1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuckerberg akanusha Facebook kudhuru watoto makusudi

6 Oktoba 2021

Mwasisi na mmiliki wa kampuni ya Facebook, Mark Zuckerberg, amepinga vikali madai kwamba mtandao huo mkubwa wa kijamii unachochea migawanyiko na madhara kwa watoto kwa makusudi ili kujinufaisha kibiashara.

https://p.dw.com/p/41Ke2
Deutschland MSC 2020 | Mark Zuckerberg
Picha: picture-alliance/AA/A. Hosbas

Akijibu tuhuma nzito zilizoelekezwa kwake na kwa kampuni yake, Zuckerberg aliandika kwenye ukurasa wake wa Faceebok kwamba kuhoji kuwa kampuni inashadidia kwa makusudi maudhui ambayo yanawakasirisha watu kwa maslahi tu ya kutengeneza faida, hakuna mantiki. 

"Siijui kampuni hata moja ya mawasiliano mtandaoni ambayo inadhamiria kubuni bidhaa zinazowasirisha ama kuwafadhaisha watu. Misingi yote ya maadili, biashara na bidhaa inaelekeza upande mwengine." Alisema mwasisi na mmiliki huyo wa mtandao mashuhuri kabisa wa kijamii ulimwenguni.

Kauli ya Zuckerberg, ambaye siku ya Jumatatu (4 Oktoba) utajiri wake ulishuka ghafla kwa dola bilioni saba kutokana na kuzimika kwa mitandao ya Facebook, Instagram na WhatsApp kwa masaa kadhaa, ilikuja baada ya mvujisha siri, Frances Haugen, kuliambia baraza la Congress nchini Marekani kwamba mtandao huo unachochea migawanyiko, una madhara kwa watoto na lazima uwekwe haraka sana chini ya uangalizi.

"Facebook inayajuwa madhara inayosababisha"

Frances Haugen Facebook-Whistleblowerin
Meneja wa zamani wa bidhaa za Facebook, Frances Haugen, akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti ya Biashara, Sayansi na Usafirishaji ya Bunge la Marekani.Picha: Drew Angerer/Pool via AP/picture alliance

"Facebook inajuwa kwamba wazazi hawakuwahi kuvijuwa vitu hivi vya mitandao, ambavyo ni kama vileo, wanawapa watoto wao ushauri mbaya. Wanasema tu kwamba: "Kwa wasiache kutumia?" Kwa hivyo, utafiti wa Facebook wenyewe unafahamu kwamba watoto wanaelezea hisia za upweke na wanapambana na mambo hayo kwa sababu hawawezi kupata msaada hata wa wazazi wao. Sasa sifahamu kwa nini Facebook inayajuwa hayo yote na haiji kwenye vyombo kama Congress kuomba msaada wa kuyatatuwa matatizo haya." Alisema Haugen wakati akitowa ushahidi wake kwenye jengo la bunge, Capitol Hill, baada ya kuvujisha sehemu ya utafiti wa ndani wa Facebook kwa maafisa serikalini na kwa jarida la Wall Street. 

Meneja huyo wa zamani wa bidhaa za Facebook aliiambia kamati ya bunge kwamba anaamini kwa dhati kuwa bidhaa za Facebook zinawadhuru watoto, zinajenga migawanyiko na kudhoofisha demokrasia ya Marekani.

Akishadidia hoja yake ya kulitaka baraza la Congress kuchukuwa hatua haraka, Haugen alisema Facebook kamwe haitalitatuwa tatizo hili yenyewe, kwa kuwa nguvu zote zimo mikononi mwa mtu mmoja, akimtaja Zuckerberg, ambaye alisema anamiliki asilimia 55 ya hisa na maamuzi.

Haugen, mwenye umri wa miaka 37, ni mwanasayansi wa data kutoka Iowa aliyehitimu wa Chuo Kikuu cha Havard na ambaye kando ya Facebook, amezifanyia kazi kampuni za Google na Pinterest, anatajwa kuwa na uwelewa wa kina juu ya kile kinachoitwa "akili ya ndani" ya Facebook. 

Bado alitarajia kuendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Congress.