1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP26 yaanza kuonyesha mafanikio

2 Novemba 2021

Zaidi ya viongozi 100 wa serikali na mataifa ulimwenguni wameahidi kuhitimisha tatizo la ukataji miti ambao wanasayansi wanasema ni chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/42TXP
Vor UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: picture alliance/dpa/AP POOL

Aidha wakuu hao wamsema watahakikisha wanakabiliana na tatizo la mmomonyoko wa udongo ifakapo mwishoni mwa muongo huu kwa ahadi ya dola bilioni 19 zitakaziowekezwa kwa ajili ya ya kulinda na kuendeleza misitu. 

Haya ni miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa na wakuu wa mataifa walioko Glasgow Scotland kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP26. Uingereza imesifu hatua hiyo ya uwajibikaji, na kuitaja kama moja ya mafanikio katika mkutano huo.

Zaidi ya dola bilioni 19 zilizoahidiwa zitawekezwa kwenye mifuko ya umma na binafsi ili kutekeleza mkakati huo unaoungwa mkono na mataifa kama Brazil, Indonesia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zenye asilimia 85 ya misitu ulimwenguni, pamoja na China, Colombia, Urusi na Marekani.

Soma Zaidi: Viongozi COP26 waahidi juhudi mpya kuokoa misitu ya dunia

Azimio hilo la Matumizi ya Misitu na Ardhi linahusisha misitu ya takriban maili milioni 13 za mraba, hii ikiwa ni kulingana na taarifa hiyo iliyochapishwa na ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, kwa niaba ya viongozi hao.

G20-Gipfel in Italien
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameahidi kuunganisha juhudi za kutekeleza azimio la utunzaji wa misitu katika mkutano wa COP26Picha: Yevgeny Paulin/Russian Presidential Press/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema baada ya azimio hilo kwamba wanataraji utekezaji wake utazisogeza pamoja pande zote zenye maslahi na uhifadhi wa misitu, na bila shaka itasaidia kutimiza malengo ya kupunguza viwango vya gesi ya ukaa

"Urusi inaunga mkono rasimu ya tamko la pamoja kuhusu misitu na matumizi ya ardhi lililopendekezwa kuidhinishwa katika mkutano wa leo. Tunatarajia utekelezaji wake kuwezesha ushirikiano wa karibu kati ya mataifa yote yenye nia ya kuhifadhi misitu. Hii bila shaka itatumika kutimiza malengo ya kupunguza viwango vya kaboni katika anga kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Paris." alisema Putin.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa upande wake amesema Tanzania kama mataifa mengine inaathirika na mabadiliko ya tabianchi, huku akiyakosoa mataifa makubwa kwa kulegalega wakati mataifa yanayoendelea kama Tanzania yanaonyesha uongozi katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

UN-Generalversammlung | Tansanias Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa COP26. Ameyahimiza mataifa yaliyoendelea kuonyesha uongozi katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchiPicha: Wang Ying/Xinhua/picture alliance

Soma Zaidi: Barua kutoka Dar: Je mkutano wa COP26 italeta ahueni ?

Alisema, "Nchini Tanzania hatujayaepuka matukio haya. Kuongezeka kwa kina cha bahari kunatafuna ardhi ya kilimo, fahari yetu, Mlima Kilimanjaro, unazidi kuwa na upara kutokana na kuyeyuka kwa barafu na tunakumbwa na mafuriko na ukame usiotabirika."

Amewatolea mwito viongozi wenzake kusaidia ufadhili wa miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili kufikia malengo yaliyopangwa.

Aidha, mataifa matano ambayo ni pamoja na Uingereza na Marekani pamoja na kundi la taasisi za kiutu ulimwenguni hii leo wameahidi kuidhinisha kiasi cha dola bilioni 1.7 zitakazowasaidia watu wa asili kuendeleza uhifadhi wa misitu na kuimarisha haki zao za ardhi.

Wanaharakati wa mazingira wanasema jamii za asili zina uwezo mkubwa wa kulinda misitu na kupambana na wavamizi wa ardhi na waharibifu wa misitu.

Soma Zaidi: Guterres: Iokoweni dunia ama tutaangamia sote

Mashrika: APE/RTRE