1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo kunadi haki za uchimbaji mafuta kwenye misitu ya mvua

20 Julai 2022

Shirika la mazingira la Greenpeace limezihimiza kampuni kubwa za mafuta kususia mnada mkubwa wa haki za uchimbaji mafuta na gesi nchini DRC, ikiwemo katika eneo la misitu ya nvua, ambao imeutaja kama bomu la kaboni.

https://p.dw.com/p/4EQ1r
Demokratischen Republik Kongo | Congo River
Picha: Frans Lanting/picture alliance

Waziri wa nishati wa Congo Didier Budimbu alitangaza siku ya Jumatatu kuwa maeneo 27 ya utafiti wa mafuta na matatu kwa ajili ya gesi yatapigwa mnada kuanzia Julai 28. Kati ya vitalu 27 vya mafuta, vitatu viko kwenye mwambao wa bonde la  Mto Congo na tisa katika bonde kubwa la eneo la msitu wa mvua mashariki mwa nchi hiyo.

Vitalu vingine 15 viko mashariki mwa nchi hiyo, karibu na maziwa Albert na Tanganyika. Vitalu vitatu vya gesi vipo kwenye ziwa Kivu, lililoko pia mashariki mwa Congo.

Soma pia: Greenpeace yahimiza moto wa Bonde la Kongo ushughulikiwe

Mkuu wa kampeni ya misitu ya Afrika kutoka shirika la Greenpeace, Irene Wabiwa, alisema mnada huo unawaweka watu wa Congo katika hatari ya rushwa, vurugu na umaskini ambavyo bila shaka vinaambatana na kile alichokiita laana ya mafuta.

Greenpeace ilionya hasa juu ya mipango ya kuchimba visima katika bonde la kati, kwenye vitalu ambavyo inasema vimo ndani ya mifumo ya ikolojia na maeneo kadhaa yaliyohifadhiwa.

Deutschland Schwedt | Greenpeace protestiert bei der Rosneft-Tochter PCK
Wanaharakati wa shirika la Greenpeace wakiwa kwenye harakati zao za kupinga uchumbaji wa mafuta.Picha: Patrick Pleul/dpa/picture alliance

Wanaharakati wa mazingira wameandamana kupinga mipango ya kuchimba visima katika bonde la kati, wakisema matarajio ya mafuta katika eneo hilo, ambayo yanajumuisha kukatwa kwa maeneo makubwa ili kuweka njia za usaifirshaji wa vifaa, yanaweza kuwa na athari mbaya kwa spishi adimu na kutoa gesi chafu ambayo imekaa bila kusumbuliwa kwa maelfu ya miaka.

'Bomu la kaboni'

Greenpeace Afrika ilisema mwezi uliyopita kwamba vitalu vitatu vinapishana na mfumo wa majani mororo wa Cuvette Centrale, ambao ni eneo la bayoanuwai  lenye takribani gigatani 30 za kaboni, sawa na miaka mitatu ya utoaji wa gesi chafu duniani, na kuonya kuwa uchimbaji wa mafuta unaweza kusababisha kutolewa kwa akiba kubwa ya kaboni inayohidahdiwa na mfumo huo.

Soma pia:Wanaharakati wa mazingira waitwisha DR Congo mzigo wa lawama 

Shirika hilo la utetezi wa mazingira linasema udongo wa maeneo hayo ni bomu la kaboni ambalo likivurugwa linaweza kutoa kiasi kikubwa cha gesi inayozuwia joto, na hivyo kuchochea ongezeko la joto duniani na kuongeza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

Serikali ya Congo inasema ilitoa idhini ya kunadiwa vitalu hivyo baada ya kukamilika kwa utafiti wa athari za kimazingira. 

Uganda Ölförderung Umwelt Indigene Total
Vitalu vingine vya mafuta viko karibu na ziwa Albert, linalokatiza kati ya DRC na Uganda.Picha: Jack Losh

Mnada huo unakuja baada ya serikali kufikia makubaliano mnamo mwezi Februari, na tajiri wa Israel Dan Gertler, kumlipa dola bilioni mbili kuachia haki zake kwenye vitalu viwili vilivyoko ziwa Albert.

Mnamo Aprili, serikali ilitangaza kwamba itaendelea na mnada huo.

Soma pia: Watu masikini waathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

Wanasayansi wametoa maonyo kadhaa kuhusu maeneo ya majani mororo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambayo yanajumuisha eneo lenye ukubwa sawa na England.

Katika eneo lote la bonde hilo, karibu tani bilioni 30 za kaboni huhifadhiwa, watafiti walikadiria katika utafiti wa jarida la Nature mwaka wa 2016. Kiwango hicho ni takribani sawa na miaka mitatu ya utoaji wa hewa chafu duniani.

Chanzo: AFP