1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar: Baraza la Usalama lahimizwa kuweka vikwazo

5 Machi 2021

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Mynmar, Thomas Andrews amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo vya silaha na vya kiuchumi dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/3qEWf
Myanmar | Demonstration gegen Militärputsch: Polizisten und Soldaten bwegen sich auf Demonstranten zu
Picha: AP/picture alliance

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema inapaswa kuweka vikwazo dhidi ya mashirika ya gesi na mafuta ya Myanmar yanayodhibitiwa na wanajeshi ambayo ni msingi mkubwa kabisa wa kuingiza fedha nchini humo.

Katika ripoti yake mpya, mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa, ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuilinda demokrasia nchini Myanmar. Ameihimiza mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kuchunguza na kisha kufungua mashtaka ya uhalifu na ukatili dhidi ya binadamu uliotokea nchini Myanmar.

kwa upande wake balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema hatua madhubuti zichukuliwe ili kuwalinda raia wa Myanmar wanaokandamizwa kwa kuwa wanatetea demokrasia. Amesema Marekani ina wasiwasi juu ya mapinduzi ya Myanmar yanayosabisha umwagikaji wa damu. Bi Thomas Greenfield ameeleza kwamba badala ya watawala wa kijeshi kuheshimu sheria na kujiepusha na vurugu na hatimae kufuata njia ya mazungumzo, watawala hao wa wameongeza kasi ya kuwadhulumu watu wa Myanmar kwa miaka kadhaa sasa. Amesema hili halikubaliki kabisa.Wakati huo huo balozi mpya wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa Tin Maung Naing amejiuzulu, kutokana na kwamba mtangulizi wake Kyaw Moe Tun ambaye  alifutwa kazi na mamlaka ya kijeshi kuendelea kuiwakilisha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa Kyaw Moe Tun
Balozi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa Kyaw Moe Tun Picha: United Nations TV/REUTERS

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametangaza matukio hayo mapya katika safu ya kidiplomasia kwamba mjumbe huyo mpya wa Myanmar amewasilisha barua yake ya kujiuzulu na hivyo balozi wa Myanmar aliyekuwepo kwenye wadhfa huo Kyaw Moe Tun ataendelea na majukumu yake. 

Soma zaidi:UN: Myanmar yaendelea kushuhudia umwagaji damu

Watawala wa kijeshi waliowaondoa mamlakani viongozi wa kiraia wa Myanmar na kuchukua madaraka katika taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia mnamo Februari mosi, walikuwa wamemfuta kazi bwana Kyaw Moe Tun mnamo siku ya Jumamosi, mara baada ya mjumbe huyo kukaidi itifaki na kuomba msaada kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa kurudisha demokrasia nchini Myanmar. Majenerali wa kijeshi mara moja walimteua naibu wake, Tin Maung Naing, kuchukua mahala pake.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Myanmar Kyaw Moe Tun alimwandikia barua rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu kusisitiza kwamba mapinduzi ya kijeshi nchini mwake Myanmar yalikuwa si halali na kwa hivyo jeshi halina mamlaka ya kumwondoa kwenye wadhfa anaoushikilia katika Umoja wa Mataifa.

vyanzo: DPA/AFP