1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanzo cha mzozo wa Mali na mshirika wake Ufaransa

Daniel Gakuba
6 Mei 2022

Mzozo kati ya Mali na mkoloni wake wa zamani Ufaransa, unazidi kuongezeka, ambapo katika hatua ya karibuni zaidi, Mali imejiondoa kwenye mikaba yote ya ulinzi na Ufaransa.

https://p.dw.com/p/4Awh5
Afrika Militär Missionen von Barkhane in Mali
Picha: Etat-major des armées / France

Kwa miaka tisa iliyopita, Ufaransa ilikuwa mshirika muhimu zaidi wa Mali katika vita dhidi ya makundi ya kijihadi, yaliyouwa maelfu ya watu na kuwafanya wengine mamia kwa maelfu kubaki bila makaazi.

Leo hii vikosi vya Ufaransa vinafungasha na kuondoka Mali baada ya uhusiano kuvurugika kati ya Paris na makamanda wa kijeshi wanaoiongoza Mali hivi sasa, ambao wiki hii walijiondoa katika makubaliano yote yaliyofikiwa kati ya Ufaransa na serikali za zamani za Mali.

Kipi kilikwenda kombo?

Ufaransa ilianzisha operesheni zake katika Ukanda wa Sahel mwaka 2013, ikiazimia kuisaidia Mali ambayo ni koloni lake la zamani kukandamiza uasi uliokuwa umechipuka upande wa kaskazini. Lakini makundi ya kijihadi yaliyofanya uasi huo yalijipanga upya na kuanzisha vita vikali katikati mwa nchi, ambavyo rais wa kuchaguliwa, Ibrahim Bubacar Keita hakuweza kuvishinda.

Soma zaidi: Kiongozi wa Togo akubali jukumu la upatanishi Mali

Agosti 2020, serikali ya Keita iliangushwa na maafisa wa jeshi waliochukizwa na utawala wake, lakini nao walifurushwa katika mapinduzi mengine ya kijeshi Mei 2021.

Mali | Colonel Assimi Goita
Kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita.Picha: Malik Konate/AFP

Tangu wakati huo, uhusiano kati ya Mali na Ufaransa umekuwa ukisambaratika, hasa kutokana na wanajeshi waliochukuwa madaraka mjini Bamako kukaidi miito ya kuweka tarehe ya uchaguzi kuelekea utawala wa kiraia. Wanajeshi hao wanaituhumu Ufaransa kuchochea nchi za Afrika Magharibi kuishupalia Mali.

Mvutano ulichukua sura mpya baada ya watawala wa Mali kujenga uhusiano wa karibu na Urusi, na kisha kuwaalika wakufunzi wa kijeshi ambao Ufaransa na washirika wake wa magharibi wanasema ni mamluki kutoka kundi binafsi la kiulinzi la Wagner.

Soma pia: UN: Zaidi ya wakimbizi 36,000 waingia Niger mwaka huu

Mwezi Januari mwaka huu Balozi wa Ufaransa nchini Mali alitimuliwa, na mwezi uliofuata Ufaransa ilitangaza kuwa ilikuwa ikiwaondoa wanajeshi wake nchini Mali, pamoja na wa nchi nyingine walioshiriki katika operesheni Takuba inayoongozwa na Ufaransa.

Mali yavunja mikataba yote ya usalama na Ufaransa

Na kuporomoka kwa uhusiano baina ya Paris na Bamako hakukuishi hao, kwani Jumatatu wiki hii watawala wa kijeshi nchini Mali waliivunja mikataba yote ya kiusalama iliyosainiwa kati ya Ufaransa na serikali zilizotangulia.

Mali Bamako Anti Frankreich Pro Russland Protest
Muandamanaji akiwa na bango linalosomeka, "Ufaransa, mkulima wa bustani ya ugaidi" wakati wa maandamano ya kudai kuondoka kabisaa kwa Ufaransa nchini Mali, Februari 19, 2022.Picha: Florent Verges/AFP

Makubaliano hayo ni pamoja na ya mwaka 2013 yaliyowapa uhuru wanajeshi wa Ufaransa kutembea watakako nchi Mali, na kubainisha upande ulio na kauli ya mwisho pale yanapotokea matatizo.

Upo pia mkataba wa ushirikiano wa kiulinzi wa mwaka 2014, na itifaki ya mwaka 2013 kuhusu kuundwa kwa kikosi maalumu cha nchi za Ulaya kijulikanacho kama Takuba, ambacho Ufaransa ilitumai kingeipunguzia mzigo wa majukumu ya usalama nchini Mali.

Soma pia:Mali yaishtumu Ufaransa kwa ukiukaji wa anga lake kupeleleza wanajeshi 

Viongozi wa kijeshi wa Mali wamesema Ufaransa imekuwa ikiyaziba masikio pale ilipotakiwa kutoa ushirikiano katika kuyafanyia marekebisho makubaliano hayo, na matokeo yake ilikuwa ikikiuka wazi wazi mamlaka na uhuru wa kitaifa wa Mali.

Mfano uliotolewa ni kwamba ndege za Ufaransa zimeingia bila ruhusa katika anga ya Mali, mara zipatazo 50 katika muda wa wiki chache zilizopia, ikikiuka amri ya kutoingia katika eneo maalumu lililokatazwa na mamlaka mjini Bamako.

Shutuma za upelelezi

Tukio jingine lililosababisha msuguano ni pale jeshi la Ufaransa lilipoonyesha mkanda wa vidio liliodai unaonyesha mamluki wa kirusi wakiizika miili karibu na kambi ya Gossi, siku moja baada ya wanajeshi wa Ufaransa kuondoka kwenye kambi hiyo.

Jeshi hilo lilisema ilikuwa ni njama ya kuja baadaye kulisingizia kuwa lilifanya uhalifu wa kivita.

Kilio cha msanii wa Mali

Watawala wa Mali walikasirishwa na kitendo hicho, wakalituhumu jeshi la Ufaransa kufanya ujasusi na kuwa na nia ya kuihujumu Mali.

Soma pia: Mali yaituhumu Ufaransa kuchafua sifa ya jeshi lake

Mkuu wa mtandao wa sekta ya usalama barani Afrika Niagale Bagayoko, ni mmoja tu wa wataalamu wengi ambao wanahofu kuwa hali ya uhasama ikiendela hivi, ipo hatari ya kuzuka makabiliano baina ya wanajeshi wa Mali na wa Ufaransa.

Mvutano huu pia unaweka mashakani ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, unaowashirikisha wanajeshi na maafisa wa polisi wapatao 14,000 kutoka nchi mbali mbali.

Chanzo: afpe