1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Afghanistan: Mikoa zaidi yaingia mikononi mwa Taliban

11 Agosti 2021

Kundi la Taliban limechukua udhibiti wa mikoa mengine mitatu nchini Afghanistan, na kufikisha idadi jumla ya mikoa tisa kati ya 34 nchini humo ilioko mikononi mwa waasi hao.

https://p.dw.com/p/3yqC1
Afghanistan Kunduz Taliban Checkpoint
Picha: Abdullah Sahil/AP Photos/picture alliance

Kundi la Taliban limechukua udhibiti wa mikoa mengine mitatu nchini Afghanistan, na kufikisha idadi jumla ya mikoa tisa kati ya 34 nchini humo ilioko mikononi mwa waasi hao. Kuchukuliwa kwa mikoa hiyo mikuu ya Badakhshan, Baghlan na Farah kunaiongezea shinikizo serikali ya Afghanistan kufanya kila iwezalo ili kuzuia makali ya waasi hao. 

Wakati mji mkuu wa Kabul ukiwa bado hauko kwenye kitisho cha moja kwa moja cha kuchukuliwa na kundi la Taliban, mashambulizi ya waasi hao yanaendelea kuvikosesha usingizi vikosi vya usalama vya Afghanistan ambao kwa kiasi kikubwa, wanapambana nao bila ya usaidizi wa vikosi vya kimataifa vya usalama baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo.

Soma zaidi:  Marekani yaapa kuitenga Taliban iwapo itachukua madaraka

Kushadidi kwa mapigano kumewatia wasiwasi wakaazi wa mji mkuu wa Kabul. Mohammed Yaseer, ni mwanafunzi anayesomea taaluma ya utabibu.

"Iwapo Taliban inataka kuchukua udhibiti wa serikali na kutawala, basi lazima wachague njia nzuri ya kisiasa kufanikisha azma yao. Vita vitaleta uharibifu. Kama mwanafunzi, sina matumaini kabisa na maisha yangu ya baadaye. Sijui kitu gani kitafanyika."

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya amesema karibu asilimia 65 ya Afghanistan iko chini ya udhibiti wa kundi la Taliban wakati serikali ikiendelea kupoteza nguvu.

Akizungumza na waandishi wa habari, afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Ulaya amesema waasi hao wamechukua udhibiti wa karibu wilaya 230 kati ya 400 nchini humo. Afisa huyo alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa hana idhini ya kuzungumza na waandishi habari.

Afghanistan Präsident Ashraf Ghani
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani akihutubia wabunge mjini KabulPicha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Serikali ya Afghanistan na jeshi la nchi hiyo halijatoa tamko lolote juu ya hilo. Hata hivyo, Rais Ashraf Ghani amefika katika mkoa uliozingirwa wa Balkh ili kutafuta usaidizi kutoka kwa wababe wawili wa kivita ili kujaribu kuzuia mashambulizi zaidi ya Taliban.

Humayoon Shahidzada, mbunge kutoka mkoa wa Farah ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mkoa huo sasa uko mikononi mwa kundi la Taliban. Kadhalika, Hujatullah Kheradmand, mbunge kutoka mkoa wa Badakhshan amesema Taliban wameuteka mkoa huo.

Soma zaidi: Kufikia amani, Taliban yataka rais wa Afghanistan kuondoka

Katika mkoa wa Farah, wapiganaji wa Taliban wameiburuta barabarani maiti ya askari wa Afghanistan na kutamka kwa nguvu: "Mungu ni mkubwa."

Waasi hao wanaopigania kuweka sheria kali za Kiislamu, wameiteka mikoa sita chini ya muda wa wiki moja, ikiwemo mkoa wa Kunduz ambao ni moja ya mikoa mikubwa nchini Afghanistan.

Mafanikio ya Taliban katika kuiteka mikoa muhimu ya taifa hilo la kusini mwa Asia, kunaongeza uhitaji wa kuanzisha tena mazungumzo yaliyokwama kwa muda mrefu nchini Qatar ambayo huenda yakawa suluhu ya kumaliza mapigano nchini humo na kuundwa kwa serikali itakayojumuisha pande zote.