1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden apata kura zaidi Georgia na kumpiku Trump

6 Novemba 2020

Mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden ameendelea kupata kura zaidi katika majimbo yenye ushindani mkali hasa Georgia na Pennsylvania. Hayo yakijiri, Rais Donald Trump amedai wizi wa kura unafanywa dhidi yake.

https://p.dw.com/p/3kwWQ
US Wahl 2020 | Joe Biden Rede
Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Kulingana na kura maalum zinazobaini nani mshindi wa urais, yaani 'electoral votes' kwa Kiingereza, Biden anazo jumla ya kura 253 huku Rais Donald Trump akiwa na kura 214. Hayo ni kulingana na baadhi ya vituo vya televisheni nchini humo.

Lakini kulingana na shirika la habari la Associated Press pamoja na Kituo cha Fox News, Biden anaongoza kwa jumla ya kura 264, ikiwa wamejumuisha pia kura kutoka jimbo la Arizona.

Mshindi anahitajika kupata kura maalum zisizopungua 270.

Joe Biden aliye na umri wa miaka 77 na ambaye pia ni makamu wa zamani wa rais huenda akawa rais mpya ikiwa atashinda kura katika jimbo la Pennsylvania au kwa kushinda majimbo mawili kati ya Georgia, Nevada na Arizona.

Infografik US Wahl 2020 Joe Biden Donald Trump

Nafasi ya Trump kushinda yazidi kudidimia

Nafasi ya Rais Trump kushinda inaonekana kuendelea kuwa ndogo, kwani anahitajika kupata ushindi kwenye majimbo ya Pennsylvania na Georgia na pia ampiku Biden katika majimbo ya Nevada na Arizona.

Katika jimbo la Pennsylvania ambalo lina jumla ya kura maalum 20, Biden amepunguza pengo lililokuwa kati yake na Trump, ambapo kwa sasa Trump yuko mbele yake kwa kura 18,000 pekee. Katika jimbo la Georgia, pia amepunguza pengo hilo na sasa Trump anamzidi kwa takriban kura 650 pekee.

Soma pia: Ushindi wanukia kwa Biden

Ilitarajiwa kuwa Biden ataendelea kupata kura zaidi katika majimbo hayo kadri kura zinavyoendelea kuhesabiwa, hasa ikizingatiwa maeneo yaliyosalia ni ngome ya chama cha Democratic, ikiwemo Philadelphia na Atlanta.

Lakini katika jimbo la Arizona, Trump pia alipunguza pengo lililokuwa kati yake na Biden, na sasa Biden amemshinda kwa kura 47,000 pekee, vile vile katika jimbo la Nevada Biden anaongoza tu kwa tofauti ya kura 12,000.

Soma pia Maoni: Trump ahujumu demokrasia

Rais Donald Trump akizungumza katika ikulu ya Marekani Novemba 5, 2020.
Rais Donald Trump akizungumza katika ikulu ya Marekani Novemba 5, 2020.Picha: Brendan Smialowski/AFP

Katika shambulizi lisilo la kawaida dhidi ya mchakato wa kidemokrasia, Rais Trump mwenye umri wa miaka 74 alidai akiwa katika ikulu kuwa wizi wa uchaguzi unafanywa dhidi yake, lakini bila ya kutoa ushahidi wowote.

"Tunadhani tutashinda uchaguzi kwa urahisi sana. Kutakuwa na kesi nyingi. Tunao ushahidi mwingi sana, ambao labda utaishia katika mahakama ya juu nchini. Tutaona. Kutakuwa na mashtaka mengi kwa sababu hatuwezi kuibiwa uchaguzi kwa njia hii.” Alisema Trump.

Aliendelea kuyarudia madai hayo kwa takriban dakika 15, na alipomaliza aliondoka bila kukubali kuulizwa maswali.

Soma pia: Uchaguzi wa Marekani wairarua demokrasia ya kiliberali

Biden ambaye awali aliwahimiza Wamarekani kuwa na subra mnamo wakati kura zikihesabiwa, alijibu kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema, "hakuna atakayeichukua demokrasia yao kutoka kwao.”

Mashtaka ya Trump yakataliwa Georgia na Michigan

Mnamo Alhamisi, timu ya kampeni ya Trump iliwasilisha kesi kadhaa mahakamani lakini majaji katika majimbo ya Georgia na Michigan walizitupa nje. Wataalamu walisema kesi hizo zilikuwa na nafasi finyu sana ya kuathiri matokeo ya uchaguzi, huku mshauri mkuu wa kisheria katika timu ya Biden Bob Bauer akiyataja mashtaka hayo kuwa mpango mpana wa kampeni ya kupotosha.

Soma pia: Nini itatokea matokeo ya uchaguzi yakipingwa?

Ikiwa ni siku ya tatu sasa baada ya uchaguzi kufanywa, maafisa wa uchaguzi katika majimbo ya Pennsylvania na Georgia wameelezea matumaini yao kwamba watamaliza mchakato wa kuhesabu na kujumuisha kura ifikapo Ijumaa majira ya Marekani. Lakini Nevada na Arizona, zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kwa siku chache zaidi.

Chanzo: RTRE