1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga; Bayern kileleni pointi sawa na Dortmund

6 Machi 2023

Kinyanganyiro bado ni kigumu katika Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, baada ushindi kwa Bayern Munich na Borussia Dortmund.

https://p.dw.com/p/4OJlr
Bundesliga  VfB Stuttgart - FC Bayern München | Eric Maxim Choupo-Moting
Picha: Bernd Feil/MIS/IMAGO

Bayern Munich wamerejea kileleni mwa Bundesliga kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Stuttgart katika uga wa Mercedes-Benz Arena.

Matthijs de Ligt alitia kimyani bao la ufunguzi kwa Bayern huku Eric Maxim Choupo-Motingakisherehekea kuongezwa kwa kandarasi yake kwa bao la pili na la ushindi kwa Bayern. Stuttgart ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 88 ya mchezo kupitia mchezaji Juan Jose Perea.

SOMA PIA; Utafiti: Borussia Dortmund ni klabu maarufu zaidi Ujerumani

Choupo-Moting amesajili rekodi ya kibinafsi ya mabao 10 msimu huu, Je siri ya mafanikio haya ni nini?

"Siri ni kujitahidi na kufurahia mchezo. Ukichanganya mambo haya mawili, nadhani unafanikiwa kila wakati. Tuna timu kubwa yenye wachezaji wa kipekee. Kila mtu akitoa asilimia 100 uwanjani, nadhani sio tu mafanikio pekee, lakini kila mchezaji atafanikiwa kibinafsi. Nina furaha kwamba inafanya kazi vizuri sana kwangu kwa sasa."

Bayern, ambao watamenyana na Paris St Germain katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa siku ya Jumatano kufuatia ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza wapo kileleni mwa jedwali kwa pointi 49, sawa na Borussia Dortmund katika nafasi ya pili tofauti ya mabao. Dortmund, walishinda 2-1 dhidi ya RB Leipzig siku ya Ijumaa. Huku sare tasa dhidi ya FC Köln ikiituliza Union Berlin katika nafasi ya tatu kwa jumla ya poiti 44.

Baada ya Ushindi dhidi ya Stuttgart kocha wa Bayern Julian Nagelsmann alikuwa na haya ya kusema:

"Nadhani tatizo lilikuwa kipindi cha pili udhibiti wetu haukuwa kamili. Kipindi cha kwanza kilikuwa bora kidogo. Kipindi cha pili tulikuwa na mashambulizi mazuri ya kujibu lakini hatukupata bao la tatu. Nadhani kama tungefunga bao la tatu, basi nadhani mchezo umekamilika. Lakini nadhani tulikuwa na nafasi ya kufunga mabao matatu au manne, kwa urahisi. Tulikuwa na mashambulizi mengi ya kushtukiza na nafasi nzuri zaidi. Mwishoni, nadhani tulistahili, lakini kwa ungumu sana."

Katika mechi nyengine

Bundesliga | SC Freiburg vs. Bayer 04 Leverkusen | Jubel 1:1
Picha: Gerd Gruendl/Beautiful Sports/IMAGO

 Mainz ilipata ushindi wa bao moja bila jibu dhidhi ya TSG Hoffeinheim. Borrussia Moenchengladbach ikatoka sare tasa na Freiburg. Schalke 04 katika nafasi ya 17 kwenye jedwali ilipata ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya timu ya mkiani Bochum. Ausburg waliishinda Werder Bremen 2-1, Bayer Leverkusen ikipata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya bibi kizee Hertha Berlin. Frankfurt na Wolfburg ziliambulia sare ya 2-2 na kukamilisha mechi za mzunguko wa 23.

Kipigo cha Ubwa

UK Liverpool v Manchester United Mohamed Salah
Mohamed Salah akishangilia bao katika mechi dhidi ya Manchester UnitedPicha: Peter Byrne/PA Images/IMAGO

Kando na Bundesliga tuelekee England ambapo Beki wa Manchester United Luke Shaw amekiri kwamba kiwango cha klabu hiyo kimeshuka tangu walipobeba kombe Carabao. Kauli hii ni baada ya kuchapwa mabao 7 mtungi na mahasimu wao Liverpool kwenye Ligi ya Premier hapo jana katika kipigo kibaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 92.

Kocha wa Man United Eric Ten Hag azungumzia kichapo hicho."Kama timu lazima tushikamane na hilo ndilo ambalo hatukufanya na hilo lilikuwa mshangao kwangu. Sijaona hili kutoka kwa timu yangu. Sidhani kama ni hivi, sidhani kama ni Manchester United. Hii ni mbaya  sana. lakini naijua timu hii, watajipanga upya na lazima turudi vizuri. Tumeonyesha huko nyuma tunaweza."

Kipigo hicho kinahitimisha mazungumzo ya ushindani mkali. United ikishikilia nafasi ya tatu, pointi 14 nyuma ya vinara wa ligi Arsenal na Manchester City inashika nafasi ya pili kwa pointi 58.

Mbabbe aweka historia PSG

Frankreich Kylian Mbappe, PSG
Kylian MbappePicha: Michel Spingler/AP Photo/picture alliance

Wakati mshambuliaji nyota Kylian Mbappe alipoongeza mkataba wake Paris St Germain mwishoni mwa msimu alisema anataka kuweka historia na klabu hiyo na alitimiza lengo hilo kwa kufunga bao lake 201 katika mechi ya ushindi wa 4-2 ya ligi ya Ufaransa ligue 1 dhidi ya Nantes.

Ushindi huu ni ujumbe uliotumwa kabla ya mechi ya marudiano siku ya Jumatano katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich baada ya kuchapwa 1-0 nyumbani katika mchezo wa kwanza. Itakua mara ya 13 kwa Bayern kukutana na PSG katika michuano ya ligi ya mabingwa.

Katika mechi nyengine Chelsea wana nafasi mmoja wa mwisho kuokoa heshima yao pale Borussia Dortmund watakapotua Stamford Bridge katika hatua ya 16 bora hapo kesho baada ya kipigo cha bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza Signal Iduna Park.

Benfica inatarajia kuendeleza matokeo mazuri watakapocheza na Brudge hapo kesho. Tottenham Hotspurs siku ya Jumatano itashuka dimbani dhidi ya AC kujaribu kupangua matokeo ya kulazwa 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza.

 

AP/Reuters