1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: Je mkutano wa COP26 utaleta ahueni?

1 Novemba 2021

Jamii zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa, hasa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, hazitarajii mipango ya kuaminika kuanza hivi karibuni anaandika Anaclet Rwegayura katika Barua kutoka Dar.

https://p.dw.com/p/42RBp
Global Ideas Simbabwe Elefanten
Picha: Columbus Mavhunga

Haya ndiyo maoni wanayotoa wakati viongozi wa dunia wakijumuika Glasgow, Scotland, kwa ajili ya Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, maarufu kama COP26. Mbali ya yote, wengi wao huamini kwamba hali nzuri au mbaya ya hewa, ikiwa pamoja na athari za ongezeko la joto duniani, ni matokeo ambayo mwanadamu hawezi kubadili au kuathiri.

Ukame unapokausha mimea yao au mafuriko kuharibu kila kilichooteshwa kwenye mashamba yao, wao husema tu ni kwa sababu ya kisasi cha Mungu kwa dhambi zinazotendwa na watu wabaya. Kisha wanatarajia kupata mavuno mazuri msimu unaofuata.

Wakati nchi za mabara tofauti zinavyopitia athari za ongezeko la joto duniani, kutoka joto kali hadi moto usioweza kudhibitiwa na kukauka kwa vyanzo vya maji, kila mtu lazima awe na wasiwasi juu ya ulimwengu ujao na kutambua haja ya kubadilisha jinsi tunavyotumia mazingira ya asili.

Katika hatua hii Afrika inahitaji uongozi wenye uelewa wa hali ya hewa na kutambua athari za ongezeko la joto linalozungumzwa sana kufikia shabaha ya nyuzi joto 1.5 ya Mkataba wa Paris.

Uganda Ölförderung Umwelt Indigene Total
Eneo la msitu nchini UgandaPicha: Jack Losh

Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Afrika Kusini mwa Sahara ni eneo dogo kabisa katika uchangiaji wa hewa ukaa duniani, chini ya asilimia tano, lakini ndilo linaathirika zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Ni uhaba wa uongozi wa kisiasa wenye maono, kabla ya sababu nyingine yoyote, ambao utafanya bara hili lishindwe kuepuka athari zinazoweza kudhibitiwa za mabadiliko ya hali ya hewa.

Litakuwa jambo la kutia moyo sana ikiwa asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kila nchi yakijitokeza kuweka viwango vipya na kanuni za maadili ya kudumisha mazingira safi ya kuishi katika maeneo yao.

Hadi sasa yamekuwepo matamko mengi sana ya kimataifa kuhusu masuala ya mazingira ambayo hayajaisogeza dunia popote karibu na mazingira bora. Taswira ya mazingira haijawahi kuonekana bora dhidi ya mioto ya misituni, barafu inayoyeyuka na sehemu za fukwe zilizochafuliwa.

Mara kwa mara tunashtushwa na ripoti kuhusu kuongezeka kwa magonjwa yanayoibuka, uchafuzi wa mazingira wenye sumu unaoenea, dharura ya hali ya hewa, na upotevu mkubwa wa baioanuwai jambo ambalo linachanganya mustakabali wa sayari yetu.

Hakuna eneo la Kijiografia ambalo limechukua jukumu kamili au kutoa mwongozo wa kurekebisha kile ambacho kilienda vibaya tangu COP ya kwanza. Kuna mambo mengi ya kuzungumza kwenye COP26. Tukio hili linapaswa kuwa fursa kwa nchi zenye kipato cha juu na nchi maskini kujitolea bila kuyumbayumba kuchukua hatua kuhusu ongezeko la joto duniani.

Kenia | Nairobi | Smog | Luftverschmutzung
Msongamano wa magari mjini NairobiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim

Kwa upana, hatua lazima zichukuliwe bila kucheleweshwa zaidi kwa sababu jambo hili laweza kusababisha mataifa kuingia migogoro na kukosekana kwa utulivu huku serikali zikishindwa kushikamana na mipango iliyokwishakubaliwa ya kupunguza joto duniani.

Tafiti za karibuni zinaonesha mabadiliko ya hali ya hewa yanawasukuma wakazi wa vijijini barani Afrika kuhamia mijini. Mwenendo usio imara wa hali ya hewa na majanga ya kimazingira yanaathiri tija vijijini, na kuwalazimu wakulima na wale wanaotegemea kilimo au minyororo yake ya thamani kuhamia mijini kutafuta njia mbadala za kujikimu.

Wakati mabadiliko ya hali ya hewa yanapozidi kuwa mabaya, miji ya Afrika ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea uzalishaji wa vijijini hivi karibuni haitakuwa tena mahali panapofaa kuhamia kwa sababu ajira lazima zibadilike kulingana na matakwa ya hali ya hewa.

Hivyo, sera na watoa maamuzi wa bara hili lazima waongoze watu wao kuchukua hatua kulingana na maamuzi yao wenyewe yasiyotegemea mikutano ya ulimwengu kwa siku zijazo.

Mataifa ya Afrika ni sehemu ya jumuiya kubwa zaidi ya kimataifa na katika masuala yanayohusu ongezeko la joto duniani lazima yazingatie sasa matumizi bora ya idadi ya watu na maliasili ili kudhibiti utoaji wa hewa ukaa.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, sayansi na mbinu za uzalishaji wa chakula, watu wengi wamenufaika sana kwa kuishi maisha yenye afya katika miongo ya hivi karibuni kuliko watangulizi wetu. Tunatarajia siku zijazo kuwa bora zaidi ingawa uhaba wa chakula bora bado unatishia maisha ya mamilioni ya watu.

Lakini lazima tukumbuke kwamba yote tunayofurahia yanategemea hali asili ya mazingira ya jamii zetu. Kwa hivyo, mkazo lazima uwe katika kufundisha kizazi kipya zaidi juu ya maumbile ya nchi. Watu wote lazima wawe na nidhamu na tuoneshe hivyo katika shughuli zetu kwamba tunathamini mazingira yetu ya asili.