1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

18 Januari 2019

Magazeti kadhaa ya Ujerumani yameandika juu ya shambulio la kigaidi lililotukia mjini Nairobi mapema wiki hii ambapo watu wapatao 21 waliuawa kwenye eneo kubwa la hoteli na ofisi nyingi

https://p.dw.com/p/3Bn0e
Kenia Angriff auf Hotel in Nairobi
Picha: Reuters/N. Mwangi

Neue Zürcher 

Shambulio la kigaidi lilifanyika tena mjini Nairobi baada ya magaidi kufanya mashambulio kwenye eneo la maduka la Westgate ambapo watu 67 waliuliwa mnamo mwaka 2013. Wasiwasi wa kutokea mashambulio mengine ulikuwapo miongoni mwa watu wakati wote nchini Kenya ila katika miaka mitatu iliyopita hofu iliondoka kwenye vichwa vya watu lakini ukweli ni kwamba watu walipaswa kuwa makini, hasa kutokana na taarifa za idara ya usalama kwamba mara kadhaa iliweza kugundua mpango wa magaidi.

Gazeti hilo la Neue Zürcher linakumbusha kwamba tangu mwaka 2011 wanajeshi wa Kenya wamekuwepo nchini Somalia kulisaida jeshi la nchi hiyo katika mapambano dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab. Kwa kufanya mashambulio mara kwa mara nchini  Kenya magaidi hao wanalipiza kisasi.

 die tageszeitung 

Polisi wa Kenya na vyombo vingine vya usalama safari hii vilifanya kazi kwa ustadi mkubwa. Katika mkasa wa Westgate polisi na wanajeshi walifyetuliana risasi wenyewe kwa wenyewe na kuhusu mkasa wa Garissa idara za  usalama zilichelewa kufika kwenye eneo la tukio lakini safari hii polisi na wanajeshi wa Kenya walifika  haraka kwenye eneo la tukio na kuanza kuchukua hatua.

Frankfurter Allgemeine

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limeyatupia macho matukio ya nchini Zimbabwe ambako linasema moto unawaka na kilichouwasha moto huo ni petroli. Gazeti hilo linatueleza kwamba uamuzi wa kupandisha bei ya petroli maradufu umesababisha ghasia nchini Zimbabwe. Matairi ya magari yamechomwa moto wakati rais Emmerson Mnangagwa akiwa nchini Urusi kuomba msaada. Hali ilizidi kuwa mbaya wakati kiongozi huyo alipokuwa anafanya mazungumzo mjini  Moscow. Maalfu ya watu walifanya maandamano katika mji mkuu Harare na katika mji wa Bulawayo ambao ni ngome kuu ya wapinzani. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limelinukulu shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International likisema kuwa watu wapatao wanane waliuliwa kwa kupigwa risasi na polisi. Watu wengine 200 walikamatwa.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hali ya maisha imezidi kuwa mbaya nchini Zimbawe ambapo mfumuko  wa bei umevuka asilimia 200. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limearifu kuwa  katika  ziara yake  nchini Urusi rais Mnangagwa alizungumzia juu ya mkopo na msaada wa kulifanya jeshi la Zimbabwe kuwa la kisasa.

Süddeutsche Zeirung

Gazeti la Süddeutsche linasema mshindi wa kweli wa uchaguzi huo ni Martin Fayulu, Gazeti hilo linadai kuwa na hati zinazothibitisha kwamba mgombea huyo wa upinzani alishinda uchaguzi. Gazeti hilo linasema matokeo ambayo hayakuchapishwa hadharani na tume ya uchaguzi yanaonyesha kuwa, aliyetangazwa mshindi bwana Felix Tshisekedi alipata asilimia 18.97 tu.

Gazeti hilo la Süddeutsche limemnukulu bwana Fayulu akisema kwamba zimefanyika njama za kuwadhulumu wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

die tageszeitung 

Gazeti la die tageszeitung linasema kwa watu wengi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ushindi wa Tshisekedi ni mpango mbadala wa rais Kabila. Baada ya dalili kuonyesha kuwa mgombea wa serikali Ramazan Shadary alikuwa anaelekea kushindwa, wakuu wa majeshi walifanya kikao cha dharura. Na muda mfupi baada ya kikao hicho rais Kabila aliwasiliana na Tshisekedi na katika siku hiyo hiyo tume ya uchaguzi iliahirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Gazeti hilo la die tageszeitung pia linatufahamisha kwamba nguzo ya mamlaka nchini Kongo ni idara ya usalama inayomtii rais Kabila. Rais huyo anayeondoka madarakani pia anawadhibiti magavana wa majimbo, idara ya upelelezi, fedha na raslimali za nchi.Gazeti hilo linasema hakuna kitakachobadilika kwa Kabila baada  ya Felix Tshisekedi kuingia madarakani.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo