1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Rwanda kushirikiana mapambano dhidi ya Covid-19

Janvier Popote2 Agosti 2021

Rais wa Tanzania ameitembelea Rwanda ambapo yeye na mwenyeji wake Paul Kagame wamesaini makubaliano mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili, na kuahidi ufumbuzi wa pamoja dhidi ya Covid.

https://p.dw.com/p/3yRMu
Ruanda | Samia Suluhu und Paul Kagame
Picha: Rwanda Presidency

Ni ziara ya siku mbili ambayo siku yake ya kwanza imekuwa hasa ni ya kuzungumza na kusaini mikataba ya kukuza undugu kati ya Rwanda na Tanzania ambao marais wote wawili wamesema upo na kuna kila sababu ya kuuimarisha.

Wakizungumza na waandishi wa habari majira ya saa nane baada ya kikao chao cha faragha, Rais Paul Kagame ameiahidi Tanzania kuwa Rwanda iko tayari kutoa ushirikiano kwa lolote ambalo linalenga maslahi ya pande mbili, ikiwemo kutafutia ufumbuzi matatizo yaliyotokana na gonjwa mtandavu la COVID-19.

"Njia pekee ya kukabili changamoto ambazo ukanda wetu unazishuhudia ni kuungana bega kwa bega na kuchangamkia fursa zilizopo ambazo zinaweza kuleta tija kwa nchi zetu mbili. Naamini tutaendelea kuungana kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo iko imara na yenye ustawi.'',alisema Kagame.

Ushirikano wa masuala ya kiafya

Ushirikiano wa kiuchumi,kipaumbele cha ziara ya rais Samia nchini Rwanda
Ushirikiano wa kiuchumi,kipaumbele cha ziara ya rais Samia nchini Rwanda Picha: Rwanda Presidency

Kwa kiasi kikubwa mazungumzo baina ya Rais Paul Kagame na mgeni wake Samia Suluhu Hassan yamegusia masuala ya kiuchumi na ukuzaji wa uwekezaji kwa faida ya Rwanda na Tanzania, na mambo mengine kama anavyoyaorodhesha Rais Samia.

"Tulizungumzia pia mambo ya ushirikiano kwenye mambo ya Tehama, kama mnavyojua Tanzania tuna mkongo ambao tumeusambaza katika nchi jirani na Rwanda wanatumia na leo hapa tumesaini makubaliano kwamba tunaendelea kuweka uhusiano mkubwa kwenye mambo ya Tehama.'',alisema rais Samia.

Kabla ya kuongeza : ''Na niwapongeze Rwanda kwamba mko mbele yetu nasi tuko tayari kuja kujifunza kwenu, lakini yapo mambo ambayo yameingia sasa ya Covid-19, nayo tumeyazungumza kwa mapana yake, na tumeweka mikakati ya kushirikiana kupitia kituo chetu cha Rusumo lakini pia kama tulivyosaini mambo ya madawa. Tumekubaliana kuendeleza ushirikiano uliopo ambao ni ushirikiano wa kihistoria na wa kindugu. Ahsanteni sana”

Mbiundo mbinu ya pamoja

Ni mara yake ya kwanza kuja Rwanda baada ya kuingia maradakani mnamo Machi mwaka huu kufuatia kifo cha mtangulizi wake Dkt John Pombe Magufuli.

Ziara yake imetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi kama jitihada katika kuharakisha mipango ya kimaendeleo iliyopo kati ya Rwanda na Tanzania, ikiwemo ujenzi wa reli ya kilomita 572 itakayounganisha Isaka na Kigali na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.

Rais Samia hapo kesho anatarajia kutembelea Kigali Special Economic Zone, eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya viwanda vikiwemo vile vinavyomilikiwa na Watanzania.