1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini: Wafuasi wa ANC wapinga muungano na DA

Bryson Bichwa6 Juni 2024

Wafuasi wa chama cha African National Congress, ANC, wameandamana jijini Johannesburg, kushinikiza viongozi wao wakatae kuingia katika muungano na chama cha Democratic Alliance, DA.

https://p.dw.com/p/4gkIX
Uchaguzi wa Afrika Kusini
Chama tawala cha ANC kwa mara ya kwanza katika miaka 30 kilishindwa kupata wingi wa viti bungeniPicha: ALAISTER RUSSELL/REUTERS
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
ANC ilishindwa kupata wawakilishi wengi bungeni ambapo sasa iinalazimika kuunda serikali ya muunganoPicha: Kyodo/picture alliance

Ni baada ya chama hicho tawala cha Afrika Kusini kufungua milango ya mazungumzo kwa chama chochote kilichopata viti bungeni kwenye uchaguzi uliopita na kinachonuwia kuunda serikali ya muungano itakayodumu kwa miaka mitano ijayo.

Maandamano haya yamefuatia kushindwa kwa chama cha ANC kupata wawakilishi wengi bungeni ambapo sasa kinalazimika kuunda serikali ya muungano na chama au vyama vilivyopata wawakilishi katika bunge la kitaifa. Lethabo Mmpo ni miongoni mwa watu walioandamana jijini Johannesburg wakipinga ushirikiano wa ANC na chama cha DA wanachodai ni chama cha kibaguzi. "Tuko hapa leo kuwasilisha wasiwasi wetu juu ya kukishirikisha chama cha DA katika serikali ya mseto, hatuamini kuwa kuna nafasi kwa chama cha kisiasa kinachopinga mabadiliko, chama ambacho kinadhani ni kawaida kuchoma bendera ya Afrika Kusini.

Wengine wameandamana pembezoni mwa mkutano maalum wa kamati kuu ya kitaifa ya chama tawala ANC, unaoendelea mjini Ekurhuleni na Esethu Hassane ni mjumbe wa kamati ya vijana wa ANC taifa aliyeungana na waandamanaji waliopiga kambi nje ya mkutano huo. "Tupo hapa kusema kwamba tunawaunga mkono katika maamuzi yoyote watakayoyachukua pasipo kukihusisha chama cha DA, kinachounga mkono mauaji ya kimbali dhidi ya watu wa Gaza, na kinachounga mkono ubaguzi wa rangi ndani ya Afrika Kusini.

Uchaguzi wa Afrika Kusini
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani John Steenhuisen akiwa na mwenyekiti wa chama cha ANCPicha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Japo baadhi ya wafuasi wa ANC hawakitaki DA kihusishwe kwenye serikali ijayo, lakini wachambuzi wa siasa na uchumi hapa Afrika Kusini wanadai kuwa, kukishirikisha DA kutavutia wawekezaji, kama alivyonieleza Peter Bigenda.

ANC kimeshafanya majadiliano na vyama mbalimbali ili kuunda serikali ya mseto, kikiwemo chama cha DA, EFF, IFP na kwa upande wa chama cha uMkhonto Wesizwe kiongozi wake Jacob Zuma, amesema wale ambao hawataki wazungumze kuhusu kumuondoa Rais Cyril Ramaphosa kwenye uongozi wa chama cha ANC hawataki majadiliano na MK.

"Huwezi kusema unataka kujadili lakini sio kuhusu rais wetu, hiyo ni nini? Hutaki tu kujadiliana, kwa sababu ungetaka tujadiliane ungesema hivi, tujadiliane na ikiwa suala hilo litajitokeza katikati mwa majadiliano yetu tutalijadili.

Uchaguzi wa Afrika Kusini
Chama cha uMkhonto Wesizwe kikiongozwa kimesema hakitafanya mazungumzo na ANC kama Ramaphosa bado ni raisPicha: Thuso Khumalo/DW

Hadi natuma ripoti hii mkutano maalum wa kamati kuu ya kitaifa ya chama tawala ANC ambao leo huenda ukategua kitendawili cha vyama gani vitaunda serikali ya mseto, ulikuwa bado haujamalizika na vyama vya kisiasa vina wiki mbili tu, kufanya makubaliano ili kuunda serikali ya muungano kabla ya bunge jipya kuketi na kuchagua rais, ambaye bado anaweza kuwa kiongozi wa ANC Cyril Ramaphosa.