1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona yaendelea kulisakama bara la Ulaya na Marekani

Saleh Mwanamilongo
6 Novemba 2020

Ujerumani imethibitisha maambukizi mapya zaidi ya 21,000 ndani ya siku moja,Huku nchi nyingine barani Ulaya zikizidisha hatua za kupambana na maambukizi.

https://p.dw.com/p/3kwc0
Coronavirus in Europa | Deutschland
Picha: Rupert Oberhäuser/picture alliance

Ujerumani imethibitisha maambukizi mapya ya virusi vya corona zaidi ya 21,000 ndani ya siku moja, ikitajwa kuwa ni kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa. Huku nchi nyingine barani Ulaya zikizidisha hatua za kupambana na maambukizi.

Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini ya Robert Koch, imesema leo Ijumaa kwamba ya maambukizi imefikia 21,506 kwa muda wa saa 24, kutoka 19 elfu siku moja iliopita.

Hadi asubuhi ya leo, Ujerumani imethibitisha visa laki 6 na 19 elfu tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona, huku watu 11,096 tayari wamekufa. Ingawa hali inayoendelea Ujerumani inaitia hofu serikali, mataifa mengine mengi ya barani Ulaya yanatajwa kuwa katika hali mbaya zaidi.

Maambukizi yaongezeka Ulaya

Uingereza imeanza kutekeleza hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na amri ya watu kubakia majumbani.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alitoa mwito wa pamoja kwa ajili ya kupambana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona. Huku Uingereza ikiweka amri ya watu kubakia nyumbani na kufungwa kwa biashara kwa kipindi cha wiki nne. Hatua sawa na hizo pia zinazingatiwa Uskochi, Wales, na Ireland ya Kaskazini.

Ufaransa, kuanzia leo imepiga marufuku migahawa na huduma ya chakula cha kuondoka nacho pamoja na kuuzwa kwa pombe kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi.

Nchini Italia, amri ya watu kutotoka nje usiku imeaanza kutekelezwa leo katika majimbo kadhaa. Hatua hiyo inatokana na tahadhari iliyotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, kuhusu ongezeko la maambukizi barani Ulaya.

Rekodi mpya ya maambukizi Marekani

USA Wahlen 2020 | Stimmauszählung in Atlanta Georgia
Picha: Tami Chappell/AFP

Marekani iliorodhesha idadi ya juu ya maambukizi ambayo ni zaidi ya 120,000 kwa muda wa saa 24, kwa mujibu wa hospitali ya Johns Hopkins. Marekani inaendelea kuongoza kwenye idadi ya watu waliokufa kutokana na corona ,ikiwa ni zaidi ya watu laki 234.

Kwingineko, Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, amejiweka karantini baada ya mtu wa karibu yake kuripotiwa kuwa na virusi vya corona. Ugiriki iliamuru watu kubaki nyumbani kwa kipindi cha wiki tatu, licha ya kwamba nchi hiyo ina idadi ndogo ya visa vya corona ukilinganisha na mataifa mengine ya Ulaya.

China inachukuwa hatua mpya dhidi ya wasafiri kutoka Ulaya. Brazil, ni nchi ya pili duniani baada ya Marekani ambayo imaethiriwa sana ikiwa na vifo zaidi ya laki moja na 61 elfu. Ikifuatiawa na India ambayo tayari ina vifo zaidi ya laki moja na 24 elfu.