1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza la Usalama la UN kupigia kura azimio la Gaza

20 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kulipigia kura azimio lililocheleweshwa linalotaka mapigano kusitishwa kwa muda katika Ukanda wa Gaza, ambako hadi sasa wapalestina 19,000 wameuwawa wakiwemo watoto.

https://p.dw.com/p/4aNpu
USA, New York | TBaraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, MarekaniPicha: Yuki Iwamura/AFP/Getty Images

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamevutana kwa siku kadhaa kutafuta kauli moja na maneno sahihi ya kutumika, juu ya azimio hilo ambalo mchakato wa kulipigia kura ulisogezwa mbele mara kadhaa kuanzia siku ya Jumatatu. Kura hiyo hata hivyo inatarajiwa kufanyika leo Jumatano (20.12.2023)

Mwanadiplomasia wa Ufaransa ziarani Israel na Ramallah

Israel inayoungwa mkono na mshirika wake mkuu Marekani, iliyo na nguvu ya kura ya turufu katika baraza hilo imepinga kutumika kwa neno usimamishaji wa mapigano. Richard Gowan mchambuzi katika kundi la kimataifa la uangalizi wa mizozo amesema kwa sasa kila mmoja anasubiri kuona namna Marekani itakavyopiga kura yake.

Baraza la Usalama la UN laahirisha kura juu ya azimio la kusitisha mapigano Gaza

Mvutano huo ulioshuhudiwa wiki hii umejiri baada ya hatua ya Marekani mwezi huu licha ya shinikizo kutolewa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres la kusitisha mapigano, ilitumia kura yake ya turufu kupinga azimio la Baraza hilo iliyotaka mapigano kusitishwa kwa muda, ili kutoa nafasi kwa misaada kufikishwa katika eneo linalokumbwa na vita la Gaza, ambako Israel inaendelea na mshambulizi yake huko, tangu Kundi la Hamas lilipoishambulia Oktoba 7.

Hadi sasa sasa wapalestina zaidi ya 19,000 wameuwawa wakiwemo wanawake na watoto.

Herzog asema Israel iko tayari kukubali hatua nyengine ya usitishwaji mapigano wa muda

Isaac Herzog/ Israel
Rais wa Israel Isaac HerzogPicha: Heinz-Peter Bader/AP/picture alliance

Huku hayo yakiarifiwa jeshi la Israel limesema llimeyalenga kwa mashambulizi maeneo 300 mjini Gaza ndani ya siku moja mashambulizi yaliyowajumuisha wanajeshi wake wa angani ardhini na majini. Israel imesema wanajeshi wake wanazilenga taasisi za mawasiliano na maghala ya silaha ya Hamas katika mji wa Khan Younis.

Kwa upande mwengine Rais wa Israel Isaac Herzog amesema taifa lake liko wazi kukubali uwezekano mwengine wa kusitisha mapigano kwa muda Gaza.

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza huku miito ya usitishwaji vita ikitolewa

Wakati huo huo, kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh amewasili mjini Cairo hii leo asubuhi kwa mazungumzo ya vita vinavyoendelea katika ukanda wa Gaza. Taarifa ya kundi hilo imesema Haniyeh atajadili pamoja na maafisa wa Misri juu ya usitishwaji wa mapigano, ubadilishanaji wa wagungwa na kusitishwa kwa mzingiro wa wanajeshi wa Israel katika ukanda wa Gaza.

Kabla ya kuwasili Cairo alikutana mjini Doha na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian. Taarifa zaidi juu ya mkutano wao bado hazijatolewa.

Hamas: Hatutoshiriki upatanishi hadi hujuma zisitishwe Gaza

Hamas imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi kama kundi la kigaidi. Hali ya kibinaadamu mjini Gaza inazidi kuwa mbaya huku afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa akisema hatua zinazochukuliwa na Israel kukubali misaada kuingia huko hazitoshi na mahitaji ya watu wa eneo hilo linalokumbwa na mapigano, yanazidi kuongezeka.

Makubaliano ya kusitisha vita Israel-Hamas kurefushwa?

ap,afp,reuters