1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden aapa kuimarisha msaada kwa Ukraine

22 Desemba 2022

Rais Joe Biden wa Marekani ameapa kuongeza msaada kwa Ukraine alipomkaribisha rais Volodymyr Zelensky katika ikulu ya Washington jana Jumatano huku akiahidi kuendelea kuimarisha uwezo wa Ukraine wa kujilinda.

https://p.dw.com/p/4LIb3
USA Biden Zelenskyy Washington PK
Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Volodymyr Zelenskyy kwamba Kyiv haitabaki peke yake, kwenye vita hivyo ingawa aliweka wazi kwamba kutakuwa na ukomo wa misaada itakayoendelea kupelekwa nchini Ukraine, ambayo mwisho wa siku haitaleta mgawanyiko miongoni mwa washirika wake.

Zelenzkyy ambaye yuko Marekani katika ziara ya kwanza ya nje ya nchi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari, kwa upande wake amesema hatakubali kushinikizwa kuingia kwenye mapatano ya amani yatakayoyaweka rehani maeneo ya Ukraine, ambayo miongoni mwake Urusi inadai ni ya kwake.

Soma Zaidi:White House: Zelensky kukutana na Biden mjini Washington

Amesema vita nchini mwake vitaisha wakati Ukraine itakapokuwa huru, pamoja na kulipwa fidia kufuatia uharibifu uliofanywa wakati wa uvamizi wa Urusi.

Kiongozi huyo wa Ukraine aidha ameishukuru Washington kwa kukubali kuwapa mfumo wa kisasa wa kujilinda na makombora angani wa Patriot ambao ni sehemu ya msaada wa kijeshi wa mabilioni ya dola uliotangazwa wakati wa ziara yake. Amesema, mfumo huo utawasaidia pakubwa kuimarisha ulinzi wa angani na kuongeza kuwa ni hatua muhimu katika kuandaa anga salama kwa Ukraine.

Russland l Rede von Präsident Putin, Sitzung des Vorstands des russischen Verteidigungsministeriums
Rais Joe Biden amemkosoa rais Vladimir Puti kwa kutotaka mazungumzo ya kumaliza mzozo huo.Picha: Sergei Fadeichev/Sputnik/Pool via REUTERS

Biden amkosoa Putin kwa kutotaka mazungumzo.

Biden awali, alimshutumu rais wa Urusi Vladimir Putin, akisema haonyeshi nia yoyote ya kumaliza vita dhidi ya Ukraine na kuongeza kuwa inaumiza kwa kile anachokifanya Putin cha kushambulia shule na vituo vya watoto yatima nchini Ukraine, huku kwa upande mwingine akimsifu Zelenskyy kwa utayari wake wa kufanya mazungumzo ya kusaka amani.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Biden alionya kwamba Urusi inajaribu kuyatumia majira ya baridi kama silaha ya vita, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Marekani na ulimwengu mzima kusikia moja kwa moja kutoka kwa kiongozi huyo kuhusu vita na umuhimu wa kusimama pamoja kwa mwaka ujao wa 2023.

Soma Zaidi:Ukraine yaomba msaada zaidi wa kijeshi

Ziara hii nyeti inafanyika miezi 10 tangu kuzuka kwa vita vilivyosababisha uharibifu mkuwa kwa pande zote mbili.

Kwenye mazungumzo yao, Zelenskyy alimpatia Biden medali ya kijeshi akisema wanajeshi wa Ukraine wamemuomba aifikishe medali hiyo kama zawadi kwa Biden, wakimtaja ni rais jasiri. Biden aliwashukuru wanajeshi hao, ingawa alisema hastahili.

Serikali ya Biden aidha inapana kutangaza vizuizi vipya kwenye bidhaa za teknolojia za wakala wa kijeshi wa Urusi, Wagner, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo viwili vyenye ufahamu na suala hilo, ikiwa ni jaribio la kudhibiti usambazaji wa vifaa hivyo, kutokana na dhima ya Urusi katika vita vya Ukraine, hatua inayoashiria uungaji mkono wa Marekani kwa rais Zelenskyy.