1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Hali ya Donbas ni mbaya sana

31 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema eneo la Donbas liko katika hali mbaya sana wakati vikosi vya Urusi vinasonga mbele kuelekea jimbo la mashariki ambalo limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

https://p.dw.com/p/4C5Jz
Ukraine | Kämpfe um Sjewjerodonezk
Picha: Aris Messinis/AFP

Akilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo, Zelensky amesema hali katika eneo la Donbas bado ni mbaya na kwamba Urusi inayalenga maeneo ya Sievierodonetsk, Lysychansk, Bakhmut, Avdiivka, Kurakhove na Slovyansk. ''Jeshi la Urusi linajaribu kuvikusanya vikosi vingi kwenye maeneo fulani ili kuweka shinikizo zaidi kwa wapiganaji wetu ambao wanalitetea eneo hilo,'' alifafanua Zelensky.

Aidha, Gavana wa jimbo la Lugansk Sergiy Gaiday amesema leo kuwa vikosi vya Urusi vimechukua udhibiti wa sehemu ya mji muhimu wa kiviwanda wa Severodonetsk ulioko mashariki mwa Ukraine, saa chache baada ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kufikia makubaliano ya kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi kwa zaidi ya theluthi mbili. Gaiday amesema sehemu ya Severodonetsk inadhibitiwa na Urusi na kwamba wanajeshi wa Ukraine bado wanaendelea kudhibiti baadhi ya maeneo.

Ukraine - Zerstörung nach russischen Angriffen
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa kwenye mji wa SeverodonetskPicha: Alexander Reka/picture alliance/dpa/TASS

Nayo mahakama ya Ukraine leo imewahukumu kifungo cha miaka 11 na nusu gerezani wanajeshi wawili wa Urusi ambao iliwakamata, baada ya kukutwa na hatia ya uhalifu wa kivita kutokana na kuushambulia mji wa mashariki mwa Ukraine.

Hukumu ya pili ya uhalifu wa kivita

Hii ni hukumu ya pili kutolewa dhidi ya makosa ya uhalifu ya kivita, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari. Wiki iliyopita, wanajeshi hao Alexander Bobikin na Alexander Ivanov, wote walikiri kuhusika na uhalifu huo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anatarajiwa kuizuru Uturuki, wiki ijayo kwa mazungumzo ya kuondoa vizuizi vya mauzo ya nafaka kutoka Ukraine, ambayo yamekwama kutokana na uvamizi wa Urusi.

Lawrow sieht "reale Gefahr" eines dritten Weltkrieges
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Attila Kisbenedek/AFP/Getty Images

Katika mahojiano na televisheni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amesema Lavrov atakayeongozana na ujumbe wa kijeshi, atawasili Uturuki Juni 8 kwa mazungumzo kuhusu suala la kufungua njia salama ambayo pia inajumuisha kusafirisha ngano kupitia Bahari Nyeusi.

Vikwazo vya Ulaya dhidi ya Urusi havitoshi

Ama kwa upande mwingine, afisa wa ngazi ya juu katika ofisi ya rais wa Ukraine amesema leo kuwa vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi havitoshi. Akizungumza mjini Madrid, nchini Uhispania, Ihor Zhovka, amesema kasi ya vikwazo hivyo kufikia sasa bado ni ndogo.

Huku hayo yakijiri, Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel ametangaza kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kuipatia Ukraine euro bilioni 9.   Michel amesema baraza hilo pamoja na kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7, zitaisaidia Ukraine na mahitaji yake ya haraka ya fedha.

Ulaya kuipatia Ukraine msaada wa euro milioni mia tano

Katika hatua nyingine meli moja ya mizigo imeondoka katika bandari ya Mariupol ikielekea Urusi, huku ikiwa na shehena ya chuma. Kiongozi wa jimbo la Donetsk amesema takribani tani 2,500 za chuma zimeondoka Mariupol kuelekea katika bandari ya Urusi ya Rostov-on-Don.

(AFP, Reuters, DW)