1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Ziara ya Xi Vietnam inatishia ushawishi wa Marekani?

Hawa Bihoga
12 Desemba 2023

China na Vietnam zimesaini mikataba zaidi ya 30 ikiwemo ule unaolenga kuendeleza uhusiano wa reli baina ya mataifa hayo. Huku Beijing ikikabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa Marekani katika taifa hilo la kikomunisti.

https://p.dw.com/p/4a5Al
Diplomasia | Rais wa China Xi Jinping akiwa na jopo lake alipokutana na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti Vietnam Nguyen Phu Trong
Rais wa China Xi Jinping pamoja na maafisa wa serikali akiwa katika mazungumzo na akiwa katika mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti Vietnam Nguyen Phu TrongPicha: Minh Hoang/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

China na Vietnam zimeahidi kuimarisha mahusiano yao na kusaini mikataba zaidi ya 30 ikiwemo ule unaolenga kuendeleza uhusiano wa reli baina ya mataifa hayo, huku Beijing ikikabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa Marekani katika taifa hilo la kikomunisti.

Hii ni ziara ya kwanza ya rais wa China katika taifa hilo na alikutana na kiongozi wa Chama tawala cha Kikomunisti cha Vietnam, Nguyen Phu Trong, katika siku ya kwanza ya ziara.

Katika taarifa ya pamoja mataifa hayo mawili yamesema yamekubaliana kujenga "jamii yenye mustakabali wa pamoja" na kuongeza kuwa ziara hiyo ilikuwa "alama ya kihistoria katika uhusiano wa pande mbili na  inachangia amani na utulivu na maendeleo katika kanda na dunia kwa ujumla wake".

Nchi hizo mbili zilitia saini mikataba zaidi ya 30, ikiwa ni pamoja na ahadi ya kuendeleza uhusiano wa reli kati ya Vietnam na China.

Vietnam kwa muda mrefu imekuwa ikifuata mbinu ya "diplomasia madhubuti", ikijitahidi kuwa na maelewano mazuri na China na Marekani.

Inaonesha wasiwasi wa Marekani kuhusu kuongezeka kwa uthubutu wa Beijing katika Bahari ya china Kusini, lakini pia ina uhusiano wa karibu wa kiuchumi na China.

Soma pia:Xi Jinping na Fumio Kishida walifanya mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa APEC, mjini San Francisco, nchini Marekani

Vietnam na China ambazo zote zimekuwa zikitawaliwa na vyama vya kikomunisti, tayari zimekuwa zina ushirikiano madhubuti wa kimkakati."

Hanoi na Washington waliboresha uhusiano wao katika kiwango cha kuridhisha, wakati Rais wa Marekani Joe Biden alipotembelea mwezi Septemba.

Ilifikiriwa kabla ya ziara hiyo Xi angeweza kuishinikiza Vietnam kujiunga na "Jumuiya ya Hatima ya Pamoja", ambayo inarejelea maono ya ushirikiano wa siku zijazo katika masuala ya kiuchumi, usalama na kisiasa.

Xi alisema katika makala iliyochapishwa Jumanne katika gazeti la Nhan Dan la Vietnam kwamba "mustakabali wa Asia hauko mikononi mwa mtu yeyote isipokuwa Waasia".

Mapokezi ya Xi katika mji wa Hanoi

Bendera za China na Vietnam zilipangwa njiani kutoka uwanja wa ndege hadi katikati mwa mji wa Hanoi siku ya Jumanne huku watu wakijitokeza kumlaki Xi nje ya hoteli aliyofikia.

Vietnam | Rais wa China Xi Jinping alipowasili Hanoi, Vietnam
Rais wa China Xi Jinping alipowasili Hanoi, VietnamPicha: Nhac Nguyen/Pool/AP/picture alliance

Xi atafanya mazungumzo Jumatano na Waziri Mkuu wa Vietnam Pham Minh Chinh na Rais Vo Van Thuong na kuweka shada la maua kwenye kaburi la kiongozi wa mapinduzi Ho Chi Minh.

Ziara hiyo inafanyika huku mvutano kati ya China na Ufilipino ukiendelea katika Bahari ya China Kusini baada ya matukio kadhaa yanayohusisha meli zao kwenye eneo ambalo mara zote huibua mizozo.

Ufilipino ilisema kuwa ilimwita balozi wa China siku ya Jumatatu na kuashiria uwezekano wa kumfukuza.

China inadai karibu eneo lote la Bahari ya China Kusini ni milki yake na imepuuzilia mbali uamuzi wa mahakama ya kimataifa kwamba madai yake hayana msingi wa kisheria.

Imekuwa ikipeleka boti zake kwa ajili ya kulinda doria kwenye njia ya majini yenye shughuli nyingi na imejenga visiwa bandia ambavyo imeviwekea vituo vya kijeshi ili kuimarisha usalama wake.

Soma pia:Kwanini Wamarekani zaidi wenye asili ya Asia wananunua silaha?

Wakati wa ziara ya Biden, Vietnam na Marekani kwa pamoja zilionya dhidi ya "tishio au matumizi ya nguvu" katika njia ya maji inayozozaniwa.

Vietnam ilikuwa mmoja wa wanachama kadhaa wa ASEAN waliokasirishwa na ramani mpya rasmi ya China iliyochapishwa mnamo Septemba ikionyesha mamlaka yake kwenye eneo hilo la baharini ambalo lina rasilimali nyingi.

Wachambuzi wanasema, kama ilivyokuwa kwa rais wa Marekani Joe Bidenmnamo Septemba, Xi anaweza kutafuta ushirikiano wa karibu zaidi na Vietnam ili kupata madini adimu yanayotumika katika utengenezaji wa vifaa vya umeme kama vile simu na betri za gari za umeme.

Vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali ya Vietnam viliripoti mwezi uliopita kwamba kampuni ya madini ya China Rare Earth Group Co. ilikuwa ikitafuta fursa za kufanya kazi na kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya Vietnam, Vinacomin.

Marekani na Vietnam zilikubaliana mwezi Septemba kushirikiana ili kuisaidia Hanoi kuhesabu na kuendeleza rasilimali zake za dunia adimu.