1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CENI yasema vifaa vyote vya uchaguzi vimewasili Kongo

Jean Noël Ba-Mweze
11 Desemba 2023

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tume Huru ya Uchaguzi, CENI, imesema vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoagizwa kutoka China tayari sasa viko Kongo na hivyo kuthibitisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu Disemba 20. Sikiliza na kusoma ripoti ya mwandishi wetu wa mjini Kinshasa, Jean-Noel Ba Mweze.

https://p.dw.com/p/4a0ld

Tume ya uchaguzi ilipokea zaidi ya kilo 92,000 za vifaa vya uchagumwishoni mwa wiki ambavyo ni mzigo wa mwisho unaojumuisha hati nyeti pamoja na karatasi za matokeo na zile za maelezo kuhusu uchaguzi.

"Tarehe 20 kutakuwa na uchaguzi kwa sababu vifaa vyote kwa ujumla vipo tayari na kweli vimesambazwa. Vifaa hivyo kwa mfano ni karatasi za matokeo, karatasi za maelezo, wino usiofutika, vyeti vya kura, yaani karatasi zote zipo na vifaa tayari viko hapa." amesema Jean-Claude Munganga, mmoja wa wasemaji tume huru ya uchaguzi.

Wakati uchaguzi huo ukithibitishwa, baadhi ya wagombea urais hawana tena jinsi ya kuendelea na ziara mikoani. Wamekwama kutokana na ukosefu wa mafuta ya ndege.

Uchaguzi wa Kongo
Wakongomani watachagua Rais, Wabunge na Madiwani katika uchaguzi wa Disemba 20Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Wanaulaumu utawala wa Rais Félix Tshisekedi kwa kuzuia mafuta katika kila uwanja ili kuwakwamisha wapinzani.

Miongoni mwa waliokumbwa na kadhia hiyo ni mgombea Martin Fayulu aliyekwama mkoani Equateur wakati akisubiriwa huko  Lubumbashi.

"Tuko wakati wa kampeni za uchaguzi katika nchi kubwa sawa ambapo ndege ndiyo njia pekee ya kupitia ili kufika katika mikoa. Lakini serikali ya nchi inayojiita jamhuri ya kidemokrasia inazuia ndege za kibinafsi kununua mafuta. Kwa hiyo nalaani vitendo hivyo visivyo vya kidemokrasia." amesema Devos Kitoko, Katibu Mkuu wa ECIDE, chama cha siasa cha Fayulu.

Mgombea Dénis Mukwege pia ametoa malalamiko hayo hayo akiilaumu serikali kwa kuzuia upatikanaji wa mafuta.

Malalamiko hayo yanatolewa chini ya siku kumi kabla ya uchaguzi mkuu ambapo Wakongo  watamchagua Rais wa Jamhuri, wabunge wa kitaifa na wale wa mikoa, pamoja na washauri wa manispaa.