1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Antonio Guterres aunga mkono kupelekwa misaada nchini Syria

25 Juni 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaunga mkono kuurefusha muda wa mpango wa kupeleka misaada nchini Syria kupitia kwenye mipaka na nchi jirani.

https://p.dw.com/p/3eIg1
Coronavirus - UN-Generalsekretär Guterres
Picha: Imago/L. Rampelotto

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika ripoti yake kwamba kupeleka misaada nchini Syria kutokea nchi jirani kutahitaji kupitia vivuko vya Bab al-Salaam na Bab al-Haw kwenye mpaka baina ya Syria na Uturuki kwa muda wa miezi 12 ijayo.

Ujerumani na Ubelgiji ziliwasilisha ombi hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Guterres ameeleza kuwa zoezi hilo litahakikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kwa mamilioni ya raia ambao Umoja wa Mataifa utaweza kuwafikia. Hata hivyo Urusi na China zimesema mpango huo utahujumu uhuru wa Syria. Urusi ilishauri wazo la kupeleka misaada hiyo ya kibinadamu kwa kupitia mji mkuu wa Syria Damascus.

Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa/SANA

Mpango ulioko sasa ulioanzishwa mnamo mwaka 2014 unamalizika muda wake ifikapo tarehe10 mwezi ujao wa Julai. Kuanzia mwezi Mei idadi kubwa kabisa ya malori ya Umoja wa Mataifa yalipeleka mahitaji kwa kupitia mipakani. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa malori 1,781 yalivuka mpaka kupeleka misaada kutokea Uturuki. Misaada inayotolewa na shirika la chakula la Umoja wa Mataifa WFP inafikia dola milioni 4.5 kwa mwezi.

Bwana Guterres ameeleza kwamba sehemu ya kaskazini mashariki mwa Syria haikuweza kupata misaada  ya vifaa tiba kwa kupitia mpakani baada ya Urusi kufunga mpaka huo mnamo mwezi Januari. Mashirika yasiyo ya kiserikali yanapungukiwa misaada hiyo wakati ambapo inahitajika haraka na kwa kiwango kikubwa hasa wakati huu wa janga la corona na kwa hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono njia ya kupelekwa misaada kupitia mipakani pamoja na misaada inayotolewa na serikali ya Syria yenyewe.

Guterres amesema kutokana na hali ya uchumi kuzidi kuzorota nchini Syria, watu wapatao milioni 9 na laki  tatu kwa sasa hawapati chakula cha kutosha. Azimio la kurefusha muda wa kupeleka misaada ya  kibinadamu nchini Syria limepitishwa kwa kura 11. Nchi nne hazikupiga kura ambazo ni Urusi, China, Marekani na Uingereza.

Chanzo:/AFP