1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupitisha mswaada wa sheria za kuwalinda walemavu.

Zainab Aziz4 Februari 2005

Mataifa wanachama wa umoja wa mataifa na makundi tetezi ya haki za walemavu yameafikia makubaliano ya mswaada wa awali utakao zingatia haki za walemavu.

https://p.dw.com/p/CHhX

Mswaada huo iwapo utapitishwa na baraza kuu la umoja wa mataifa basi utakuwa ni mswaada wa kihistoria ambao utatumika kote duniani.

Mswaada wa awali ambao unatetea haki za walemavu kote duniani umeafikiwa na nchi wanacha wa baraza kuu la umoja wa mataifa na mashirika tetezi ya haki za walemavu na hivi karibuni mswaada huo utajadiliwa rasmi katika baraza la umoja wa mataifa.

Watetezi wa haki za walemavu wamesisitiza katika mswaada huo uzingatie haki ya walemavu ya kuwa huru na uwezo wa kupata ajira kama mtu mwingine yeyote miongoni mwa haki zingine za kibinadamu.

Iwapo mswaada huu utapitishwa na baraza kuu la umoja wa mataifa basi utafungua mwanya kwa walemavu kuweza kushiriki zaidi katika maswala ya kisiasa na ya kimaendeleo pamoja na kufurahia mazingira kama binadamu wengine.

Katika mataifa mengi haki za walemavu zimeendelea kupuuzwa jambo ambalo limewakosesha walemavu wengi nafasi sawa na wasiyo walemavu.

Wanaharakati wa kutetea haki za walemavu waliwasilisha malalamiko yao juu ya kukiukwa kwa haki za walemavu katika utoaji wa huduma bora za afya na kutengwa katika huduma za usafiri

Umoja wa mataifa unakadiria kuwa watu milioni mia sita kote duniani wanaishi na ulemavu wa aina fulani iwe ni upofu, uziwi au hali nyingine ya ulemavu.

Ripoti ya benki ya dunia inatafsiri kuwa mmoja kati ya watu watano miongoni mwa maskini milioni 450 duniani ni mlemavu hii ina maana kwamba walemavu ndio wanaokumbwa zaidi na hali ya umasikini hadi kufikia kiwango cha kutojimudu kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Venus Ilagan mwenyekiti wa walemavu duniani amesema kuwa haki sawa katika mambo mbali mbali inapaswa kutiliwa maanani katika maisha ya mwanadamu kama vile maswala ya kisheria, ya kijamii na mengineyo na wala siyo ulemavu wa mtu uwe ndio sababu ya kutopata haki hizo kikamilifu.

Katika mkutano huo Mathew Sapolin mkurugenzi mkuu wa miradi ya walemavu katika ofisi ya meya wa jiji la New York alisema kuwa, shida kubwa inayowakabili walemavu sio hali yao bali kutengwa na kunyanyaswa na jamii.

Aligusia umuhimu wa kuwepo mfumo bora wa elimu kwa walemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi za kazi. Marekani ikiwa ni mojawapo ya mataifa tajiri duniani inakabiliwa na asilimia 70 ya walemavu wasio na kazi hali inayosababishwa na ukosefu wa vifaa vya elimu kwa walemavu na mafunzo ya huduma za kazi mbali mbali vilevile swala la makaazi kwa walemavu bado halijakabiliwa vilivyo.

Nchi 119 wanachama wa umoja wa mataifa ziliorodheshwa katika mashauri hayo ambapo zaidi ya nchi wanachama 100 zimeunga mkono azimio hilo huku baadhi ya nchi wanachama zimetoa hoja ya kupinga azimio hilo. Rais Bush wa Marekani ametoa hoja ya kutaka swala la walemavu lishughulikiwe na mataifa binafsi.

Hata hivyo umoja wa mataifa umelaumiwa na baadhi ya mashirika tetezi ya walemavu kwa kutowashirikisha walemavu wenyewe moja kwa moja katika harakati za kupunguza umaskini.