1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CAR: Uchaguzi kufanyika licha ya wasiwasi wa usalama

Daniel Gakuba
25 Desemba 2020

Wagombeaji kadhaa kwenye uchaguzi wa Jumapili katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wamesema wanajiengua kutokana na sababu za kiusalama. Hata hivyo, serikali inasisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.

https://p.dw.com/p/3nDMe
Zentralafrikanische Republik Bangui | Ausschreitungen | UN-Kräfte
Hakuna shughuli nyingi katika mitaa ya mji mkuu, BanguiPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

 

Wagombea wawili wa urais, Eloi Anguimaté na Aristide Briand Reboas, wamezungumza na vyombo vya habari, na kuelezea wasiwasi wao juu ya maandalizi ya uchaguzi huo wa Disemba 27. Hali kadhalika wagombea wote wa ubunge kutoka Lobaye kusini mwa nchi walijiunga na miito ya kutaka uchaguzi huo uahirishwe.

Rais wa sasa Faustin Archange Touadera anatarajia kushinda na kuchukuwa muhula wa pili madarakani, akiwapiku wapinzani 15 waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho cha urais.

Hali ya wasiwasi yatanda mjini Bangui

Kulingana na maoni ya wakaazi wa mji mkuu, Bangui, hali ya usalama haitoshelezi kuhakikisha uchaguzi salama siku ya Jumapili. Huko Bambari, eneo la katikati mwa nchi ambalo ni kitovu cha mapigano, wapo wanajeshi wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa,  MINUSCA, lakini pia na wanamgambo waasi ambao wamejihami.

Soma zaidi: Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelekea uchaguzi mkuu

Askofu mkuu Richard Appora anasema hana uhakika na hali ya mambo. "Mji umetulia, naona watu wakizunguka katika maeneo, lakini maafisa wa MINUSCA na wa jeshi la serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, hawaonekani popote. Ni kweli kwamba milio ya risasi inayosikika inatufanya tuhofie kuwa kilichotokea mwaka 2013 kinaweza kujirudia wakati huu.''

Zentralafrikanische Republik Wahlkampf 2020
Rais Faustin Archange Touadera anapigiwa upatu kushinda muhula wa pili mamlakaniPicha: Camille Laffont/APF/Getty Images

Katika mkoa mwingine wa katikati mwa nchi wa Dekoa, kulikuwepo ripoti za kutokea uhasama, na viongozi wa tawala za mkoa pamoja na wananchi wa kawaida walikimbilia kwenye kambi ya MINUSCA kutafuta usalama. Na huko Boali, umbali wa kilomita takribani 60 kaskazini mwa mji mkuu, Bangui kulikuwa na taarifa za mapigano asubuhi ya siku kuu ya Krismasi, kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo waasi wa kundi linalojiita Muungano wa Kizalendo kwa ajili ya Mabadiliko, CPC.

Soma zaidi: Rwanda na Urusi zatuma wanajeshi Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kupelekwa kwa majeruhi katika mji wa Bangui kumeeneza hofu katika mji huo, na kulemaza shughuli za serikali na za watu binafsi. Ofisi za Umoja wa Mataifa tu ndizo zilikuwa zikifanya kazi.

Msaada wa jeshi la anga la Urusi

Wakati hali hiyo ikijiri, waziri wa Ulinzi na ukarabati wa nchi, Marie-Noëlle Koyara amejaribu kutuliza wasiwasi wa umma.

"Tunasikitika kulazimika kuja kuilaani hali hii. Kura ni haki ya kikatiba. Serikali inajipanga, tutatumia vikosi vyetu vyote ili usalama na utulivu urudi nchini mwetu."

Russland Zenzralafrikanische Republik | Faustin Archange Touadera und Putin
Rais Faustin Archange Touadera (kushoto) na mwenzake wa Urusi Vladimir PutinPicha: Sergei Chirikov/AP Photo/picture alliance

Lakini ukweli ni kwamba vikosi vya jeshi la serikali vimevunjika moyo, licha ya hakikisho kutoka kwa Rais Faustin Archange Touadera, kwamba wanakaribia kupata msaada wa anga kutoka Urusi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto inayowakabili.

Kauli hiyo ya rais Touadera ni ishara kwamba serikali yake haitaki kubadilisha msimamo wake, kwamba lazima uchaguzi ufanyike tarehe 27 Desemba kama ilivyopangwa,licha ya wasiwasi huo uliopo.

Muungano wa waasi watangaza kusitisha mapigano kwa saa 72

Huku hayo yakiarifiwa, ushirika wa waasi wa CPC umesema utasitisha mapigano kwa siku tatu, kuelekea uchaguzi huo wa Jumapili.

Zentralafrikanische Republik Bangui | Wahlkampf Präsident
Kampeni za uchaguzi zinafanyika chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya Umoja wa MataifaPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Taarifa ambayo imetolewa na muungano huo ulioanza mashambulizi dhidi ya serikali Ijumaa iliyopita, imesema wapiganaji wake wote watasitisha vita kwa saa 72 kote nchini humo.

Makundi mawili kwenye muungano huo wa CPC, yameilithibitishia shirika la habari la AFP kuwa taarifa hiyo ni kweli.

Soma zaidi: Walinda amani wapelekwa Afrika ya Kati kulinda uchaguzi

Muungano wa CPC uliundwa Disemba 19 na makundi yenye silaha yaliyomtuhumu Rais Faustin Archange Touadera kuwa na njama ya udanganyifu kwenye uchaguzi huo wa Jumapili ambamo rais na Wabunge watachaguliwa.

Wanachama wa muungano huo hutoka katika makundi ya wanamgambo ambayo kwa pamoja hudhibiti theluthi mbili ya nchi hiyo.

afpe, dpae