1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken aihakikishia NATO kuhusu msaada wa Marekani

Josephat Charo
23 Machi 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken (23.03.2021) ameahidi kuijenga upya na kuiimarisha jumuiya ya kujihami ya NATO baada ya miaka minne ya mvutano.

https://p.dw.com/p/3r0a9
Belgien NATO l US-Außenminister Blinken u Jens Stoltenberg in Brüssel
Picha: Yves Herman/AFP

Akizungumza katika ziara yake ya kwanza barani Ulaya katika makao makuu ya NATO mjini Brussels, Blinken alisema jumuiya hiyo iko katika hatua muhimu ikikabiliwa na vitisho kote ulimwenguni, pamoja na mabadiliko ya tabia nchi. Baada ya miaka minne ya misuguano kati ya Marekani chini ya utawala wa rais aliyeondoka madarakani Donald Trump, ambaye alisema NATO imepitwa na wakati, washirika wa NATO barani Ulaya pia wamekaribisha mabadiliko ya muelekeo na kauli kutoka kwa utawala wa sasa wa rais Joe Biden.

Blinken alisema amekwenda Brussels kuihakikishia tena NATO kwamba Marekani imejitolea kwa dhati kwa jumuiya hiyo. Amesema changamoto zinazoikabili Marekani zinazowaathiri pia moja kwa moja raia wake, hakuna hata moja inayoweza kutatuliwa na nchi moja pekee na kwa hivyo Marekani itashirikiana na Urusi itakapokuwa ikipigania masilahi yake. Aliutaja mkataba mpya wa START wa kudhibiti silaha za nyuklia kama mfano wa ushirikiano huo. Hata hivyo Blinken alisema kwa upande mwingine, Marekani itapinga kwa nguvu zote uchokozi wa Urusi na hatua nyingine zinazochukuliwa na nchi hiyo kuiyumbisha NATO.

Blinken aliwaambia waandishi habari mjini Brussels alipokutana na katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg, kwamba Marekani inataka kuujenga upya ushirikiano na washirika wa NATO na kuipiga jeki jumuiya hiyo. "Kujumuisha hatua kadhaa zinazochukuliwa, likiwemo suala la Mediterania mashariki, pia si siri kwamba Uturuki ni mshirika muhimu wa muda mrefu na ambaye naamini tuna masilahi makubwa ya kuendelea kuishirikisha katika NATO. Na naamini hilo pia liko katika masilahi ya Uturuki."

Blinken na wenzake wa mataifa wanachama wa NATO walikutana ana kwa ana mjini Brussels kuandaa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi akiwemo rais wa Marekni, Joe Biden. Mkutano huo ni wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO tangu mwaka 2019.

Belgien NATO l US-Außenminister Blinken u Jens Stoltenberg in Brüssel
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken, kushoto, na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg mjini BrusselsPicha: Yves Herman/AFP

Blinken alisema kuimarika kwa jeshi la China na juhudi za Urusi kuyayumbisha mataifa ya magharibi ni vitisho ambavyo vinaitaka NATO kushirikiana, akiihimiza Uturuki kuukumbatia muungano huo wa kijeshi wenye wanachama 30. Alisema Marekani itahakikisha NATO inajikita zaidi na kuelekeza nguvu kwa baadhi ya changamoto zinazosababishwa na China kwa mahitaji ya mfumo wa kimataifa ambao ni sehemu ya maono ya mwaka 2030.

"Kuna tofauti na kutokubaliana kuhusu hali mashariki mwa Mediterania. Na nilielezea wasiwasi wangu mjini Ankara na viongozi wa Uturuki katika masuala kadhaa, ikiwemo athari za uamuzi wa kununua ndege chapa S400. Wakati huo huo, naamini kwa dhati kwamba NATO inatakiwa kuwa jukwaa ambapo washirika pia hukaa chini pamoja katika meza ya mazungumzo kunapotokea tofauti, kuzijadili, kuzishughulikia na kutafuta njia ya kuzitatua," alisema Stoltenberg.

Suala la Afghanistan

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wowote wa kuondoka Afghanistan, Blinken alisema Marekani inadurusu mapendekezo na itasikiliza na kushauriana na washirika wake. Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO watajadili suala la Afghanistan siku mbili zijazo mjini Brussels.

Stoltenberg ametenga maeneo ambayo NATO inaweza kujiendeleza na kuwa ya kisasa, kuanzia hatua za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi hadi ufadhili endeleu wa harakati za kijeshi, na inahitaji msaada wa Marekani.

Suala la Ujerumani kuendelea kushinikiza ujenzi wa bomba la gesi chini ya bahari ya Baltic kutoka Urusi limebaki pasuakichwa na kusababisha mgawanyiko. Blinken alisema mradi huo wa Nord Stream 2 unakinzana na masilahi ya Umoja wa Ulaya na huenda ukayafuja masilahi ya Ukraine. Alisema atalizusha suala hilo katika mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas.

(dpa, reuters)