1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Usalama wa chakulaKimataifa

Mpango wa usafirishaji nafaka: Athari za uamuzi wa Urusi

19 Julai 2023

Urusi imetangaza kujiondoa kwenye mpango wa kimataifa wa usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi. Uamuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa hasa katika suala zima la usalama wa chakula duniani.

https://p.dw.com/p/4U6hp
Ukraine I Weizen Export
Picha: Andrew Kravchenko/AP/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyataja makubaliano hayo ya usafirishaji nafaka za Ukraine  kuwa ya matumaini. Kwa miezi kadhaa, makubaliano hayo yamekuwa yakirefushwa mara kwa mara, lakini sasa Urusi imetangaza wazi kuwa inajiondoa katika mpango huo, jambo ambalo linaweza kuwa na athari kubwa ulimwenguni.

Ukraine ni mojawapo ya wasambazaji wakubwa wa nafaka duniani. Kulingana na takwimu za Mpango wa Chakula Duniani WFP, nafaka za Ukraine hulisha watu wapatao milioni 400 duniani kote. Wakati uvamizi wa Urusi ulipoanza nchini Ukraine mnamo Februari 2022, nchi nyingi zilihofia kukabiliwa na tatizo la njaa hasa huko Afrika na Mashariki ya Kati.

Soma pia: Urusi yashambulia bandari za Ukraine baada ya kujiondoa katika mkataba wa usafirishaji salama wa nafaka katika Bahari Nyeusi

Nigeria Reis-Pyramide gegen den Hungersnot im Land
Wakulima wa NIgeria wakifanya maonyesho ya mchele katika kutaka kutafutia suluhu mzozo wa chakula nchini humo.Picha: Ubale Musa/DW

Bei ya vyakula ilikuwa juu hata kabla ya kuanza kwa vita vya Ukraine, lakini uvamizi wa Urusi ulisababisha ongezeko la bei duniani kote. Aidha, kitendo cha Urusi kuzuia usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi kilimaanisha kuwa mamilioni ya tani za nafaka zilikwama kwenye maghala ya Ukraine, zikiwa katika hatari ya kuoza. Kulingana na Umoja wa Ulaya, kudumisha mpango wa usafirishaji na usambazaji wa nafaka za Ukraine bado ni muhimu kwa usalama wa chakula duniani.

Je, nini kinaweza kutokea ikiwa mkataba huo utafikia kikomo?

Ikiwa Urusi itashikilia msimamo wake wa kutorefushwa kwa makubaliano hayo,  haifahamiki iwapo Ukraine itaendelea kusafirisha kiasi kikubwa cha nafaka duniani kote. Na hilo ni kutokana na gharama kubwa ya bima  kwa meli zote zinazotakiwa kuvuka Bahari Nyeusi. Bima hiyo muhimu hugharimu maelfu ya dola kwa meli hizo. Kampuni za usafirishaji zitasita kutuma meli zao kupitia eneo la vita ikiwa hakutokuwa na idhini ya Urusi.

Ukraine | Getreideexporte
Lori likishusha nafaka katika bandari ya Izmail nchini Ukraine (26.04.2023)Picha: Andrew Kravchenko/AP Photo/picture alliance

Inaweza pia kuwa vigumu kusafirisha nafaka hizo kwa njia ya barabara. Tangu kuanza kwa vita, Ukraine imeuza kiasi kikubwa cha nafaka kupitia nchi za mashariki mwa Ulaya, lakini kuna malori machache mno ya kuweza kusafirisha nafaka zote za Ukraine.

Soma pia: Zelenskyy: Mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi lazima uendelee

Aidha, wakulima katika baadhi ya nchi za mashariki mwa Ulaya, huchukizwa na kuona nafaka za Ukraine zikisafirishwa kupitia nchi zao, wakidai kuwa inapunguza usambazaji wa bidhaa za ndani na wanakosa uwezekano wa kuuza mazao yao wenyewe. Kutokana na hali hiyo, mapema mwezi huu, Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo vya kuagiza bidhaa hizo na kuamua kwamba nafaka zinaweza kusafirishwa tu kupitia nchi za Bulgaria, Hungary, Poland, Romania na Slovakia lakini haziwezi kuuzwa katika nchi hizo.

Mkataba huo wa usafirishaji nafaka unafanyaje kazi?

Mkataba huo unadhibiti mauzo ya nafaka kupitia bandari za Bahari Nyeusi zinazodhibitiwa na Ukraine za Odesa, Chornomorsk na Pivdenny. Meli zinazopitia Bahari Nyeusi kutoka na kuelekea mjini Istanbul, hupitia ukanda salama wa bahari na hukaguliwa katika kituo maalum kinachodhibitiwa na maafisa wa Uturuki na kuwajumuisha wakaguz wa Urusi, Uturuki, Ukraine na Umoja wa Mataifa. Vikosi kazi vya Umoja wa Mataifa vinahakikisha kuwa nafaka za Ukraine zinaweza kusafirishwa katika Bahari Nyeusi, na pia hurahisisha usafirishaji wa bidhaa za vyakula na mbolea za Urusi.

Mpango huo wa usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi ulisaidia kudhibiti na kupunguza bei ya vyakula duniani ambapo zaidi ya tani milioni 30 za nafaka na bidhaa nyingine za chakula zimesafirishwa mwaka huu kutokana na makubaliano hayo.