1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky kukutana na Guterres na Erdogan mjini Lviv

18 Agosti 2022

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky atakutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Alhamisi katika mji wa magharibi mwa Ukraine wa Lviv.

https://p.dw.com/p/4Fi2t
ARCHIV | Ukraine Kiew | Pressekonferenz Antonio Guterres und Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukraine Presidency/ZUMA Wire/IMAGO

Viongozi hao watatu watazungumzia makubaliano ya hivi karibuni yaliyofikiwa kati ya Urusi na Ukraine ya kuazisha tena usafirishaji wa nafaka ya Ukraine, hali tete katika kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Urusi, na juhudi za kusaidia kumaliza vita vilivyodumu kwa takribani miezi sita, kwa kutafuta suluhu ya kisiasa.

Guterres aliwasili Jumatano

Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, amesema Guterres aliwasiji Jumatano katika mji wa magharibi mwa Ukraine wa Lviv, uliopo karibu na mpaka wa Ukraine na Poland, na atazungumzia pia juhudi zake za jumla za kufanya anachoweza kimsingi kupunguza mzozo uliopo kadri inavyowezekana kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Erdogan kuizuru Ukraine tangu kuanza kwa vita vya Urusi. Rais huyo wa Uturuki anatarajiwa kufanya mkutano wa saa moja na Zelensky mchana huu, kabla ya wote wawili kukutana na Guterres.

Recep Tayyip Erdogan | türkischer Präsident
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: DHA

Mwezi uliopita, Uturuki na Umoja wa Mataifa zilisimamia kufikiwa kwa makubaliano ya kufungua njia kwa Ukraine kusafirisha tani milioni 22 za mahindi na nafaka nyingine zilizokwama katika bandari zake kupitia Bahari Nyeusi, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari.

Wakati huo huo, wizara ya mambo ya ulinzi ya Urusi imesema huenda kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kikafungwa, iwapo vikosi vya Ukraine vitaendeleza mashambulizi katika kinu hicho. Msemaji wa wizara hiyo Igor Konashenkov, amesema Urusi inaishutumu Ukraine kwa kupanga ilichokiita ''uchochezi'' katika kinu hicho wakati wa ziara ya Guterres.

Urusi: Ukraine imepanga uchokozi Agosti 19

''Agosti 19, utawala wa Kiev unajiandaa kwa uchokozi wa wazi katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambapo baadae Urusi itashutumiwa kwa kuanzisha janga la kibinaadamu katika kinu hicho,'' alisisitiza Konashenkov.

Hata hivyo, Ukraine imeyakanusha madai hayo. Shirika la habari la Urusi, RIA limeripoti kuwa wizara hiyo imesema hakuna silaha za kivita katika kinu hicho au katika wilaya za karibu. Kwa mujibu wa wizara hiyo, mfumo wa kukisaidia kinu hicho umeharibiwa kutokana na mashambulizi. Mwezi Machi, vikosi vya Urusi vilichukua udhibiti wa kinu cha Zaporizhzhia na kimekuwa kikishambuliwa mara kwa mara kwa makombora katika wiki za hivi karibuni. Urusi na Ukraine zimekuwa zikitupiana lawama ya mashambulizi hayo.

Ukraine Charkiw | Russischer Raketenabschuß aus der Region Belgorod
Makombora ya Urusi yameshambulia jimbo la Kharkiv Alhamisi ya 18.08.2022Picha: Vadim Belikov/AP Photo/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, watu wanne wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa leo asubuhi baada ya Urusi kulishambulia jimbo la Kharkiv. Gavana wa jimbo hilo, Oleh Synehubov amesema hadi sasa watu 18 wamejeruhiwa, miongoni mwao ni watoto wawili. Mashambulizi hayo yametokea saa chache kabla ya mkutano wa Guterres, Erdogan na Zelensky.

Huku hayo yakijiri, wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema leo kuwa meli nyingine iliyopakia chakula kutoka Ukraine, wakati huu ikiwa mahindi, inatarajiwa kuondoka katika Bahari Nyeusi. Meli hiyo itaondoka kwenye bandari ya Chornomorsk na sio bandari ya Odesa, ambako meli nyingi zenye nafaka ziliondokea. Kwa ujumla meli 25 zimeondoka Ukraine chini ya mkataba wa kusafirisha nafaka, zikiwemo meli tatu zilizoondoka jana Jumatano.

(AFP, DPA, AP, Reuters)