1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Afrika Kusini kufanya luteka ya kijeshi na Urusi na China

17 Februari 2023

Afrika Kusini inatarajiwa kuanzisha luteka ya pamoja ya kijeshi na Urusi na China, hatua ambayo inaweza kuhatarisha uhusiano muhimu na washirika wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/4NduW
Südafrika | Gemeinsames Marinemanöver mit China und Russland
Picha: Chen Cheng/Photoshot/picture alliance

Siku ya Jumatatu meli ya kijeshi ya Urusi, ''Admiral Gorshkov'' ilitia nanga kwenye bandari ya Cape Town kabla ya kuanza luteka ya kijeshi ya majini inayoendeshwa na Afrika Kusini kuanzia Ijumaa tarehe 17 hadi 27 Februari.

Haya ni mazoezi ya pili kufanyika ambayo yanahusisha vikosi vya jeshi la maji la Urusi, Afrika Kusini na China. Mazoezi ya kwanza yalifanyika mwaka 2019. Uhusiano wa kihistoria kati ya Urusi na chama tawala cha Afrika Kusini, ANC unaweza kuelezea msimamo wa Rais Cyril Ramaphosa.

Ni luteka ya pili

Luteka hiyo inayoitwa ''Mazoezi ya Pili ya Mosi'', inayomaanisha ''moshi'' kwa lugha ya Kitswana, inaenda sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, na imewatia wasiwasi washirika wa Magharibi wa Afrika Kusini.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell alisema katika mkutano wake wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor kwamba mpango wa luteka hiyo la jeshi la majini halikuwa jambo zuri.

Südafrika | russische Militärfregatte Admiral Gorschkow im Hafen von Kapstadt
Meli ya kijeshi ya Urusi, ''Admiral Gorshkov'' kwenye bandari ya Cape Town, Afrika KusiniPicha: AFP/Getty Images

Naibu Mkurugenzi wa Mradi wa Taasisi ya Kimataifa ya kushughulikia Migororo, ICG barani Afrika, Pauline Bax, anasema ingawa serikali ya Afrika Kusini haijazungumzia chochote kuhusu luteka hiyo, ukweli ni kwamba kufanyika kwa mazoezi hayo wakati wa kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, ni jambo la kutatanisha sana.

Bax ameiambia DW kwamba wanadiplomasia wengi wa Magharibi wanaona mazoezi hayo ya kijeshi kama yanayopingana na madai ya Afrika Kusini ya kutoegemea upande wowote. ''Siwezi kusema kwamba imewakasirisha wanadiplomasia wa Magharibi, lakini wana wasiwasi na wanataka kufahamu msimamo wa Afrika Kusini,'' alifafanua Bax.

Awali Afrika Kusini ililaani uvamizi wa Urusi

Waziri Pandor, mara ya kwanza alilaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lakini Rais Ramaphosa alimlazimisha kubatilisha kauli yake na kumpokea waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov kwa heshima zote mwishoni mwa mwezi Januari.

Uhusiano kati ya Urusi na Afrika Kusini ni wa muda mrefu, kwani Urusi ilikiunga mkono chama cha ANC wakati wa mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo.

Joe-Ansie van Wyk, profesa wa Siasa ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, UNISA mjini Pretoria, anasema kwamba Afrika Kusini pia ina lengo la kuimarisha uhusiano wake na Urusi na China ambao ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambako bara la Afrika kwa muda mrefu limetoa wito wa kuwa na sauti zaidi.

Südafrika Besuch Außenminister Lawrow Russland
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Van Wyk ameiambia DW kwamba Afrika Kusini ni sehemu ya kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi za BRICS, inayozijumuisha Urusi, India, China na Brazil. ''Jambo la mwisho ni kwamba sisi ni washirika katika uundwaji wa BRICS, mataifa kutoka eneo la kusini mwa ulimwengu ambao tunajaribu kuanzisha eneo hili kukabiliana na nchi za Magharibi,'' alisisitiza Van Wyk.

Vita vya Ulaya havitishii usalama wa Afrika

Bax anasema vita vya Ulaya havitishii usalama wa Afrika na nchi za Afrika hazitaki kulazimishwa kuchagua upande wowote, ingawa vita vya Ukraine vilikuwa na madhara kadhaa barani Afrika, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta na vyakula. Hivyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Nchi nyingi za Afrika zinahisi kwamba zinaweza kuwa na washirika tofauti.hazitaki kuchaguliwa upande wowote ule. Na tatizo kwamba vita vya Ukraine vimeanzisha kile ambacho mataifa ya Magharibi yanahisi kwamba Afrika sasa inatakiwa kuchagua upande.

Kwa mujibu wa van Wyk, jinsi Rais Ramaphosa anavyoishughulikia hali ya urusi inaweza kuwa kosa na kuashiria kuondoka katika sera ya kigeni ya awali wa Afrika Kusini, ambayo inaangazia haki za binaadamu.

(DW)