1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 kuendelea kwa wiki au miezi kadhaa, Robert Koch

31 Machi 2020

Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani Robert Koch imetoa tahadhari kuwa janga la corona litaendelea kwa wiki na hata miezi kadhaa. Idadi ya maambukizi ulimwenguni kote sasa imepindukia 780,000.

https://p.dw.com/p/3aF03
Berlin - Lothar Wieler während PK
Picha: picture-alliance/dpa/C. Koall

Visa vya maambukizi ya virusi vya corona vilivyoripotiwa ulimwenguni kote vimepindukia 780,000, huku vifo vikiwa zaidi ya watu 37,000. Hayo yanajiri wakati taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani Robert Koch ikitoa tahadhari kuwa janga la corona litaendelea kwa wiki na hata miezi kadhaa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Lothar Wieler ambaye ni mkuu wa taasisi inayodhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani Robert Koch, ametoa onyo hilo kuwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 utaendelea kuhangaisha nchini Ujerumani kwa wiki au miezi kadhaa na hivyo kuhimiza kuwa mikakati ya kuwalinda watu walioko katika hatari kubwa ya maangamizi itaendelea pamoja na kuimarisha utoaji huduma za afya.

Hayo yanajiri wakati mji wa Jena ulioko mashariki mwa Ujerumani ukiwa wa kwanza kutangaza kuwa ni sharti kwa kila mtu kuvaa barakoa  kila anapoingia katika maduka au wanapotumia usafiri wa umma mjini humo. Hiyo ikiwa miongoni mwa njia za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Onyo la Beki Kuu ya Dunia

Wataalam hawajafaulu kupata tiba au chanjo dhidi ya virusi vya corona.
Wataalam hawajafaulu kupata tiba au chanjo dhidi ya virusi vya corona.Picha: picture-alliance/M. Schönherr

Kwingineko, Benki Kuu ya Dunia imeonya kuwa mdororo wa uchumi unaosababishwa na mripuko wa ugonjwa wa COVID-19, huenda utasitisha kabisa ukuaji wa uchumi wa China, hali itakayowaingiza zaidi ya watu milioni 11 mashariki mwa Asia kwenye umaskini.

Nchini India, maafisa leo wameyafunga makao makuu ya kundi la kimishonari la Kiislamu, na kuamuru uchunguzi ufanywe dhidi ya madai kuwa kundi hilo liliandaa mikutano ya kidini, ambayo maafisa wa serikali wanahofia ilisababisha watu kadhaa kuambukizwa virusi vya corona.

Bado tukisalia nchini India, maafisa wa polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafanyakazi waliokaidi amri ambayo imetangazwa nchini humo ya kutokuwepo nje ili kuzuia ueneaji wa virusi vya corona. Amri hiyo imewaacha maelfu kwa maelfu ya watu nchini humo bila kazi.

Kufikia leo, jumla ya watu walioambukizwa virusi vya corona ulimwenguni imepindukia watu 780,000. Zaidi ya watu 37600 wamefariki kutokana na virusi hivyo huku zaidi ya watu 165,300 wakiwa wamepona.

Maambukizi yaendelea kuongezeka Marekani

Visa 780,000 vya corona vimeripotiwa ulimwenguni
Visa 780,000 vya corona vimeripotiwa ulimwenguni Picha: Reuters/F. Lo Scalzo

Marekani inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walioambukizwa, takwimu zikionyesha kuwa wagonjwa nchini humo kwa sasa ni 164,274.

Italia ndiyo inaongoza kwa idadi ya vifo ulimwenguni kote ikiwa imeripoti jumla ya vifo 11,591.

Bendera nchini Italia na Uhispania zinapepea nusu mlingoti kuwaomboleza waliofariki.

Tangu mlipuko huo ulipoanza mwezi wa Disemba nchini China, maambukizi yameripotiwa katika zaidi ya nchi 200, ikiwemo bara la Afrika ambalo limeripoti visa 5,000.

Vyanzo: RTRE, AFPE, DW