1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baadhi waipinga Ujerumani kuipa silaha Ukraine

29 Aprili 2022

Watu kadhaa na wenye umaarufu mkubwa nchini Ujerumani wamesema kwamba hatua ya Ujerumani ya kupeleka silaha nzito nchini Ukraine inaweza ikautumbukiza ulimwengu kwenye Vita vya Tatu vya dunia ama mzozo wa kinyuklia.

https://p.dw.com/p/4AdId
Leopard 2A7V MBT
Picha: picture-alliance/Ralph Zwilling - Tank-Masters.de

Watu kadhaa na wenye umaarufu mkubwa nchini Ujerumani wamemuandikia barua ya wazi kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wakisema kwamba hatua ya Ujerumani ya kupeleka silaha nzito nchini Ukraine inaweza ikautumbukiza ulimwengu kwenye Vita vya Tatu vya dunia ama mzozo wa kinyuklia. Hapo jana bunge la Ujerumani liliidhinisha hatua hiyo iliyobadilisha mkondo wa sera za kivita za Ujerumani. 

Soma Zaidi: Ujerumani yavunjwa moyo na Ukraine

Sehemu ya barua hiyo imesema japokuwa ni dhahiri kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin amekiuka sheria ya kimataifa kwa kuishambulia Ukraine, lakini haihalalishi kwamba mzozo huo ugeuke na kuwa vita vya nyuklia. Barua hiyo imeongeza kuwa kwenye mzozo kama huo si kwamba mvamizi halisi tu ndiye atakayewajibika bali pia na wale wanaosaidia huku wakifahamu fika kwamba msaada huo unaweza kutumika kwa uhalifu.

Deutschland | Ukraine Krieg | Statement Olaf Scholz
Kansela Olaf Scholz amekuwa akisitasita kupeleka silaha nchini Ukraine, hatua iliyoibua ukosoaji kutoka ndani na nje ya Ujerumani.Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Ujerumani ilisitasita kuchukua uamuzi kama huo.

Barua hiyo hadi sasa imesainiwa na watu maarufu 28 ikiwa ni pamoja na mhariri mkuu wa jarida maarufu la masuala ya wanawake la Emma, Alice Shwarzer, mwandishi wa vitabu Martin Walser na mwandishi wa masuala ya sayansi Ranga Yogeshwar. Schwazer amesema barua hiyo inaweza pia kusainiwa na umma.

Kansela Scholz amekuwa akisitasita kuchukua hatua ya kupeleka silaha nchini Ukraine akiangazia sababu kama hizo zilizotolewa kwenye barua hiyo. Watu walioisaini wanasema walikuwa wanaunga mkono msimamo wa kansela huyo, wakitofautiana na wakosoaji wengi walimshutumu Scholz kwa kujihadhari kupita kiasi.

Nje ya Ujerumani, huko nchini Uholanzi waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss amefanya mazungumzo na maafisa wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC ya mjini The Hague, baada ya mapema leo kusema Uingereza itapeleka wataalamu Ukraine kusaidia kukusanya vidhibiti na kufungua kesi ya uhalifu wa kivita kwenye mahakama hiyo.  

"Kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria ni kuzuia pia ukatili zaidi unaoendelea Ukraine, kuwaonyesha watu iwapo wanafanya uhalifu wa kivita, iwapo wanatumia ubakaji kama silaha ya vita, watawajibishwa ili kuzuia ukatili zaidi. Tunaangalia njia zote zinazowezekana, ikiwa ni pamoja na namna ya kufungua mashitaka ya uhalifu wa uvamizi, lakini kipaumbele kwa sasa ni kukusanya ushahidi," alisema Truss.

Ukraine-Krieg Kiew | UN-Generalsekretär Antonio Guterres  und Präsident Selenskyj
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wakati wa ziara ya katibu mkuu nchini Ukraine Picha: Ukrainian Presidential Press/PA/dpa/picture alliance

Ukraine yashutumu shambulizi la Urusi mjini Kyiv.

Nchini Ukraine, rais Volodymyr Zelensky ameituhumu Urusi kwa kujaribu kuudhalilisha Umoja wa Mataifa baada ya kuivurumishia makombora Kyiv wakati wa ziara ya katibu mkuu wa umoja huo Antonio Guterres nchini humo. Zelensky amesema shambulizi hilo linazungumza mengi kuhusu tabia za Urusi kuelekea taasisi za kimataifa, kuhusu majaribio ya mamlaka za Urusi ya kuudhalilisha umoja huo na kila kitu kinachowakilishwa na taasisi hiyo na kwa maana hiyo inahitaji kujibiwa vikali.

Ujerumani nayo imesema kupitia msemaji wake Wolfgang Buechner imelaani vikali shambulizi hilo, ikisema kwa mara nyingine linaudhihirishia ulimwengu kwamba rais Vladimir Putin na utawala wake hawaheshimu chochote kinachohusiana na sheria za kimataifa.

Jijini London, maelfu ya wanajeshi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na mataifa mengine ya kaskazini mwa Atlantiki watashiriki katika msururu wa luteka za kijeshi kote barani Ulaya, katika kipindi cha wiki zijazo wakati mataifa ya magharibi yakiangazia namna ya kuizuia Urusi.

Soma Zaidi: Putin aamuru vikosi vya kujilinda viwe kwenye tahadhari

Waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema mazoezi hayo yatawakutanisha wanajeshi wa NATO na washirika wao, lakini pia vikosi vya pamoja maalumu vya kivita ili kuonyesha mshikamano na nguvu katika moja ya ushirika mkubwa kabisa wa kijeshi tangu Vita Baridi.

Mashirika: DW/APE