1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

28 Septemba 2018

Mnamo wiki hii pamoja na mengine tunaangazia juhudi za kuzuia kuenea kwa jangwa zinazofanywa na Yacouba Sawadogo kutoka Burkina Faso. Na kutokana na hizo juhudi zake mwanaharakati huyo ametunukiwa tuzo mbadala ya Nobel. 

https://p.dw.com/p/35fSx
Simbabwe Wahl | Emmerson Mnangagwa, Präsident
Picha: picture-alliance/Photoshot/S. Jusa

die tageszeitung

Yacouba Sawadogo ni mkulima  anayetambulika kwa juhudi zake za miaka mingi  zenye lengo la kuligeuza eneo la Sahel kuwa la kijani tena kwa kupanda miti. Sawadogo mwenye  umri wa miaka 76 ni raia wa Burkina Faso aliyeanza shughuli za kupanda miti miaka 40 iliyopita na mpaka sasa amepanda hekta 40. Mbinu anayotumia ni kuchimba mashimo madogo madogo katika safu moja. Gazeti  la die tageszeitung linasema katika eneo ambako mvua ni haba mbinu hiyo ni muhimu na kwa njia hiyo ardhi inaweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu.

Mshindi wa tuzo mbadala ya Nobel Yacouba Sawadogo
Mshindi wa tuzo mbadala ya Nobel Yacouba SawadogoPicha: Right Livelihood Award/Mark Dodd

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limechapisha makala juu ya mgongano kati ya waziri wa fedha na rais nchini Zimbabwe. Wakati waziri huyo Mthuli Ncube anataka kuleta mageuzi rais Emmerson Mnangagwa anashauri kuwepo subira. Hadi hivi karibuni tu mfumo mpya wa fedha unaofanya kazi ulianza kuonekana baada ya waziri Ncube kusema kuwa Zimbabwe inahitaji kuwa na mfumo wake wa fedha madhubuti. Lakini aliwaambia wananchi wake kwamba kwanza Zimbabwe inapaswa kurejesha imani ili kuweza kuingiza fedha za kigeni lakini hatua za waziri huyo hazikufika mbali.

Gazeti hilo linaeleza kwamba rais Mnangagwa anataka Zimbabwe iendelee na mfumo wa fedha uliopo sasa, hadi hapo uchumi wa nchi utakapoimarika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kuwa wawekaji vitega uchumi watalazimika kuendelea kufanya biashara kwa kutumia hati maalumu za benki, utaratibu unaowatatiza wafanya biashara hao inapobidi kupata dola za kimarekani.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba kutokana na sera mbovu za utawala wa rais wa hapo awali Robert Mugabe uchumi wa Zimbabwe ulivurugika sana. Miaka 9 iliyopita Zimbabwe iliacha kutumia sarafu yake ya kitaifa-dola ya Zimbabwe baada ya kushindwa kuzuia mfumuko wa bei uliokuwa unaendelea kukimbia kama farasi aliyeshtushwa. Dola ya Zimbabwe ilipoteza thamani yake yote, na ndipo nchi hiyo ilipoanza kutumia dola ya Marekani.

Gazeti hilo linatilia maanani kuwa pendekezo la waziri wa fedha wa Zimbabwe Mthuli Ncube, juu ya Zimbabwe kuwa na sarafu yake ya kitaifa, linaungwa mkono pia na wataalamu wa masuala ya kiuchumi. Mtaalamu, Anthony Hawkins kutoka chuo kikuu cha Zimbabwe amenukuliwa na gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine akisema nchi zote zilizojaribu kutumia sarafu za nje hazikufanikiwa.

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki
Rais wa Eritrea Isaias AfwerkiPicha: picture-alliance/dpa/SPA

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linatupasha habari katika makala yake kwamba Eritrea inawatumia, kama mtaji, wakimbizi wa nchi hiyo walioko Ujerumani. Wakimbizi wa Eritrea wanatakiwa kulipa kodi kwa serikali yao ili kufidia gharama za huduma wanazopata kwenye balozi za nchi yao. Mkimbizi yeyote wa Eritrea anayetaka kupatiwa kitambulisho hana budi kulipa kodi kwa dikteta wa nchi hiyo. Mkimbizi kutoka Eritrea anahitaji kuwa na kitambulisho maalumu ili aweze kupatiwa hati ya kumwezesha kupata pasipoti ya wakimbizi nchini Ujerumani. Kitambulisho hicho maalumu kinatolewa na balozi za Eritrea tu na kwamba kila anayepatiwa hati hiyo lazima atoe asilimia 2 ya mapato yake kwa serikali kama kodi kutoka ughaibuni.

Gazeti la Neues Deutschland halikumalizia hapo bali linafahamisha zaidi juu ya kadhia hiyo na linaeleza kwamba kila mkimbizi wa Eritrea anayepata msaada wa fedha kutoka idara ya kijamii, hapa nchini Ujerumani anapaswa kulipa kodi ya Euro nane kila mwezi kwa dikteta wa nchi yake. Watu hao wanaikimbia nchi yao ili kukwepa kulitumikia jeshi la taifa. Kila kijana wa Eritrea anapaswa kulitumikia jeshi hilo kwa muda wa miezi 18 tu lakini vijana wengi wanatumikishwa kwa muda mrefu zaidi, kwa ujira usiokidhi mahitaji ya kila siku hata chembe! Gazeti la Neues Deutschland linasema baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeubainisha utaratibu huo kuwa ni utumwa nchini Eritrea.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo