1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Marekani yaapa kuwatenga Taliban

Josephat Charo
10 Agosti 2021

Marekani imeapa kulitenga kabisa kundi la Taliban ikiwa litachukua madaraka kwa kutumia nguvu nchini Afghanistan. Umoja wa Mataifa ukitahadharisha kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na vitendo vya uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/3yoLP
US-Sondergesandter Khalilzad für Afghanistan
Picha: Getty Images/AFP/K. Jaafar

Mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya Afghanistan Zalmay Khalilzad amesafiri kwenda Doha, Qatar ambako Taliban wana afisi yao ya kisiasa, kuwafahamisha kuwa serikali yoyote itakayoingia madarakani kwa nguvu haitatambuliwa kimataifa. Khalilzad na wengine wana matumaini ya kuwashawishi Taliban warejee kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya Afghansitan wakati wanajeshi wa Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO wakiendelea kuondoka nchini humo.

Taliban wanadhibiti miji mikuu ya majimbo sita kati ya majimbo 34 na sasa wanaelekeza nguvu Mazar-i-Sharif, mji mkubwa kabisa wa kaskazini, ambao kuanguka kwake kutaashiria kusambaratika kabisa kwa udhibiti wa serikali katika eneo ambalo limekuwa likiwapinga sana Taliban. Vikosi vya serikali vinapambana na Taliban katika mikoa ya kusini ya Kandahar na Helmand, ambayo ni ngome yao.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya uwezekano wa uhalifu wa kivita. Kamishna Mkuu wa umoja huo anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu, Michelle Bachelet amesema idadi ya raia wanaouwawa inaendelea kuongezeka na ripoti zinaendelea kuchipuka za vitendo vya ukiukaji wa haki ambavyo vinaweza kuelezwa kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Msemaji wa Bachelet, Ravina Shamdasani, amesema tangu Julai 9 katika miji minne pekee ya Lashkar Gah, Kandahar, Herat na Kunduz, raia wapatao 183 wameuwawa na wengine 1,181 kujeruhiwa, wakiwemo watoto. Ravina amesema Bachelet anataka mapigano yakome mara moja Afghanistan kuepusha umwagaji zaidi wa damu.

"Taliban lazima wasitishe operesheni zao za kijeshi na kama pande zote haziterejea kwenye meza ya mazungumzo na kuafikiana makubaliano ya amani, hali mbaya ya sasa inayowakabili raia wengi wa Afghanistan itafanywa kubwa mbaya zaidi."

Afghanistan | Zwischen den Fronten | Taliban erobern Kundus
Taliban wakipiga doria mjini Kunduz Jumatatu Agosti 9, 2021Picha: Abdullah Sahil/AP/picture alliance

Wito wa msaada watolewa

Ghulam Bahauddin Jilani, waziri wa Afghanistan anayeshughulikia usimamizi wa majanga, amesema familia zipatazo 60,000 zimelazimika kuyahama makazi yao mikoani katika miezi miwili iliyopita kutokana na mapigano yanayoendelea, idadi ambayo amesema ni kubwa mno. Jilani amesema wameorodhesha familia 17,000 mjini Kabul zilizowasili kutokea mikoa mbalimbali, lakini wengi kutokea kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi. Ameyataka mashirika ya kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa kuwashinikiza zaidi Taliban waache ukandamizaji na ukatili dhidi ya raia, akisema watu hukimbia wilaya zilizotekwa na Taliban kwa sababu ya ukatili wao.

Ametaka msaada wa kiutu uongezwe Kabul na mikoani. "Tunaitolea wito jumuiya ya kimataifa namashirika ya kimataifa yasaidie na yashirikiane haraka iwezekanavyo katika kutoa chakula na mahitaji mengine muhimu ya msingi kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao."

Wakati haya yakiarifiwa Umoja wa Ulaya umesema leo kuwa raia wapatao 400,000 wa Afghanistan wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mzozo katika miezi ya hivi karibuni na idadi ya watu wanaokimbilia nchini Iran imeongezeka katika kipindi cha siku 10 zilizopita.

Mataifa sita ya Umoja wa Ulaya yametuma barua kwa rais wa halmashauri kuu ya umoja huo kumtahadharisha juu ya kusitisha safari za kuwarejesha kwao Waafghani ambao maombi yao ya uhamiaji yalikataliwa, licha ya mafanikio waliyopata wapiganaji wa Taliban katika kuyadhibiti maeneo ya nchi. Ujerumani, Austria, Denmark, Ubelgiji, Uholanzi, na Ugiriki zimesema katiakb arua hiyo kuwa kusitisha kuwarudisha kwao raia wa Afghanistan kutatoa ujumbe usio sahihi na huenda ukawashawishi Waafghan zaidi kuondoka nchini mwao kukimbilia nchi za Umoja wa Ulaya.

(afpe, ap,reuters)