1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo-Brazzaville:Sassou Nguesso atarajiwa kushinda uchaguzi

Zainab Aziz Mhariri:Sylvia Mwehozi
21 Machi 2021

Raia wa Jamhuri ya Congo Brazzaville wamepiga kura leo Jumapili kumchagua Rais ambapo, rais aliyepo madarakani Denis Sassou Nguesso anatarajiwa kushinda uchaguzi huo na hivyo kuongeza muda wa utawala wake wa miaka 36

https://p.dw.com/p/3qw48
Republik Kongo Wahlen Brazzaville
Picha: Hereward Holland/REUTERS

Matokeo yanatarajiwa kutolewa siku nne zijazoa na ikiwa hakuna mmoja kati ya wagombea saba atakayepata zaidi yaasilimia 50% ya kura, basi duru ya pili itafanyika ndani ya siku 15 baadaye.Sassou, mwenye umri wa miaka 77, aliingia madarakani mnamo mwaka 1979. Alipoteza kiti chake kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Congo -Brazzaville mwaka 1992 na hatimaye kunyakua tena kiti cha urais mnamo 1997 baada ya nchi hiyo kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Na kisha kuibadili katiba ambayo iliruhusu kuongeza mihula ya kutawala.

Mpinzani mkuu wa rais huyo, waziri wa zamani wa serikali Guy-Brice Parfait Kolelas, mwenye umri wa miaka 60 amelazwa hospitalini kwa ugonjwa wa COVID-19. Kwa mujibu wa mkurugenzi wake wa kampeni alipozungumza na redio ya France international ameeleza kuwa Kolelas anatarajiwa kupelekwa nchini Ufaransa.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha (MCDDI) Guy Brice Parfait Kolelas
Kiongozi wa chama cha upinzani cha (MCDDI) Guy Brice Parfait KolelasPicha: Marco Longari/AFP

Kolelas, ambaye alimaliza wa pili kweenye uchaguzi wa mwaka 2016, alizungumza kwa njia ya video kutoka kwenye kitanda chake hospitalini aliwasihi Wakongo wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura ili kuleta mabadiliko. Akizungumza baada ya kupiga kura yake, Sassou Nguesso alisema kuwa hali ya amani ilitawala wakati wa kampeni za uchaguzi lakini alipoulizwa juu ya usalama wakati wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi, na kukumbushia wimbi la vurugu lililotokea baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2016, alijibu: "Mimi sio Mungu".

 Sassou Nguesso pia alithibitisha kuwa ndege ya matibabu ilikuwa imewasili katika mji mkuu wa Brazzaville ambayo itambeba mpinzani wake Kolelas Paris na kumpeleka kutibiwa huku akimtaka "apone haraka".

Jamhuri ya Congo-Brazzaville imekuwa na idadi ya chini ya watu 10,000 waliothibitishwa kuugua COVID-19 tangu janga la corona lilipoanza na mpaka sasa jumla ya 134 wamekufa nchini humo kutokana na ugonjwa huo.

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya hawakualikwa kufuatilia uchaguzi huo, nawakati huohuo wizara ya mambo ya ndani imekataa kuwaruhusu waangalizi wa Kanisa Katoliki wapatao 1,100 kushiriki kwenye zoezi  hilola uchaguzi.

Hata hivyo waangalizi hao wana matumaini kwamba uchgauzi utakuwa wa amani tofauti na uchaguzi uliopita wa mwaka 2016 ambao uliathiriwa na vurugu za hapa na pale.

Rais wa Congo-Brazzaville Denis Sassou Nguesso
Rais wa Congo-Brazzaville Denis Sassou NguessoPicha: picture-alliance/Zumapress/W. Songyu

Serikali ilisaini makubaliano ya amani na kundi la waasi waliokuwa wanampinga Sassou Nguesso mnamo mwaka 2017, hatua iliyounyamazisha mzozo kusini mwa nchi hiyo.

Mstaafu Michel Bedo, mwenye umri wa miaka 80, baada ya kupiga kura yake kwenye shule moja katika mji mkuu wa Brazzaville alisema atnaumai zoezi la kura litakwenda shwari bila vurugu kutokea Wakongo hawataki machafuko.

Kulingana na Benki ya Dunia Congo-Brazzaville ni mzalishaji mkuu wa mafuta, lakini asilimia 41% kati ya wananchi wake milioni 5 na laki 4  wanaishi katika umaskini mkubwa.Nchi hiyo ya Afrika ya Kati inayozalisha mafuta imetumbukia kwenye mgogoro wa kiuchumi. Wanaharakati wa kupambana na ufisadi wanasema pesa nyingi zimepotezwa na wapambe wa wa Rais Sassou, shutuma ambazo serikali inazikanusha.

Vyanzo:AFP/RTRE/AP