1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC imekua rasmi mwanachama wa saba wa EAC

8 Aprili 2022

Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata mwanachama mpya wa saba baada ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kujiunga rasmi.

https://p.dw.com/p/49gNh
Staatsbesuch von Präsident Uhuru Kenyatta in der Demokratischen Republik Kongo
Picha: Presidential presse office DRC

Kenya ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rais wa Kongo Tshisekedi aliye ziarani Kenya kwa siku mbili alitia rasmi saini mkataba wa uanachama. Hafla hiyo ilifanyika kwenye hema kubwa jeupe lililokuwa na nakshi za bendera za nchi wanachama na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bendi ya Ikulu ya Nairobi iliwatumbuiza wajumbe kwa miziki ya Lingala na kuwaenzi wasanii mashuhuri wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Nchi hiyo, sasa imejiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa mwanachama wa saba. Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jumuiya hiyo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi imetimiza vigezo vyote vya kuwa mwanachama wa EAC. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alisisitiza kuwa wakaazi wa jumuiya wana mengi yanayowaunganisha ikiwemo lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Antoine Tshisekedi amepokea vizuri tukio hilo ambalo amelitaja kuwa la kihistoria. Kwenye hotuba yake alisisitiza kuwa upo umuhimu wa ushirikiano hasa katika masuala ya biashara, kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi na kudumisha amani.

Raia wa DRC wanataka zaidi usalama

Kwa kujiunga na jumuiya, Wakongo wanataka si tu kufurahia matunda ya ushirikiano wa biashara bali kudumisha kwanza uhusiano uliojikita kwenye amani na usalama kwa wote. Kauli hizo zinaungwa mkono na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dokta Peter Mathuki.

Staatsbesuch von Präsident Uhuru Kenyatta in der Demokratischen Republik Kongo
Rais Felix Tshisekedi na mwenyeji wake Uhuru KenyattaPicha: Presidential presse office DRC

Hii ni ziara rasmi ya Tatu ya Rais Tshisekedi nchini Kenya. Rais Tshisekedi anatazamiwa kuhudhuria Kikao cha viongozi hapo kesho tarehe 9 kitakachowaleta pamoja wawakilishi wa Kenya, Rwanda na Uganda. Tshisekedi amesindikizwa na mawaziri wa masuala ya kigeni, kilimo, uvuvi na ufugaji. Kwa upande mwengine, kwenye kikao cha 19 cha marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha mwishoni mwa Machi mwaka huu, viongozi hao waliridhia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo iliyo na utajiri mkubwa wa rasilimali iwe mwanachama. Samia Suluhu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Soma zaidi: Jamii ya Batwa washambuliwa mbuga ya Kahuzi-Biega

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ndiyo nchi kubwa zaidi kwenye eneo lililo Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika. Kongo inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati ambapo kitisho cha uasi bado kinashuhudiwa kwenye eneo la mashariki. Ifahamike kuwa waasi wa M23 walioko mashariki ya Kongo walitiliana saini na serikali kuu mwaka 2009 kubwaga silaha ila bado mwafaka unaregarega. Jumuiya ya Afrika Mashariki iliasisiwa Mwaka 1967, ikasambaratika baada ya miaka kumi na kufufuliwa upya Mwaka 2000.

DW Nairobi.