1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken ashinikiza kusitishwa mapigano Gaza

19 Agosti 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amezitaka Israel na Hamas kutovuruga mazungumzo ambayo amesema, yanaweza kuwa ni fursa ya mwisho ya kupatikana mwafaka wa vita vya Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

https://p.dw.com/p/4jcYQ
Israel | Antony Blinken na Isaac Herzog
Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken. Kulia: Rais wa Israel Isaac Herzog.Picha: Kevin Mohatt/AFP/Getty Images

Waziri Blinken, ambaye yuko katika ziara yake ya tisa ya kikanda tangu kundi la Hamas lilipofanya mashambulio katika ardhi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita amesema amerejea mjini Tel Aviv ili kushinikiza kupatikana makubaliano ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza na kuachiwa mateka. Blinken aliyasema hayo alipokutana na Rais wa Israel Isaac Herzog.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken baadaye leo atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na maafisa wengine kabla ya kusafiri kuelekea mjini Cairo, ambako mazungumzo ya kusitisha mapigano yanatarajiwa kuanza tena wiki hii.

Israel Tel Aviv | Kuwasili kwa Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alipowasili mjini Tel AvivPicha: Kevin Mohatt/AP Photo/picture alliance

Soma Pia: Duru mpya ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Gaza  

Wapatanishi wa Marekani, Qatar na Misri, wamefanya mazungumzo kwa miezi kadhaa, lakini mpaka sasa wameshindwa kufikia makubaliano.

Ari ya kufikiwa makubaliano 

Lakini sasa ari ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza imeongezeka tangu mwishoni mwa mwezi Julai baada ya mauaji ya viongozi wa Hamas akiwemo mkuu wa kisiasa wa kundi hilo Ismail Haniyeh huku mzozo wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa ukizidi kuongezeka pia.

Israel na Hamas wamekuwa wakilaumiana kwa kuchelewa kufikia makubaliano ambayo wanadiplomasia wanasema yanaweza kuepusha kusambaa kwa vita katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, polisi wa Israel wamethibitisha mlipuko wa mjini Tel Aviv kuwa ni shambulio la kigaidi.

Israel Tel Aviv | Ufuo wa Bahari
Ufuo wa Bahari katika jiji la Tel AvivPicha: Ariel Schalit/dpa/picture alliance

Begi la kubeba mgongoni lilipuka jana Jumapili jioni wakati mtu aliyebeba begi hilo alipokuwa anatembea barabarani katika eneo la kusini mwa jiji, la Tel Aviv.

Soma Pia: Netanyahu aishutumu Marekani kwa kuzuia msaada wa silaha 

Polisi wamesema mtu aliyekuwa amebeba begi hilo lililolipuka aliuawa pia wamesema mpita njia mmoja aliyekuwa anaendesha pikipiki alijeruhiwa.

Huko nchini Lebabon wizara ya afya imesema watu wawili wameuawa kusini mwa Lebanon leo Jumatatu katika mashambulizi ya Israel huku Hezbollah ikidai kuwashambulia wanajeshi na maeneo ya kijeshi kaskazini mwa Israel.

Vyanzo: AFP/DPA