1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yatolewa mwito kuwa watulivu

11 Januari 2019

Mataifa yazungumzia kwa uangalifu mkubwa matokeo ya uchaguzi wa uraisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaliyotangazwa mapema jana. Wengi wajiepusha kumpongeza mshindi Felix Tshisekedi.

https://p.dw.com/p/3BMLZ
DR Kongo Lage nach Wahlsieg von Tshisekedi
Picha: Reuters/B. Ratner

Viongozi wa jumuiya za kimataifa wameendelea kuzungumzia lakini kwa uangalifu mkubwa matokeo ya uchaguzi wa uraisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaliyotangazwa mapema jana, huku wengi wakichagua kutompongeza kiongozi wa upinzani aliyetangazwa mshindi Felix Tshisekedi na kutoa mwito wa mivutano yote kumalizwa kwa amani. 

Matokeo ya awali yalipeleka ushindi kwa kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi. Lakini mgombea mwenzake ambaye paia anatokea upinzani Martin Fayulu mara baada ya kutangazwa matokeo hayo alilalamikia mchezo mchafu na kuyaita matokeo hayo mapinduzi ya uchaguzi.

Marekani imetoa tamko hii leo kwa kutaka ufafanuzi zaidi wa matokeo hayo, huku ikiwapongeza wapiga kura wa taifa hilo kwa ujasiri waliouonyesha.

Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Robert Palladino amesema kupitia taarifa ya wizara hiyo kwamba baada ya tume ya uchaguzi ya CENI kutangaza matokeo hayo ya awali, Marekani itahitaji ufafanuzi zaidi juu ya maswali yaliyoibuliwa kuhusiana na kuhesabiwa  kura. Lakini pia amewataka wadau wote kuwa watulivu wakati mchakato huo ukiendelea.

UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Antonio Guterres, UN-Generalsekretär
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres awataka Wacongo kujizuia na aina yoyote ya machafuko. Picha: Getty Images/AFP/J. Skarzynski

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Stephane Dujarric alisema katibu mkuu huyo amezitaka pande zote kujiepusha na machafuko na kusaka suluhu ya mivutano ya uchaguzi kwa amani.

Tshisekedi alishinda kwa asilimia 38.57, akimshinda mgombea mwenzake Fayulu.

Katibu mkuu ameelezea matumaini yake kwamba tume huru ya uchaguzi,serikali, mahakama ya katiba, vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa pamoja watasalia kwenye misingi ya majukumu yao ili kuendeleza utulivu na demokrasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Faki Mahamat nae akitolea mwito kama huo.

Umoja wa Ulaya wenyewe umesema unasubiri uamuzi utakaotolewa na waangalizi wa uchaguzi. Msemaji wake Maja Kocijancic amesema Umoja wa Ulaya kwa wakati huu unawaomba wanasiasa nchini humo kujiepusha na aina yoyote ya machafuko na kuruhusu mchakato wa kudemokrasia kuendelea. Ufaransa hata hivyo, iliyapinga wazi matokeo hayo.

Tume huru ya uchaguzi nchini humo, CENi ilimtangaza Tshisekedi kushinda kwa asilimia 38.57 ya kura, akimpiku Martin Fayulu aliyepata asilimia 34.8. Ramazani Shadary, mteule wa rais Jodeph Kabila, aliambulia asilimia 23.8 tu ya kura. 

Matokeo ya uchaguzi wa wabunge ambao pia ulifanyika sambamba na huu wa uraisi yanatarajiwa kutangazwa hii leo jioni na wabunge wengi wa chama cha Kabila wamejitangaza kushinda viti vya ubunge.

Chaguzi mbili zilizopita za mwaka 2006 na 2001, ambazo rais Kabila alishinda ziligubikwa na umwagikaji mkubwa wa damu na wengi wanahofia kurudia kwa machafuko hayo iwapo matokeo ya uchaguzi yatakosa uhalali. Tayari polisi wawili na raia wawili wameuawa jana, na wengine 10 kujeruhiwa baada ya kuzuka maandamano katika mji wa magharibi mwa Congo, Kikwit ambako ni ngome ya Fayulu.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu