1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

ECOWAS wasitisha mkutano muhimu wa kijeshi juu ya Niger

12 Agosti 2023

Mataifa ya Afrika ya Magharibi yameusitisha mkutano muhimu wa kijeshi juu ya mzozo wa Niger, siku moja baada ya kusema yangelituma kikosi cha dharura kumrejesha madarakani Rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum.

https://p.dw.com/p/4V5ZE
Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS
Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWASPicha: Gbemiga Olamikan/AP/picture alliance

Wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, walikuwa wakutane leo katika mji mkuu wa Ghana, Accra, kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi kwenye jumuiya hiyo. Lakini jioni ya jana, kulitolewa tamko la kuuakhirisha mkutano huo kwa muda usiojulikana.

Soma zaidi: ECOWAS waamua kujizuia kuingilia kati kijeshi Niger

Vyanzo hivyo vinasema mkutano huo ulikuwa umeandaliwa ili kuwaeleza viongozi wa ECOWAS juu ya "njia bora zaidi" za kuunda na kutuma kikosi hicho cha dharura nchini Niger. Bado ECOWAS haijafafanuwa undani wa kikosi hicho wala ratiba ya hatua zake, huku viongozi wake wakisisitiza kuwa bado wanataka suluhisho la amani. Ahirisho la mkutano huo lilitangazwa wakati maelfu ya wananchi wa Niger wakikusanyika kuunga mkono jeshi lao mbele ya kituo kimoja cha jeshi la Ufaransa jana Ijumaa. Mkoloni huyo wa zamani ana wanajeshi zaidi ya 1,500 nchini humo.