1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky arejea wito kwa Ukraine kupatiwa silaha nzito

17 Januari 2023

Ukraine imeyarai kwa mara nyingine mataifa ya magharibi kuongeza na kuharakisha msaada wa silaha kwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4MIMb
Ukraine-Krieg | Ukrainische Soldaten und Panzer an der Front bei Bachmut
Picha: Vladyslav Smilianets/REUTERS

 Wito huo umetolewa katika wakati hujuma za Urusi zinaongezeka upande wa mashariki ikiwemo shambulizi la hivi karibuni lililowaua watu wasiopungua 40 huko karibu na mto Dnipro.

Kupitia hotuba ya kila siku anayoitoa kwa taifa, rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky amerejea wito wake wa kuyataka mataifa washirika kuacha kujivutavuta na itume nchini Ukraine silaha zaidi na kwa haraka ili kuvisaidia vikosi vya taifa hilo kudhibiti kile amekitaja kuwa hujuma kutoka Moscow.

Matamshi hayo ya Zelensky ambayo amekuwa akiyatoa kila wakati tangu kuanza kwa vita yamechochewa na mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya Urusi huko wa mashariki.

Mwanzoni mwa wiki vikosi vya Urusi viliyalenga maeneo kadhaa kwa makombora mazito ikiwamo shambulizi moja lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 40 huko karibu na mto Dnipro.

Zelenskyy amelitaja shambulizi hilo kuwa juhudi za Urusi kujiongezea nguvu na udhibiti katika uwanja wa vita na ameyataka mataifa yanayoiunga mkono nchi yake kufanya maamuzi haraka ya kuongeza usambazaji wa silaha.

"Kilichotokea Dnipro, ukweli kwamba Urusi inajiandaa kwa hatua mpya za kujiimarisha kwa vita, na ukweli kwamba hali ya sasa kwenye uwanja wa mapambano inahitaji maamuzi mapya ya kuongeza silaha, yote hayo yanasisitiza vipi ilivyo muhimu kuunganisha nguvu zetu kwa mataifa yote washirika kuilinda Ukraine na uhuru na kuharakisha kufanya maamuzi” amesema rais Zelensky.

Wito kuelekea mkutano wa washirika wa Ukraine nchini Ujerumani 

Ukraine's President Zelenskiy attends a phone call with Britain's Prime Minister Sunak in Kyiv
Rais Volodmyr Zelenskyy wa Ukraine Picha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Yumkini rais Zelensky alikuwa analenga kutuma ujumbe wa wazi kabla ya mkutano wa mataifa rafiki kwa Ukraine utakaofanyika nchini Ujerumani wiki hii.

Mkutano huo wa siku ya Ijumaa kwenye kambi ya jeshi ya Ramstein magharibi mwa Ujerumani utakuwa jukwaa la mataifa ya magharibi kujadili nyongeza ya silaha kwa Ukraine.

Mawaziri wa Ulinzi wa mataifa karibu mataifa 40 washirika wa Ukraine na maafisa wengine waandamizi wa jumuiya za ulinzi ikiwemo NATO watahudhuria mkutano huo.

Katika miezi ya karibuni shinikizo linaongezeka hasa kwa Ujerumani kuongeza msaada wake wa silaha kwa Ukraine. Ukraine ingependelea kupatiwa vifaru vya kisasa chapa Leopard inavyohitaji sana kwenye uwanja wa vita.

Hata hivyo utawala wa Kansela Olaf Scholz inaonesha bado haujafikia uamuzi wa kutuma aina hiyo ya silaha nzito na hilo haliwafurahishi washirika wengine wa magharibi.

Rais wa Poland Andrzej Duda na mwenzake wa Lithuania wamekaririwa kwa nyakati tofauti hii leo pembezoni mwa mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi unaoendelea mjini Davos wakiitaka Ujerumani kuacha kujikokota na ipeleke vifaru vya Leopard nchini Ukraine.

Poland yenyewe imekwishasema itatuma aina hiyo vifaru angalau 14 kwa Ukraine.

Uingereza yatuma vifaru vya kisasa wakati mapambano yamepambana moto mashariki mwa Ukraine

Hapo jana Uingereza nayo ilitangaza kuwa itatuma aina nyingine ya vifaru mamboleo chapa Challenger 2 pamoja na vifaa vya kijeshi kwa Ukraine ikiwemo magari na makombora ya ulinzi wa anga.

Russland Verteidigungsminister Sergej Schoigu verkündet Umbau der Armee
Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei ShoiguPicha: Russian Defence Ministry/AP/picture alliance

Huko kwenye uwanja wa vita mashariki mwa Ukraine, duru zinasema Urusi imevurumisha zaidi ya makombora 70 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Makaazi zaidi ya 15 yamelengwa karibu na mji wa Bakhmut na mji mwingine jirani wa mkoa wa Donetsk wa Soledar eneo ambako vikosi vya Urusi na Ukraine wamekuwa vinnapambana vikali kwa wiki kadhaa.

Hii leo Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alivitembelea vikosi vya Urusi ndani Ukraine.

Alikutana na makamanda wa jeshi la Urusi na kusalimiana na wanajeshi ambapo amekaririwa akiwasifu kwa kusema "wanalinda utu wa ardhi ya nyumbani na ushindi unakaribia"