1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yaishutumu Israel kwa mauaji ya kimbari

11 Januari 2024

Afrika Kusini imeishutumu Israel kwa ''mauaji ya kimbari'', wakati wa kusikilizwa kwa kesi katika Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, ambayo Afrika Kusini imeifungua kupinga operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza.

https://p.dw.com/p/4b8Li
Niederlande | Internationaler Gerichtshof in Den Haag zum Nahostkonflikt
Picha: THILO SCHMUELGEN/REUTERS

Mawakili wa Afrika Kusini wamesema Alhamisi kuwa Israel inatumia ghasia ambazo hazijawahi kushuhudiwa kuharibu maisha ya Wapalestina, na wawakilishi hao wa kisheria wametoa wito wa kuwepo ulinzi wa kisheria wa maisha ya Wapalestina na imewataka majaji wa Mahakama ya ICJ, kuamuru kukomeshwa mara moja kwa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza.

Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amesema nchi yake inalaani vikali shambulizi la Hamas dhidi ya Israel, lakini shambulizi la Oktoba 7 la kundi hilo, haliwezi kuhalalisha Israel kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.

Akizungumza wakati wa kesi hiyo, Wakili wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini, Adila Hassim ameelezea vitendo vya ghasia vinavyofanywa na jeshi la Israel kama vile mashambulizi ya mabomu na kuzuia msaada wa kiutu, ni sawa na "vitendo vya mauaji ya kimbari."

''Kwa muda wa siku 96 zilizopita, Wapalestina huko Gaza wameuawa kwa silaha na mabomu ya Israel kutoka angani, nchi kavu na baharini.

Pia wako katika hatari ya kufa kwa njaa, upungufu wa maji mwilini, na magonjwa kutokana na kuzingirwa na Israel,'' alifafanua Adila.

Israel yapuuza tuhuma za Afrika Kusini

Waziri wa  sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Vusimuzi Madonsela balozi wa nchi hiyo Uholanzi
Waziri wa sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Vusimuzi Madonsela balozi wa nchi hiyo UholanziPicha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Kwa upande wake Israel imeyapuuza madai dhidi yake na kusema kuwa kesi hiyo haina msingi. Aidha, imeishutumu Afrika Kusini kwa kuwa ''mwakilishi wa kisheria'' wa wanamgambo wa Hamas, wakati ambapo mawakili wa Afrika Kusini wakiwasilisha kesi hiyo kwenye mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Lior Haiat ameielezea kesi ya Afrika Kusini kama moja ya vitendo vikubwa vya kinafiki katika historia.

Haiat amesema Afrika Kusini imepuuzia ukweli kwamba magaidi wa Hamas walijipenyeza Israel na kuwaua, kuwabaka na kuwateka nyara raia wa Israel, kwa sababu tu walikuwa Waisraeli, katika jaribio la kutekeleza mauaji ya kimbari. Israel inatarajiwa kuwasilisha hoja zake Ijumaa.

Wakati kesi hiyo ikisikilizwa, watu wanaoiunga mkono Palestina walikusanyika mbele ya mahakama ya ICJ, huku wengine wakiandamana kuelekea kwenye mahakama hiyo iliyoko The Hague, Uholanzi.

Mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya shauri hilo baada ya wiki chache zijazo. Aidha, kesi kuhusu madai ya mauaji ya kimbari inaweza kuchukua miaka kadhaa.

Maoni  ya Marekani na Lebanon  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema nchi yake inaamini kuwa hatua ya Afrika Kusini kuwasilisha madai hayo dhidi ya Israel, inavuruga juhudi muhimu za ulimwenu za amani na usalama. Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema wataifuatilia kesi hiyo kwa umakini.

Wizara ya mambo ya nje ya Lebanon imesema wana matumaini kwamba uamuzi wa haki utatolewa ambao unaakisi kuheshimu maadili na haki za binadamu, hasa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Afisa wa masuala ya kisiasa wa kundi la Hamas linalotawala Gaza, Basem Naim ameipongeza hatua ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, akisema wanatazamia kuona uamuzi wa mahakama unatoa haki kwa wahanga wa Palestina, kukomesha uvamizi dhidi ya Gaza na kuwajibishwa kwa wahalifu wa kivita.

Huku hayo yakijiri, Israel leo imeshambulia kusini mwa Ukanda wa Gaza, wakati ambapo Blinken amemaliza ziara yake ya kikanda yenye lengo la kuzuia vita kati ya Israel na Hamas kusambaa.

Kituo chake cha mwisho kilikuwa Cairo, Misri ambako alikutana na Rais Abdel Fatah al-Sisi, ambaye ni mpatanishi katika vita vya gaza ambavyo sasa vimeingia mwezi wake wa nne.

Kwanini Afrika Kusini inaishtaki Israel ICJ?