1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe na upungufu wa pasi za kusafiria

3 Julai 2019

Taifa la Zimbabwe linakabiliwa na upungufu wa hati za kusafiria pamoja na vibao vya namba za magari hatua inayowafanya raia kusubiri muda mrefu ili kuvipata. Si hilo tu bali njaa pia inatishia taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3LWvk
Simbabwe Wahl | Emmerson Mnangagwa, Präsident
Picha: picture-alliance/Photoshot/S. Jusa

Wakati haya yakiripotiwa, rais Emmerson Mnangagwaamesema hii leo kwamba taifa hilo linahitaji kuagiza tani 800,000 za mahindi kutokana na ukame ulioathiri mazao na kupunguza zaidi ya nusu ya mavuno, lakini akiahidi hakuna mtu yoyote atakayekumbwa na njaa.

Wazimbabwe waliokuwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya hali baada ya rais Mnangagwa kuchukua madaraka kutoka kwa Robert Mugabe baada ya mapinduzi ya mwaka 2017, bado hawajaweza kushuhudia mabadiliko hayo. Badala yake Zimbabwe imekumbwa na upungufu mkubwa wa dola ya Marekani, mafuta, mikate na umeme kukatika kwa masaa 15.

Mapema leo, mamia ya watu walikuwa wamefurika kwenye ofisi za kutolea pasi hizo zilizopo mjini Harare, wengine wakiwa wamefika ofisini hapo kuanzia saa 11 za alfajiri, wakiwa wamejikunyata kutokana na baridi kali, ili kupanga mstari wa kuomba pasi hizo. Baadaye waliarifiwa kuzifuatilia mwaka 2022.

Na hiyo inatokana na kukosekana kwa karatasi maalumu na wino vinavyotumika kutengeneza pasi hizo. Vifaa hivyo huagizwa kutoka nje, lakini kwa sasa hakuna fedha za nje za kuagizia.

Simbabwe Währung
Hali hiyo imesababishwa na kukosekana kwa fedha za nje za kuagizia vifaa vya kutengenezea pasi za kusafiria. Picha: Imago Images/Xinhua Afrika

Mmoja ya waliokuwa wamepanga mstari wa kuomba pasi, Bothwell Mhashu amesema anataka kutoroka kwenda Namibia kuishi na kaka yake mkubwa kutokana na hali mbali ya uchumi. Aliomba pasi tangu Junie 2018 na alitakiwa kuwa ameipata baada ya miezi mitatu. Mhashu alilalama kwamba hiyo si sawa.

Mwaka 2008 Wazimbabwe walilazimika kulala kwenye ofisi hizo za kutolea pasi ili wawe wa mwanzo ifikapo asubuhi kuanza mchakato wa maombi, katika wakati ambapo mzozo wa uchumi na ongezeko kubwa kabisa la bei kwa pamoja vikizidi kuishusha thamani ya sarafu ya taifa hilo, wakati huo chini ya Mugabe. 

Simbabwe Dürre Maisfeld
Njaa pia ni kitisho kingine kinachoinyemelea Zimbabwe kufuatia mvua kubwa za El NinoPicha: picture alliance/Photoshot

Pasi ya kawaida hugharimu dola ya Zimbabwe 53, ambayo ni sawa na dola 6.32 ya Marekani, wakati pasi ya dharura ambayo hutolewa katika kipindi cha masaa 24 ikigharimu dola za Zimbabwe 318. hata hivyo, hakuna pasi ya dharura ambayo hutolewa, labda tu kwa maafisa wachache waandamizi wa serikali.

Msajili mkuu Clemence Masango amekataa kuzungumzia suala hilo, alipoulizwa na shirika la habari la Reuters hii leo.

Lakini maafisa kwenye ofisi yake wamesema kulikuwa na mipango ya kuchapisha pasi kwa kutumia kiwanda cha kuchapisha kinachomilikiwa na benki kuu cha Fidelity Printers and Rifiners ili kupunguza rundo la zaidi ya maombi 50,000 ya pasi, lakini ni hadi vifaa vya kutengeneza pasi hizo vitakapoagizwa.

Nyakati hizi za giza zinawakumbusha Wazimbabwe enzi ngumu chini ya rais Mugabe, ingawa rais Mnangagwa anasema ni maumivu yatokanayo na mageuzi yanayoendelea.

Na wakati hayo yakiendelea, kitisho kingine ni njaa, ambapo rais Mnangagwa amesema wanahitaji kuagiza tani 800,00 za mahindi kufuatia upungufu wa mavuno. Shirika la Umoja wa Mataifa limesema hadi Wazimbabwe milioni 5, sawa na theluthi ya idadi ya watu watahitaji msaada wa chakula mwaka huu, kufuatia ukame uliosababishwa na mvua za El Nino.

Tanzania imekwishakubali kuiuzia hadi tani 700,000 za mahindi, hatua ambayo rais Mnangagwa amesema itachochea biashara baina ya mataifa hayo.