1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelekea uchaguzi mkuu

22 Desemba 2020

Wiki moja kabla ya uchaguzi wa urais na bunge katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hali ya wasiwasi imeongezeka. Kuna wagombea 17 waliojitokeza kuwania kiti cha rais.

https://p.dw.com/p/3n2Tl
Zentralafrikanische Republik Wahlkampf 2020
Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Hali ya usalama katika taifa hilo ni tete ikiwa ni wiki moja  tu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu Desemba 27 ambapo kuna ripoti zinazozungumzia juu ya tayari kuwepo mapambano makali. Waasi nchini humo wanataka kuuteka nyara mchakato mzima wa uchaguzi,kuwazuia waliojiandikisha kupiga kura na wamepanga kufanya visa vya mashambulizi.Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati kugombea uchaguzi ujao

Baadhi ya ripoti  zinazotolewa huenda ni uzushi uliochochewa na hofu ya kuzuka kwa vurugu na machafuko mapya katika nchi hiyo.

Zentralafrikanische Republik Wahlkampf 2020
Vijana na wafuasi wa upinzani nchini Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: Camille Laffont/APF/Getty Images

Taarifa iliyotolewa na shirika la habari la Ufaransa la AFP imeeleza kwamba kuna makundi takriban matatu ya waasi yenye silaha ambayo yanataka kuinglia kati ikiwa rais aliyeko madarakani anayetetea nafasi yake Faustin Archange Touadera atarudishwa tena madarakani kwa njia za udanganyifu.

Ikumbukwe kwamba ni miaka michache tu iliyopita nchi hii ilishuhudia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu ambapo waasi kutoka upande wa wakristo waliowengi  na Wale wa jamii ya waislamu walipopambana. Maelfu ya watu walipoteza maisha ingawa idadi kamili ya waliouwawa haifahamiki. Soma 

Inaarifiwa kwamba hadi sasa kuna wakimbizi kiasi milioni 1.3 kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati na zaidi ya nusu ya wakimbizi hao wamebakia kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao.

Na juu ya hilo kati ya kila watu watano kiasi 3 nchini humo wanauhitaji wa msaada wa dharura wa kibinadamu limearifu shirika la Umoja wa Mataifa la uratibu wa msaada wa dharura UNOCHA.

Mbali na hayo bado hadi sasa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSMA upo nchini humo ukiendelea na shughuli ya kulinda amani. Ujumbe huo unasaidia kwamfano katika harakati ya kusambaza fomu za upigaji kura nchi nzima.

Mnamo mwezi Februari mwaka 2019 serikali na makundi 14 ya waasi walisaini makubaliano ya amani ambayo yanajulikana kama makubaliano ya Khartoum.

Mchambuzi wa masuala ya migogoro Peter Knoop ambaye pia ni mshauri wa serikali kadhaa na mashirika mbali mbali anasema kwamba makubaliano hayo yalileta.

Zentralafrikanische Republik Catherine Samba-Panza
Catherine Samba-Panza mgombea urais Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: Pressebüro Samba-Panza

Anasema makubaliano ya Khartoum yalifanikiwa kupunguza machafuko na kiwango cha mapigano nchini humo na baadhi ya wapiganaji walijumuishwa katika jamii.

Ingawa pia amebaini kwamba makubaliano hayo hayakutekelezwa kikamilifu kwa kutazama vurugu hizi zinazoendelea sasa nchini humo.

Kwa mtazamo wa mtaalamu huyo mazingira bado sio mazuri kwa uchaguzi ujao wa tarehe 27 mwezi huu kuelekea mchakato wa amani ambao bado ni tete.Uchaguzi huo unaweza kuleta mgawanyiko wa makundi ya  waasi yaliyosaini makubaliano ya amani kuliko kuleta mshikamano.

Alichosema mtaalamu huyo wakati akizungumza na DW ni kwamba katika uchaguzi hapana shaka hali ya kutofautiana mitizamo  ni kawaida.Na wakati uchaguzi huo unakaribia tayari hali ya wasiwasi na machafuko imeongezeka kwa mara nyingine katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Uchaguzi ukikaribia kwa upande mwingine nchi hiyo sio tu inakabiliwa na hali ya mvutano wa ndani lakini pia inakabiliwa na ushawishi wa mataifa ya kigeni.Miongoni mwao ni koloni lake la zamani Ufaransa pamoja na Urusi ambazo zinajaribu kulinda maslahi yao katika nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW