1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Trump watofautiana vikali kuhusu rekodi zao

28 Juni 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na mpinzani wake Donald Trump wamekabiliana katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais unaopangwa Novemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4hcEf
Mdahalo wa uchaguzi wa rais Marekani 2024
Donald Trump na Joe Biden wamekabiliana katika mdahalo wa ana kwa ana kabla ya uchaguzi wa NovembaPicha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP/Getty Images

Biden na Trump wamejibizana kuhusu rekodi zao za masuala ya kiuchumi, utoaji mimba na uhamiaji katika mdahalo huo ambao kila mgombea alitafuta kumpiku mwenzake katika kinyang'anyiro kikali cha Ikulu ya White House. Biden mwenye umri wa miaka 81, na Trump mwenye umri wa miaka 78,hawakusalimiana kwa kupeana mikono wakati waliposimama jukwaani katika studio za makao makuu ya televisheni ya CNN mjini Atlanta. Hakukuwa na watazamaji ukumbuni na vipaza sauti vilizimwa wakati kila mmoja akizungumza.

Biden ambaye aliripotiwa kuwa na mafua, alimshambulia Trump akitaka kuwakumbusha mamilioni ya watazamaji wa televisheni kuwa kama Trump atachaguliwa, atakuwa rais kwanza aliyehukumiwa kwa uhalifu kuingia White House. Trump alimshambulia Biden akitilia shaka afya yake na uwezo wake wa kutamka maneno kwa sababu kuna wakati hakuwa akisikika vizuri au kukamilisha sentensi. Trump amesema azakubali matokeo ya uchaguzi kama anafikiri yatakuwa ya haki.