1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la virusi vya Corona laleta mgongano Umoja wa Ulaya

8 Aprili 2020

Nchi zinazotumia sarafu ya Euro zimeshindwa kuwa na mshikamano katika mpango wa kiuchumi wa kupambana na janga la virusi vya Corona na kusababisha wasiwasi wa hali itakavyokuwa katika vita hii

https://p.dw.com/p/3adCz
EU-Finanzministertreffen per Videoschalte
Picha: Imago Images/photothek/T. Imo

Kwanza kabisa ifahamike kwamba katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja mataifa ya Ulaya yamekuwa yakijaribu kushirikiana kwa karibu kushughulikia janga hili na viongozi wa Ulaya wamekuwa wakijitahidi kushirikiana kuondowa madhila ya kibinadamu na kiuchumi kufuatia janga hili duniani ambalo limeuvuruga kabisa mfumo wa maisha ya kila siku ya mabilioni ya watu na kuuporomosha uchumi wa mataifa mbali mbali ya dunia.

Lakini bado nchi hizi zinapambana na katika upande wa kiuchumi na kifedha mawaziri kutoka nchi 19 zinazotumia sarafu ya euro zilishindwa kufikia leo Jumatano kupata makubaliano kuhusu jinsi ya kutumia kipengele chake cha fedha na kwa umbali gani kinaweza kuimarisha mshikamano kati ya nchi masikini na zile tajiri wanachama wake.

Sasa hatua hii ya kutofikiwa makubaliano na migongano mengine imesababisha athari kadhaa ikiwemo kujiuzulu mara moja kwa rais wa baraza linalosimamia utafiti wa kisayansi barani Ulaya Profesa Mauro Ferrari ambaye amevunjwa moyo na jinsi viongozi wa Ulaya wanavyolishughulikia suala la mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Symbolbild Coronavirus - EU-Videogipfel
Picha: picture-alliance/ANP

Hatua yake hii imezidisha shinikizo kwa taasisi mbali mbali za Umoja wa Ulaya ambazo zimeshutumiwa kwa kutoshirikiana kukabiliana na janga hili la dunia. Benki kuu ya Ulaya imewaambia mawaziri hao wa nchi zinazotumia sarafu ya euro kwamba huenda zikahitaji euro trilioni 1.5 za mipango ya uokozi wa kiuchumi kutokana na janga hili la Covid-19.

Juu ya hayo huko nchini Uingereza bado kinachozungumzwa ni kuendelea kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi waziri mkuu Boris Johnson aliyeambukizwa virusi vya Corona huku hali yake ikitajwa kuendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa wa magonjwa ya mapafu nchini humo. Zaidi ya watu 55,000 wameambukuzwa na takriban 6,200 wameshafariki Uingereza.

Coronavirus Premierminister Boris Johnson
Picha: Reuters/S. Dawson

Lakini pia mgogoro huu wa virusi vya Corona umesababisha malumbano ya aina yake ambapo rais wa Marekani Donald Trump amelikosoa sana shirika la afya duniani WHO akilituhumu kujielekeza zaidi kwa China huku pia akitowa kauli mbaya akisema atasimamisha ufadhili wa Marekani katika shirika hilo.

Lakini huko China katika mji wa Wuhan vilikoanzia virusi hivi matumaini ya faraja yameripotiwa ambapo marufuku ya kutotoka nje imeondolewa baada ya miezi miwili na hali ya maisha ya kawaida inatajwa imeanza kurejea leo Jumatano, kumbuka katika mji huu zaidi ya watu 50,000 walipata maambukizi na zaidi ya  2,500 walifariki. Ama kwa kuiangalia hali halisi duniani kufikia leo Jumatano zaidi ya watu milioni 1.38 wameambukizwa na 81,451 wameshafariki. Nchi zenye visa vya maambukizi kwa ujumla duniani ni 212.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW