1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mnangagwa akatisha ziara baada ya Maandamano ya umma

Caro Robi
21 Januari 2019

 Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesitisha ziara Ulaya alikokuwa ahudhurie jukwaa la kimataifa la kiuchumi baada ya nchi yake kukumbwa na maandamano ya umma ambayo wanaharakati wanasema zaidi ya watu 10 wameuawa. 

https://p.dw.com/p/3BtFt
Weißrussland: 
Der belarussische Präsident Lukashenko und der Präsident von Simbabwe, Mnangagwa während der Begrüßungszeremonie in Minsk
Picha: Reuters/V. Fedosenko

Kupitia ukurasa wa Twitter, Rais Mnangagwa hajataja maandamano hayo wala ripoti hizo za vikosi vya usalama kutumia nguvu dhidi ya waandamananaji, bali amesema anarejea nyumbani kutokana na hali ya kiuchumi iliyoko nchini mwake na jambo atakalolipa kipaumbele ni ''kuifanya Zimbabwe tulivu, thabiti na kufanya kazi tena''.

Rais Mnangagwa ameonekana kuwa na mtizamo wa maridhiano ulio tofauti na ule wa msemaji wake George Charamba ambaye amesema msako dhidi ya waandamanaji ni kionjo tu cha yale yanayokuja huku kukiwa na madai ya kukamatwa kwa nguvu kwa viongozi wa upinzani, wanaharakati na raia.

Jeshi latumia nguvu kupita kiasi

Shirika lisilo la serikali la kutetea haki za binadamu limesema watu wasiopungua 12 wameuawa na 78 wametibiwa baada ya kupata majeraha ya risasi katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Umoja wa Mataifa umeishutumu serikali kwa jinsi ilivyoshughulikia maandamano hayo ya umma yaliyoanza tarehe 14 mwezi huu.

Zimbabwe Fuel Protests
Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini HararePicha: picture alliance/AP Photo

Mnangagwa amekuwa akishinikzwa kurejea Zimbabwe kutoka ziara ya wiki mbili aliyokuwa anafanya katika nchi za magharibi baada ya kuibuka ripoti kuwa vikosi vya usalama vimetumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wanapinga kuongezeka maradufu kwa bei ya mafuta.

Wiki iliyopita, maelfu ya watu waliandamana kupinga kuongezeka kwa bei ya mafuta kwa zaidi ya asilimia 100, inayotajwa kuwa bei ya juu zaidi ya mafuta duniani. Msemaji wa polisi Charity Charamba amewashutumu wahalifu kwa ghasia zilizojiri katika maandamano.

Katika jukwaa la kimataifa la kiuchumi la Davos alitarajia kuomba uwekezaji wa kigeni na mikopo kuisaidia nchi yake kujikwamua kiuchumi na kifedha, lakini ziara yake ilitarajiwa kuwa na changamoto kwani kuna mashaka miongoni mwa wawekezaji, mwaka mmoja baada ya kiongozi huyo kuchukua madaraka baada ya kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe.

Je, kuna tofauti kati ya Mnangagwa na Mugabe?

Utawala wa Mnangagwa uliongia madarakani ukibeba matumaini makubwa ya Wazimbabwe na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, umeshindwa kuboresha uchumi na unashutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya umma.

Evan Mawarire Pastor Aktivist
Mchungaji na Mwanaharakati Evan MawarirePicha: AFP/Getty Images/M. Safodien

Hali haijaonekana kubadilika kutoka utawala wa Mugabe kwani bado Wazimbabwe wanakabiliwa na ugumu wa maisha,kuongezeka kwa  mfumko wa bei, kutopatikana kwa bidhaa muhimu na wengi hawana ajira.

Zaidi ya watu 600 wamekamatwa katika msako huo akiwemo mchungaji mashuhuri na mwanaharakati Evan Mawarire ambaye aliunga mkono maandamano ya amani na sasa anakabiliwa na kesi ambayo huenda akafungwa miaka 20 jela.

Mawarire amesema inavunja moyo kuona utawala wa Mnangagwa hauna tofauti na wa Mugabe aliyelazimishwa kuondoka madarakani miezi 14 iliyopita.

Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe limelaani jinsi serikali ilivyoshughulikia maandamano, kushindwa kuudhibiti uchumi na kusema taifa hilo linapitia mojawapo ya vipindi vigumu zaidi katika historia.

Wakati huo huo, Afrika Kusini imesema haitaipa Zimbabwe mkopo wa dola bilioni 1.2 ifikapo Desemba. Msemaji wa wizara ya fedha ya Afrika Kusini Jabulani Sikhakhane amesema hawana kiasi hicho cha fedha kuwapa jirani yao Zimbabwe.

Mwandishi: Caro Robi/ap/Afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef