1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wasema watahudhuria mazungumzo ya amani ya Moscow

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
16 Machi 2021

Wanachama wakuu wa Taliban wamesema watahudhuria mazungumzo na serikali ya Afghanistan huko mjini Moscow nchini Urusi yatakayofanyika siku ya Alhamis wiki hii kujadili mustakabali wa Afghanistan inayokumbwa na vita.

https://p.dw.com/p/3qhPy
Katar Taliban Friedensgespräche
Picha: Ibraheem al Omari/REUTERS

Pande hizo mbili za Taliban na serikali ya Afghanistan zitakutana kwa mwaliko wa Urusi siku ya Alhamisi na mwisho wa mwezi Mei Rais wa Marekani Joe Biden ataamua ikiwa nchi yake itaendelea au itasitisha uwepo wa wanajeshi wake nchini Afghanistan. Wanajeshi wa Marekani wamekuwepo nchini humo kwa kipindi cha miaka kumi. Msemaji wa ofisi ya Taliban iliyopo nchini Qatar Mohammad Naeem amesema, Ujumbe wa ngazi ya juu wa wanachama 10 wa kundi hilo wakiongozwa na mwanzilishi mwenza wa kundi laTaliban Mullah Baradar Akhund watahudhuria mkutano huo utakaoofanyika Moscow.

Licha ya kuwa na mvutano kati yake na Urusi, Marekani imepokea vyema jukumu la Urusi katika mazungumzo hayo na pia imewasiliana na mpinzani wake mwingine China ishara kwamba diplomasia inachukua mahala pake. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema siku ya Jumatatu kwamba mjumbe maalum wa nchi hiyo anayeshughulikia masuala ya Afghanistan, Zalmay Khalilzad, pia atahudhuria mkutano huo wa mjini Moscow kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za Marekani za kuhamasisha na kuunga mkono mchakato wa amani nchini Afghanistan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amewaandikia barua viongozi wa Afghanistan akiwahimiza wafikirie swala la kuunda serikali mpya, itakayojumuisha pande zote. Blinken pia amependekeza kwamba mazungumzo yafanyike ndani ya wiki kadhaa nchini Uturuki ili kufanikisha kutiwa saini makubaliano ya amani na kundi la Taliban.

Soma Zaidi:Serikali ya Afghanistan kushiriki mazungumzo yote ya amani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake inapanga kuandaa mkutano wa amani ya Afghanistan mjini Istanbul mnamo mwezi Aprili. Jitihada za Urusi na Uturuki zitaendeshwa kwa pamoja na mazungumzo yaliyosimamiwa na Qatar kati ya serikali ya Afghanistan na Taliban yaliyofanyika mjini Doha na ambayo yamekuwa yakiendelea pamoja na kuwepo vipindi virefu vya kuyapumzisha tangu mwezi Septemba mwaka jana wa 2020.

Huku mazungumzo ya amani ya Afghanistan yakiendelea kuungwa mkono, nchini humo watu wasiopungua 21 waliuawa katika mashambulio yaliyofanywa kwenye sehemu mbalimbali katika muda wa saa 24 zilizopita. Kwenye mashambulio hayo yaliyofanywa katika mikoa minane ya nchini Afghanistan watu wengine 35 walijeruhiwa kulingana na takwimu zilizotolewa na maafisa nchini humo. Kundi la Taliban limekanusha kuhusika na mashambulio hayo.

Vyanzo:AFP/DPA