi Niger

Ouattara alisema viongozi wa jumuiya hiyo "wamedhamiria kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum" aliyepinduliwa na wanajeshi wiki mbili zilizopita.

Mapema jioni ya Alkhamis, Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Omary Touray, alitangaza kutumwa kwa wanajeshi wa jumuiya hiyo nchini Niger. 

Marekani, Ufaransa zaunga mkono

Uamuzi huo wa ECOWAS uliungwa mkono na Marekani na Ufaransa, mataifa mawili ya Magharibi yenye maslahi makubwa na ya moja kwa moja kwenye taifa hilo la Ukanda wa Sahel. 

Nigeria Abuja | ECOWAS-Treffen zu Niger-Putsch
Rais wa Kamisheni ya ECOWAS Omar Touray (kushoto) akimpokea Rais Alassae Ouattara wa Ivory Coast kuhudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa ECOWAS mjini Abuja, Nigeria. kuzungumzia suala la Niger.Picha: KOLA SULAIMON/AFP

"ECOWAS, jumuiya inayokusanya mataifa ya Afrika Magharibi, ina jukumu muhimu la kuhakikisha amri ya kurejesha utawala wa kikatiba na tunaunga mkono kikamilifu uongozi na kazi ya ECOWAS kwenye hili." Alisema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken.

Soma zaidi: Viongozi wa Niger wakutana na wajumbe kutoka Nigeria kabla ya mkutano wa ECOWAS

Kwa upande wake, mkoloni wa zamani, Ufaransa, imesema kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni kwamba inaunga mkono kikamilifu uamuzi wote uliofikiwa na viongozi wa Afrika Magharibi.

"Ufaransa inarejelea msimamo wake kulaani vikali jaribio la mapinduzi linaloendelea nchini Niger na pia kuzuiliwa kwa Rais Bazoum na familia yake." Ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na wizara hiyo.

Hapo awali, Rais Bola Tinubu wa Nigeria, ambaye nchi yake ndiyo inayoshikilia uwenyekiti wa muda wa ECOWAS, alikuwa amesema bado upo uwezekano wa kulimaliza suala hili kwa njia ya amani, na kuirejeshea Niger demokrasia na utulivu wake. 

Wanajeshi waunda serikali mpya Niger

Licha ya uamuzi huo wa ECOWAS, utawala mpya ya kijeshi mjini Niamey ulikuwa unaendelea kuchukuwa hatua za kujiimarisha madarakani na kupuuzia miito yoyote ya kimataifa kwa kuteuwa baraza jipya la mawaziri.

Ecowas-Treffen in Nigeria | Bola Tinubu
Rais wa Nigeria na mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS, Bola Tinubu.Picha: Gbemiga Olamikan/AP/dpa/picture alliance

Baraza hilo lenye wajumbe 21 litaongozwa na Waziri Mkuu Ali Mahaman Lamine Zeine, mwenyewe akiwa kiongozi wa kiraia aliyewahi kushikilia nafasi za uwaziri wa fedha na uchumi katika serikali za zamani.

Soma zaidi: Wanajeshi Niger watangaza baraza la mawaziri

Wizara za ulinzi na mambo ya ndani zitashikiliwa na wanajeshi.

Viongozi hao wa kijeshi walishakaidi onyo la awali la ECOWAS iliyokuwa imewapa hadi Jumapili iliyopita wawe wameshamuachilia huru na kumrejesha madarakani Rais Bazoum, ama wakabiliwe na hatua za kijeshi. 

Bado kunangojewa kauli au hatua mpya ya Mali, Burkina Faso na Guinea, ambazo nazo pia zinaongozwa na wanajeshi na ambazo pia zimesitishwa uanachama wao wa ECOWAS. 

Awali mataifa hayo yalishasema kwamba hatua yoyote ya kuivamia Niger kijeshi itachukuliwa kuwa ni tangazo la vita dhidi yao pia, kauli ambayo inatishia kuliingiza eneo zima la Afrika Magharibi kwenye mzozo mkubwa wa kijeshi.

Vyanzo: AFP, AP, Reuters