1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Marekani wairarua demokrasia ya kiliberali

Josephat Charo
5 Novemba 2020

Uchaguzi wa Marekani unararua mishono ya misingi ya demokrasia ya kiliberali. Ndivyo anavyosema mwandishi wa DW, Mimi Mefo Takambou, katika uhariri wake.

https://p.dw.com/p/3ku1C
US-Wahlen 2020
Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Uchaguzi wa Marekani unararua mishono ya misingi ya demokrasia ya kiliberali. Ndivyo anavyosema mwandishi wa DW, Mimi Mefo Takambou, katika uhariri wake.

Kimsingi kila kipengee cha sera ya kigeni ya Marekani katika miongo kadhaa iliyopita, iwe mizuri au mibaya, imetawaliwa na maadili mawili - kusimikwa kwa maadili ya kiliberali ya Marekani na kuendelezwa na kuheshimiwa kwa maadili ya demokrasia.

Marekani ilihalalisha vita vya nchini Vietnam, Iraq, Afghanistan na Libya kwa kudai ilikuwa mlinzi wa demokrasia, ambayo ina jukumu ya kuindeleza na kuilinda kote ulimwenguni. Maadili yayo hayo ya demokrasia sasa yamo hatarini nchini Marekani. Kukataa kwa Trump kutangaza wazi kwamba atakubali matokeo kama atashindwa, kunaibua hali ya wasiwasi kuhusu mustakhbali wa demokrasia ya kiliberali, demokrasia kwa maana ya mfumo wa utawala ambapo watu wa jamii wanamchagua kiongozi wao na uliberali kwa maana falsafa, mtazamo au msimao wa kupenda uhuru na usawa katika jamii.

Undumakuwili wa Marekani

Kwa hakika, kufikiri na kutenda kwa mtindo huo kunatakiwa kuachiwa nchi za Afrika au sehemu nyingine za ulimwengu ambako Marekani kwa miongo kadhaa imedai kufanya kazi bila kuchoka kufundisha nini maana halisi ya kuwa na demokrasia.

Itakumbukwa kauli za Trump kuhusu nchi kadhaa za Afrika na maadili yao. Tutafakari kuhusu undumakuwili. Nakumbuka kwa mfano mwaka 2018, kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Zimbabwe, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani wakati huo, Heather Nauert, alikuwa makini sana kutaja kwambaa uchaguzi huo uliipa nchi hiyo fursa ya kihistoria kusonga mbele zaidi ya mizozo ya kisiasa na kiuchumi ya miaka iliyopita na kuelekea mageuzi ya kidemokrasia.

Kamerun Journalistin Mimi Mefo
Picha: Mimi Mefo

Maswali kuhusu udanganyifu, uchakachuaji wa matokeo na machafuko ya baada ya uchaguzi, Marekani inaonekana kufuata mkondo tofauti kabisa ambao umekuwa ukishuhudiwa katika mataifa ambayo hayakuwa na sifa nzuri kuhusu kuheshimu demokrasia. Bila kujali matokeo ya uchaguzi wa Marekani, hii itakuwa mara ya kwanza kwa mgombea mwenye umri zaidi ya miaka 75 kuingia ikulu ya White House. Iwapo Biden atashinda atakuwa zaidi ya miaka 80 atakapokamilisha awamu yake ya kwanza ya miaka minne. Viongozi wengi wa kiafrika wamekaa madarakani katika umri ambao kimsingi wanatakiwa kustaafu kama wakuu wa nchi.

Shambulizi dhidi ya misingi ya uliberali

Marekani huenda ikatumbukia pabaya, iwapo mambo yatakwenda kama anavyobashiri Trump na kama atakataa kukubali kushindwa kwa misingi ya kufanyika udanganyifu katika mchakato mziwa wa uhesabuji wa kura. Lakini iwapo ataibuka mshindi, swali litakalobaki ni kama alishinda kwa sababu ya udanganyifu huo ambao amekuwa akiuzungumzia sana na kuueneza. Kanuni za msingi za demokrasia ya kiliberali kwa hivyo ziko katika hali taabani ya kukabiliwa na changamoto kubwa sana kutokana na jinsi uchaguzi huu wa Marekani na kipindi cha baada ya uchaguzi huo kinavyosimamiwa, bila kujali matokeo rasmi ya mwisho yatakavyokuwa.

Huku Waafrika kote ulimwenguni wakiendelea kushuhudia matukio na sinena inayoendelea kujitokeza Marekani mbele ya macho yao, watapata mtihani kuelewa maana ya demokrasia halisi. Kama ilivyo kwa Waafrika wengi wenzangu, mwenendo wa uchaguzi huu wa Marekani umeacha ladha ya uchungu kinywani mwangu.