1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Addis Ababa. Waethiopia kupiga kura kesho, huku baraza la haki za binadamu nchini humo likidai kuwa serikali inaendelea na usumbufu dhidi ya wapinzani na waangalizi wa uchaguzi huo.

14 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFDZ

Katika mkesha wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Ethiopia, chama cha kutetea haki za binadamu nchini humo pamoja na makundi ya vyama vya upinzani wamelalamikia kile wanachosema ni usumbufu unaofanywa na serikali dhidi ya wapinzani na kupinga tathmini ya rais wa zamani wa Marekani Bwana Jimmy Carter kuwa kampeni ziliendeshwa vizuri.

Licha ya uhakikisho kutoka kwa maafisa kuwa uchaguzi wa kesho utafikia katika viwango vya kimataifa, baraza la haki za binadamu nchini Ethiopia EHRCO, na chama cha United Ethiopia Democratic Forces UEDF vimesema matukio ya kukamatwa watu kisiasa na uchochezi wa serikali bado vinaendelea.

Makamu mwenyekiti wa wa chama cha UEDF Beyene Petros amesema kuwa hata kwamba imebaki siku moja kabla ya kupiga kura, wasimamizi wa chama hicho wanakamatwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi zao. Chama hicho pamoja na chama Coalition for Unity and Democrasy CUD, vimekataa hadi sasa kutia saini makubaliano ya kutokufanya ghasia siku ya uchaguzi pamoja na chama tawala.

Wakati huo huo Andargachew Tesfaye, mkuu wa baraza la haki za binadamu, amewaambia waandishi wa habari kuwa kundi lake linazuiliwa kuweka wachunguzi wake 1,644 katika vituo vya kupigia kura na viongozi wanaosimamia uchaguzi wakienda kinyume na uamuzi wa mahakama.