1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel imeanza The Hague

11 Januari 2024

Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, imeanza kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel, ambayo inaishutumu nchi hiyo kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4b6zk
Mafisa wa Afrika Kusini na Israel wakiwa ICJ
Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola, wakili Adela Hassim na maafisa wa Afrika Kusini wakiwa ICJPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Afrika Kusini ambayo inapinga kwa kiasi kikubwa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza, imeifungua kesi hiyo kwenye mahakama ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi.

Afrika Kusini inataka ICJ kuilazimisha Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi huko Gaza, ambapo inasema Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, na ICJ iyazingatie matendo ya Israel kwenye ardhi hiyo ya Wapalestina chini ya Mkataba wa Kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari uliopitishwa mwaka 1948.

Kulingana na mkataba huo, mauaji ya kimbari ni matendo yanayosababisha vifo vya watu wengi kwa lengo la kusambaratisha kwa sehemu au kwa jumla, taifa zima, kabila au jamiii ya watu wa rangi ama dini moja. Afrika Kusini na Israel zote zimesaini mkataba huo ambao unazilazimisha kutofanya mauaji ya kimbari na pia kuyazuia na kuyaadhibu.

Shambulizi la Hamas halihalalishi uvunjaji wa mkataba wa mauaji ya kimbari

Akizungumza katika ufunguzi wa kesi hiyo, Wakili wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini, Adela Hassim amesema shambulizi la Oktoba 7 la Hamas, haliwezi kuhalalisha Israel kuvunja Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema hatua yao ya kupinga mauaji ya watu wa Gaza, imewasukuma wao kama nchi kufungua kesi ICJ.

Hata hivyo, Israel imekanusha shutuma za kufanya mauaji ya kimbari, ikisema hazina msingi wowote na imesema kuwa inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Maafisa wanaoiwakilisha Israel kwenye mahakama ya ICJ
Mwanasheria wa Uingereza Malcom Shaw, mshauri wa kisheria wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel Tal Becker na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Israel Gilad Noam wakiwa kwenye mahakama ya ICJPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa anataka kuweka wazi mambo kadhaa kwamba Israel haina nia ya kuikalia kwa mabavu Gaza au kuwaondoa raia wake.

Soma zaidi: Kesi ya mauaji ya kimbari ya Afrika Kusini dhidi ya Israel inahusu nini?

''Israel inapambana na magaidi wa Hamas, na sio idadi ya Wapalestina, na tunafanya hivyo kwa kuzingatia kikamilifu sheria ya kimataifa. IDF inafanya kila iwezalo kupunguza vifo vya raia, huku Hamas ikifanya kila iwezalo kuviongeza kwa kuwatumia Wapalestina kama ngao ya binadamu dhidi ya mashambulizi,'' Netanyahu.

Netanyahu amekanusha madai hayo siku moja kabla ya mahakama ya ICJ kuanza kusikiliza kesi hiyo itakayodumu kwa siku mbili.

Afrika Kusini kutoa hoja Alhamisi, Israel Ijumaa

ICJ itasikiliza hoja za Afrika Kusini Alhamisi na majibu ya Israel Ijumaa. Uamuzi wa kuchukuliwa hatua za dharura unatarajiwa kutolewa baadae mwezi huu. Hata hivyo, Mahakama hiyo haitotoa uamuzi wakati huo, kuhusu madai ya mauaji ya kimbari.

Wakati huo huo, operesheni za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Gaza zinaulenga mji wa kusini wa Khan Younis pamoja na kambi za wakimbizi katikati ya eneo hilo. Shambulizi kubwa lililofanyika jana, liliangusha jengo la ghorofa mbili katikati ya mji wa Deir al-Balah, karibu na Hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa, na kuwaua takribani watu 20.

(DPA, AP, AFP, Reuters)