1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza la Usalama laahirisha kura juu ya vita ukanda wa Gaza

20 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyengine limeahirisha kura juu ya azimio jipya la kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza kufuatia ombi la Marekani.

https://p.dw.com/p/4aMtP
Marekani, New York | Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood akizungumza wakati wa kura juu ya kusitisha mapigano Gaza.Picha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Wanadiplomasia kadhaa wameliambia shirika la habari la dpa kwamba kura hiyo sasa imepangwa kufanyika baadaye leo.

Rasimu ya azimio lililowasilishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu limehimiza kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza ili kutoa fursa ya kupelekwa misaada zaidi ya kibinadamu.

Marekani, mshirika wa karibu wa Israel na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na yenye nguvu ya kura ya turufu, imepinga matumizi ya neno "kusitisha mapigano" kwenye azimio hilo.

Mwanadiplomasia mmoja kutoka nchi mwanachama wa Baraza la Usalama ameeleza kuwa kusogezwa mbele kwa kura hiyo kumefanyika ili kuishawishi Marekani kutotumia kura ya turufu kupinga rasimu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linahimiza kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza.