Champions League -duru ya kwanza leo
19 Septemba 2007Duru ya kwanza ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya msimu huu, inarudi uwanjani tena leo baada ya jana klabu 2 za Ujerumani: Bremen na Schalke, kushindwa kutamba.
Bayern Munich –mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani, msimu huu, ni miongoni mwa mabingwa 4 wa zamani wa champions League,watakaoingia kesho uwanjani kwa duru ya kwanza ya kombe la UEFA.
Mabingwa wa dunia-Itali, wamerudi kileleni miongoni mwa timu bora za dimba duniani mwezi uliopita.
Mabingwa wa dunia Itali wameparamia tena kileleni mwa ngazi ya FIFA ya timu bora kabisa duniani iliotoka leo.Itali imeipiga kumbo Brazil hadi nafasi ya tatu.
Mabingwa wa dunia wamerudi kileleni kufuatia ushindi wao wa mabao 2:1 dhidi ya Ukraine na ikatoka sare 0:0 na makamo-ningwa Ufaransa mapema mwezi huu.Argentina imechukua nafasi ya pili wakati ujerumani imepanda hadi nafasi ya 4.
Baada ya kuparamia nafasi ya kwanza,Itali imetangaza ina miadi na wenyeji wa kombe lijalo la dunia 2010-Afrika kusini hapo oktoba 17.Changamoto hiyo itakua huko Toscana.Siku 4 kabla mpambano huo, mabingwa wa dunia watacheza na Georgia mjini Genoa kuania tiketi ya finali za kombe la Ulaya 2008 huko Uswisi.
Katika champions-league-kombe la klabu bingwa barani ulaya ,leo ni zamu FC Barcelona ya Spain ikicheza na Olympique Lyon ya Ufaransa.Mabingwa wa Ujerumani VFB Stuttgart watakuwa wageni wa Glasgow rangers huko Scotland.
Stuttgart watakuwa na kazi ngumu kuepuka wembe uliozinyoa jana timu 2 za Ujerumani Schalke na Bremen usiwanyoe na wao ugenini.
Valencia ya Spain iliizaba Schalke bao 1:0 tena nyumbani mwao Gelsenkirchen.
Bremen ilikiona cha mtema kuni kutoka kwa Real Madrid ilipotandikwa mabao 2:1.ilikua raul na van Niestelrooy waliolifumania lango la Bremen.
Wakati Real Madrid na mabingwa AC Milan walianza vyema msimu wao Chelsea na Liverpool zilibidi kuridhika na sare .
Bayern Munich ambayo msimu huu haikukata tiketi ya champions League, imeangukia kombe la UEFA-kombe la shirikisho la dimba la Ulaya.Kesho,Munich inaikaribisha nyumbani Beleneses ya Ureno.
Stadi wa kamerun anaeichezea Hamburg Thimothee Atouba, amefungiwa kucheza mechi 4 na shirikisho la dimbala Ujerumani kwa kumpiga kisugudi mchezaji wa Frankfurt, Albert Streit.Kitendo hicho hakijaonekana na rifu uwanjani bali kamera baadae zilifichua kisa hicho.
Korea ya kaskazini imeapa kucheza kufa kupona jumamosi hii pale itakapoumana katika robo-finali na wasichana wa ujerumani katika kombe la dunia la wanawake huko China.Wasichana wa Ujerumani wameibuka juu ya kundi lao A na kila kitu kinawaendea vyema kuteta taji lao la ubingwa.Wasichana wa Ujerumani wanadai, hawatawaachia wakorea ya kaskazini kuwatilia kitumbua chao mchanga hapo jumamosi .