1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bishara yaimarika Jumuiya ya EAC licha ya COVID19

23 Agosti 2021

Biashara miongoni mwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, imeongezeka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita licha ya makali ya janga la COVID-19. Biashara kati ya Kenya na Tanzania imeongezeka mara sita zaidi

https://p.dw.com/p/3zO3v
Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania | mit Uhuru Kenyatta
Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Matamshi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya EAC Peter Mathuki ambaye ni wa sita tangu kuasisiwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanajiri anapokamilisha siku 100 tangu kuchaguliwa kwake katika nafasi hiyo. Huku akielezea hatua ambazo Jumuiya hiyo imepiga, alikuwa mwepesi wa kusema kuwa, kuna nafasi ya kuboresha hali ya sasa.

Biashara kati ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni asilimia 15, ikilinganishwa na asilimia 70 katika mataifa ya Jumuiya ya Ulaya. Akielezea ufanisi na changamoto katika makao ya jumuiya hiyo iliyoko Arusha kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu wa Jumuiya Hiyo Peter Muthuki amesema atajaribu kuongeza kiwango hicho katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

”Tumefanikiwa kufanya mazungumzo na marais wa mataifa washirika na mawaziri, kuelewa matarajio yao kama sekretariati, sasa mahusiano kati ya sekretariati na mataifa washirika ni bora zaidi,” alisema Peter Mathuki.

Kuhusu matumizi ya sarafu moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, katibu mkuu huyo alibaini  kuwa, sheria hiyo ilianza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu, na kwamba, mataifa washirika wameombwa kuwasilisha mapendekezo ya kuandaa kongamano. Sekretariati ya Jumuiya hiyo imeanza kukagua na kuthibitisha maombi hayo na mahali pazuri pa kuandaa kongamano hilo.

Mazungumzo kuhusu Shirikisho la Siasa la Jumuiya yanaendelea, huku yakiandaliwa katika mataifa ya Burundi na Rwanda. Muthoki amesema kuwa mipango iko mbioni ya kuandaa mazungumzo hayo katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Sudan Kusini.

Kamati ya EAC yaendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na corona

Logo Ostafrikanische Gemeinschaft EAC
Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa ikishinikiza mataifa wanachama kuwa na hati  moja inayoonesha matokeo ya vipimo vya Covid-19 kwa wale waliochanjwa katika eneo zima.

Kamati Shirikisho ya Jumuiya hiyo imekuwa ikiunga mkono juhudi za kukabiliana na janga la covid, ikiwemo kutoa mafunzo, sera za muongozo na vifaa vya kupimia wananchi kwenye mipaka. Stephen Mulote ni Naibu Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Tunaomba kuwa ataendelea na ukakamavu huo hata zaidi. Sisi wakuu pamoja na wafanyikazi wote tutaendelea kumuunga mkono, ili tufanikishe maono ya jumuiya,” alisema Stephen Mulote.

soma zaidi:Tanzania, Rwanda kushirikiana mapambano dhidi ya Covid-19

Muthuki ameunga mkono hatua ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na Jumuiya akisema kuwa ujumbe uliokuwa katika taifa hilo sasa unajumuisha ripoti yake itakayowasilishwa kwa baraza la mawaziri.

Kuingia kwa DRC katika jumuiya ya Afrika Mashariki kunatarajiwa kuongeza soko la jumuiya hiyo. DRC iliyo na watu milioni 180, itakapojiunga, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na watu milioni 300. Muthuki amesema kuwa, mapato ya biashara yataongezeka kwa asimilia 50.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi