1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bilioni 500 kusaidia kunusuru uchumi wa Ulaya

10 Aprili 2020

Wawakilishi wa mataifa 19 ya ukanda wa sarafu ya Euro wamekubaliana kutolewa mara moja kiasi cha Euro bilioni 500 kwa ajili ya kuuimarisha uchumi wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3ajbT
EU Corona Bonds Symbolbild
Picha: picture-alliance/ROPI/Fotogramma/Mantero

Hatua hiyo imefikiwa wakati ikipambana kunusuru kuanguka kwa uchumi kutokana na janga la corona.

Waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno La Maire amesema makubaliano hayo ni mazuri mno. Mataifa makubwa kiuchumi Ulaya, ya Ujerumani na Ufaransa yamekuwa yakipambana kupata suluhu ya kushughulikia athari za kiuchumi kufuatia janga hilo, wakati mawaziri wa fedha wakijadiliana kuhusu suala hilo jana Alhamisi.

Waziri wa fedha wa Ujerumani,Olaf Scholz amesifu uamuzi huo akitaja kama siku njema kwa mshikamano wa Ulaya.

Soma zaidi: Janga la virusi vya Corona laleta mgongano Umoja wa Ulaya

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliomba baraza la usalama la Umoja huo kuonyesha mshikamano, wakati lilipokutana kujadiliana kuhusu janga la virusi vya corona. Guterres amesema mbele ya baraza hilo lililogawanyika kwamba ishara ya mshikamano ya wanachama wake 15 itasaidia pakubwa katika wakati huu wa mashaka.

Kikao hicho cha kwanza cha baraza hilo kimefanyika kwa siri kupitia video, lakini Umoja wa Mataifa ulichapisha hotuba ya katibu mkuu. Baraza hilo linakutana baada ya wiki kadhaa za kutokukubaliana, hususan kati ya Marekani na China, ambako janga hilo lilianzia mwezi Disemba mwaka jana.

Bildergalerie Prominente & Corona-Infektion | Boris Johnson, Premierminister Großbritannien
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, yuko wodini akiendelea kufuatiliwa kwa karibuPicha: Reuters/Andrew Parsons/10 Downing Street

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameondolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi jana jioni na kurejeshwa wodini ambako ataendelea kupata uangalizi wa karibu wakati anapoendelea kupata nafuu. Msemaji wa Downing Street amearifu jana jioni kupitia taarifa yake. Johnson amekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku tatu baada ya hali kubadilika na kuwa mbaya, kufuatia maambukizi ya virusi vya corona. 

Nchini Marekani, mtaalamu mwandamizi wa magonjwa ya kuambukiza Dr. Anthony Fauci amesema mahitaji ya kuwalaza hospitalini wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona yamepungua sana. Fauci amesema wakati huohuo wakati wanashuhudia kuongezeka kwa vifo.

Nchini humo karibu raia milioni 17 wamepoteza ajira tangu katikati ya mwezi machi kufuatia kuanguka kwa uchumikutokana na janga hilo. Kiasi watu milioni 6.6 wamewasilisha maombi ya malipo ya kukosa kazi wiki iliyopita, hii ikiwa ni kulingana na takwimu zilizotolewa na wizara ya kazi. Hili ni ongezeko la watu zaidi ya milioni 10, waliowasilisha wiki kadhaa huko nyuma.

Katika hatua nyingine, studio za kurekodi za Universal zilizofunga maeneo yake kurekodia nchini humo katikati ya mwezi Machi, yameongeza muda wa kufunga maeneo hayo hadi Mei 31.

USA Präsident Donald Trump Coronavirus Pressekonferenz
Rais Donald Trump wa Marekani, amesifu mazungumzo kuhusu bei ya mafuta ingawa kunashuhudiwa anguko zaidi la bei ya bidhaa hiyoPicha: Getty Images/W. McNamee

Aidha, rais Donald Trump amesema amekuwa na mazungumzo mazuri na rais Vladimir Putin wa Urusi na mfalme ya Saudi Arabia, huku akielezea matarajio yake kwamba shirika la nchi zinazozalisha na kuuza mafuta kwa wingi duniani - OPEC pamoja na mataifa mengine watatangaza makubaliano waliyoyafikia hivi karibuni.

OPEC pamoja na washirika wake wanaoongozwa na Urusi wamekubaliana kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mafuta na kusema walikuwa wakitarajia Marekani na wazalishaji wengine wataungana nao katika juhudi hizo za kuimarisha bei ya mafuta iliyoathiriwa pakubwa na janga la corona.

Hata hivyo mapema hii leo kumeripotiwa kushuka kwa bei ya mafuta, wakati wazalishaji hao wakubwa wakiendelea kusaka makubaliano ya pamoja kuhusu hatua ya kupunguza uzalishaji wa mafuta, ili kukabiliana na kushuka kwa mahitaji kutokana na janga hilo la coorna.

Afrika Kusini nayo jana imeongeza muda wa kusitisha shughuli nchini humo kwa siku 14 zaidi. Zuio la awali lilitarajiwa kudumu kwa siku 21. Afrika Kusini ina visa vingi zaidi vya virusi vya corona vilivyofikia 1,934 na wagonjwa 18 wakiwa wamefariki.

Nchini Ubelgiji, polisi wameweka vizuizi vipya vya ukaguzi katika mji mkuu Brussels ili kuzuia safari zisizo na umuhimu. Polisi wanakagua nyaraka za madereva na kuwauliza madhumuni ya safari zao.

Mashirika: DW